January 2, 2018


KIM


Na Saleh Ally
KIKOSI cha Simba kinaendelea kuongoza Ligi Kuu Bara baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ndanda FC, mechi iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Ushindi huo unakuwa ni wa saba kwa Simba dhidi ya timu hiyo ya Mtwara, lakini ni furaha kubwa kwa Kocha Mkuu wa Muda wa Simba, Irambona Masoud Djuma raia wa Burundi ambapo ndiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza akiwa bosi.

Djuma, kocha wa zamani wa Rayon Sports, amechukua nafasi hiyo baada ya uongozi wa Simba kuamua kuachana na Kocha Joseph Omog.

Omog ambaye aliwahi kubeba ubingwa na Azam FC bila ya kupoteza hata mechi moja, ameondoka akiwa ameiachia Simba historia nzuri kabisa ya kuibebesha ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports ambalo ndilo lililomponza baada ya kuvuliwa na Green Worriers inayoshiriki ligi daraja la pili.


Kocha huyo Mcameroon, ndiye aliyeirejesha Simba katika michuano ya kimataifa baada ya ubingwa huo wa Kombe la Shirikisho lakini ndiye aliyeirudisha Simba katika ushindani sahihi dhidi ya Yanga.

Kwa misimu minne mfululizo, ukiwemo ule mmoja ambao Omog alibeba ubingwa akiwa na Azam, Simba imekuwa ikishika kuanzia nafasi ya tatu hadi ya nne na moja na mbili zilikuwa ni Yanga au Azam FC.

Msimu wa mwisho, Omog aliipa Simba nafasi ya pili tena ikilingana pointi na mabingwa Yanga lakini tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, ikawaangusha.

Baada ya kuondoka Omog, Simba imempa nafasi hiyo Djuma lakini bado inaonekana ina hofu kwa kuwa Djuma anaweza asiwe na nguvu za kutosha kukiongoza kikosi hicho katika michuano ya kimataifa.

Huenda huko mbele lakini kwa timu za mwanzo, mfano Gendamarie ya Djibouti ambayo Simba wamepangiwa kuanza nayo, kocha huyo hatakuwa na presha hata kidogo.

Lakini Simba pia hawako katika mstari mbaya kwa kuamua kuangalia kocha gani anaweza kuwasaidia katika michuano hiyo ya kimataifa na ikiwezekana kubeba angalau ubingwa wa Tanzania Bara wanaousubiri kwa hamu na ikizingatiwa, hawana tena ubingwa wa Kombe la FA.

Awali ilielezwa anaweza kubaki Djuma na Selemani Matola akarejea na kuwa msaidizi wake. Lakini baadaye kumekuwa na majina ya makocha wengi kutoka nje na inaonekana Simba imepania kuleta Mzungu.

Majina mawili ndiyo yana nafasi kubwa, huenda akawa Kim Poulsen raia wa Denmark ambaye amekuwa akizifundisha timu za vijana za Tanzania na pia muda mfupi aliinoa Taifa Stars.

Kocha wa pili ni Goran Kopunovic, huyu ni raia wa Serbia aliyewahi kuinoa Simba kwa miezi kadhaa na kuiwezesha kubeba Kombe la Mapinduzi.

Makocha wote wawili ni wazuri lakini kumekuwa na taarifa ya mvutano mkubwa kati ya wajumbe wa kamati ya usajili kwa kuwa ni jambo la kawaida wao pia kujadili na kutafakari kabla ya kumpata mchezaji au kocha wanayemtaka. 

Kwa maana ya ubora, hakuna anayeweza kumpinga Poulsen ambaye hii ni mara ya pili, Simba inaonyesha nia ya kutaka kumpata. 

Lakini ni kocha ambaye alikuwa akizinoa timu za taifa tangu ametua nchini, hatujawahi kuiona nguvu yake katika kikosi cha klabu. Huenda linaweza kuwa ni chaguo zuri lakini litakuwa ni suala la kujaribu tena kwa Simba.

KOPUNOVIC

Maana yake itakuwa hivi; Simba inaweza kumjaribu Djuma kuona kama ataweza kwa kuwa aliiongoza Rayon Sports ya Rwanda kucheza michuano ya kimataifa, hivyo anaweza kuiongoza Simba.

Kumchukua Poulsen ni kujaribu mara ya pili, kwa kuwa naye hatujawahi kuiona nguvu yake katika ngazi ya klabu. Hivyo, Simba wataendelea kujaribu kwa makocha wawili ndani ya wakati mmoja.

Katika soka, suala la kujaribu lipo na wakati mwingine linakuwa ndiyo au hapana. Hivyo wakiamua kujaribu ni suala la kukubali matokeo yatakayofuatiwa hasa kama Poulsen atazidiwa na presha kwa kuwa ile ya timu ya taifa inakuwa chini sana.

Kopunovic, hata kama Simba itakuwa inajaribu, itakuwa ikifanya hivyo kwa nafasi kubwa sana ya kujiamini kwa kuwa ilifanya kazi na kocha huyo kwa nusu mwaka. 

Anaiweza presha ya Simba, kazi yake ilionekana ni nzuri na hata kuondoka kwake si kwamba alishindwa kazi badala yake alipotaka kulipwa ada ya usajili na Simba haina kitu, safari yao ikaishia hapo.

Kocha huyo aliitoa Simba kutoka nafasi ya nane na kuirejesha kwenye ushindani katika nafasi ya tatu, pili na kuirudisha tena kuwa na hadhi yake.

Usisahau, ndiye kocha aliyeanza kuwapa wachezaji wengi nafasi ya kucheza tena wale waliokuwa hawaaminiki na mmoja wao ni Said Ndemla.

Simba inaweza kuamua chochote kati ya haya matatu, lakini lengo litakuwa ni kujenga. Kibaya zaidi kamati inaweza kujichanganya kwa matakwa binafsi wakati wa kujadili masuala yao kuhusiana na kupata mtendaji sahihi.

Wajumbe wanapaswa kujadili mambo kwa maslahi ya Simba kwa lolote lile wanalotakiwa kufanya badala ya kuanza kufikiria urafiki wao na fulani au la.

Wakati Kopunovic akiondoka, alikorofishana na baadhi ya viongozi wa Simba na baadhi wako kwenye kamati, wengine hawapo. Sasa wale walio kwenye kamati, kama wanaona kuna sababu za msingi kumkataa kocha huyo wanatakiwa kuweka mezani zijadiliwe lakini si kufikiria uhusiano wao.

Hakuna urafiki au uadui wa kudumu hasa unapozungumzia kazi au biashara. Kikubwa viongozi wenye nafasi Simba wajue hiyo ni klabu ya watu na wamepewa dhamana, wasijisahau.


Matakwa binafsi weka kando unapofikia kujadili maslahi ya klabu kwa kuwa kufanya hivyo ni kuonyesha kuwa Simba ni sawa na gari lako au nyumba yako na unaweza kuamua unachotaka kufurahisha nafsi yako, hili ni jambo baya kabisa kwa kiongozi anayejielewa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic