February 23, 2018


YANGA inatarajiwa kukipiga dhidi ya Township Rollers FC ya Botswana katika Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua hiyo imekuja baada ya kuiondoa St Louis ya Shelisheli kwa jumla ya mabao 2-1 katika raundi ya awali.

Inayofuata ni Raundi ya Kwanza ya michuano hiyo, inavyoonekana Yanga itakuwa na kazi ngumu dhidi ya wapinzani wao hao wa Botswana kwa kuwa wanaonyesha wapo katika kiwango kizuri cha kuongoza ligi ya nyumbani kwao na pia kuiondosha El Marreck ya Sudan kwa jumla ya mabao 4-2.

Township Rollers FC
Jina lake la utani ni Tse Tala, The Blues, Popa-Popa, ilianzishwa mwaka 1965 ikijulikana kwa jina la Mighty Tigers kabla ya kubadilishwa jina baadaye.

Uwanja wake wa nyumbani mara nyingi ni Uwanja wa Taifa wa Botswana, pia imekuwa ikitumia Uwanja wa Chuo Kikuu cha Botswana na Uwanja wa Gaborone Station Fire Department.

Kwa sasa ndiyo kinara katika Ligi Kuu ya Botswana, inashiriki michuano hiyo ya Afrika baada ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu uliopita.


Timu hii inaongoza kwa kuwa na mataji mengi ya ligi kuu na mengine madogo ya ndani ya nchi, hiyo inamaanisha kuwa ni timu yenye sifa kubwa nchini humo.

Kama ilivyo upinzani wa Yanga na Simba, mabingwa hao nao wana upinzani wa jadi dhidi ya Gaborone United ambapo pindi wanapokutana mchezo wao unajulikana kwa jina la Gaborone Derby.

Kuthibitisha kuwa klabu hii ina nguvu nchini humo ndiyo inayoongoza kwa kuwa na wafuasi wengi kuliko klabu nyingine zozote katika mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter, Google + na Instagram.

Yanga inajulikana kwa kuvaa jezi za rangi ya njano na kijami, wapinzani wao hao ni maarufu kwa kuvaa jezi za njano pia pamoja na bluu.

Miaka ya hapo kati kuanzia mwanzoni mwa 2000, ilipitia kipindi cha kupanda na kushuka kabla ya baadaye kuamka na kufanya vizuri.

Mashabiki wengi 
Timu hii inaongoza kwa kuwa na mashabiki wengi na ambao wana nguvu katika soka la Botswana. Wanajulikana kwa kushangilia muda mwingi wa mchezo hasa wanapokuwa wanacheza kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Umaarufu wake umekuwa ukiongezwa na kitendo cha mashabiki wao kuvaa jezi za blue, njano na rangi ya dhahabu ambayo inatumiwa na timu hiyo, katika mitaa mingi ya Gaborone, ilipo timu hiyo.

Ndani ya Botswana, kuna matawi 52 ambayo yote yanatambulika na uongozi wa klabu na yana kamati yake maalum inayoyasimamia matawi hayo.

Haina rekodi ya kutisha kimataifa
Pamoja na kufanya vizuri katika ligi ya ndani, bado imekuwa haina matokeo mazuri ngazi ya kimataifa, rekodi zinaonyesha kuwa mwaka 2006 ilishiriki Kombe la Shirikisho na kufika Hatua ya 16 Bora, baada ya hapo ikashiriki Ligi ya Mabingwa mwaka 2011 na 2015, mara zote mbili iliishia hatua ya awali.

Mwaka 2017 inashiriki tena na imevuka hatua ya awali na sasa ipo Raundi ya Kwanza ikitarajiwa kuivaa Yanga. 


MATAJI YA TOWNSHIP ROLLERS

Ligi Kuu ya Botswana (14)
1979, 1980, 1982, 1983, 1984, 1985, 1987, 1995, 2004-05, 2009-10, 2010-11, 2013-14, 2015-16, 2016-17

Coca Cola Cup (6)
1979, 1993, 1994, 1996, 2005, 2010

Gilbeys Cup (3)
1991, 1992, 1996.

Orange Kabelano Charity Cup (5)
2002, 2004, 2006, 2014, 2015

Mascom Top 8 Cup (1)
2012


LIGI YA MABINGWA AFRIKA 2017/18 

Februari 10, 2018
Yanga 1-0 St Louis
Township 3-0 Al-Merrikh

Februari 21, 2018
St Louis 1-1 Yanga
Al-Merrikh  2-1 Township 

Raundi ya Kwanza
Machi 6, 2018
Yanga vs Township 

Machi 16, 2018
Township vs Yanga 


Ligi Kuu ya Botswana 2017/18
  P GD PTS  
1. Township Rollers 18 19 43  
2. Miscellaneous 19 11 34  
3. Jwaneng Galaxy 17 10 34  
4. Orapa United 19 6 32  
5. Gaborone Utd 18 8 26  

# Kuna jumla ya timu 16 


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic