SIMBA imerejea kwenye michuano ya kimataifa, tayari imeitoa Gendarmerie Nationale ya Djibouti kwa jumla ya mabao 5-0 katika hatua ya awali na sasa imeingia Raundi ya Kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ushindi katika michezo miwili ya nyumbani na ugenini lilionekana ni jambo la kawaida kwa kuwa wapinzani wao hawakuwa na nguvu kubwa, lakini sasa wanaenda kukutana na Waarabu kutoka Misri, Al-Masry.
Al-Masry wao wamefuzu hatua hiyo baada ya kuitoa Green Buffaloes ya Zambia kwa jumla ya mabao 5-2, mchezo wa kwanza Waarabu walishinda 4-0 lakini mechi ya pili wakafungwa 2-1.
Raundi ya Kwanza
Simba wataanzia nyumbani kukipiga na Waarabu hao kati ya Machi 6 au 7 na kurudiana Machi 16 au 18. Kuelekea mchezo huo kuna mambo kadhaa muhimu ambayo Wanasimba wanapaswa kuyajua juu ya wapinzani wao hao.
Wachezaji watatu hatari
Rekodi zinaonyesha Al-Masry siyo timu ya kutisha, inashika nafasi ya tano kwa umaarufu nchini Misri nyuma ya Al Ahly, Zamalek, Ismaily na El Ittihad El Sakandary, lakini kuna wachezaji watatu ambao wamekuwa na takwimu nzuri kwa msimu huu.
Mostafa Mohamed, huyu ndiye mchezaji pekee aliyefunga hat trick kikosini hapo katika Ligi Kuu ya Misri. Ahmed Shoukry ametoa asisti tano na ndiye anayeongoza kwa asisti kikosini hapo.
Ahmed Gomaa huyu ndiye kinara wa mabao kikosi kwake, amefunga mabao 11 na anashika nafasi ya tatu katika orodha ya wafungaji wa msimu huu hadi sasa, amekuwa msaada mkubwa kikosi chake kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu.
Imepoteza mechi tano
Al Masry imeshacheza mechi 23 katika ligi kuu ikiwa imeshinda 12, sare 6 na kupoteza 5, licha ya kuwa hawana kasi kubwa ya kufunga pia ukuta wao siyo mgumu sana kuruhusu mabao kwani wamefunga 36 na kufungwa 23.
Al Masry, mechi 10 zilizopita (ligi kuu)
El Masry 0-0 El Raja
Misr 1-4 El Masry
El Masry 0-0 El Gaish
Zamalek 0-1 El Masry
El Masry 2-1 Petrojet
Wadi Degla 0-0 El Masry
Smouha 3-2 El Masry
El Masry 6-3 Tanta
Enppi 2-1 El Masry
Al Nasr 2-3 El Masry
Ligi Kuu ya Misri 2017/18
P W D L Pts
1.Al Ahly 25 21 3 1 66
2. Ismaily 24 13 7 4 46
3. Zamalek 25 13 6 6 45
4. Al Masry 23 12 6 5 42
5. Smouha 24 11 5 8 38
# Zipo timu 18 katika ligi
Ilipotoka Al-Masry SC
Inajulikana kwa jina la utani la Bosi wa Canal, The Green Eagles na The Pharaonic Horus. Ilianzishwa miaka 97 iliyopita, inamiliki Uwanja wa Al Masry ambao unaingiza watu 17,000. Msimu uliopita ilifanikiwa kumaliza katika nafasi ya pili.
Makao makuu ya timu hii yapo katika Mji wa Port Said, tangu kuanzishwa kwake imeshinda mataji 22.
Jina la Al-Masry au El Masry linamaanisha ‘The Egyptian’ yaani Mtu wa Misri, ilianza kushiriki ligi kuu mwaka 1948. Ilikosa misimu miwili ya 1958/59 na 1959/60 ambapo kutokana na kushuka daraja. Pamoja na mapambano yote haijawahi kushinda taji la ligi kuu.
Rangi na nembo
Al-Masry inatumia zaidi jezi zenye rangi nyeupe na kijani. Nembo ya klabu ina alama ya mafarao ikiendeleza utamaduni wa nchi hiyo.
Michezo mingine
Klabu hii pia ina timu za michezo mingine ambayo imekuwa ikishiriki kwenye michuano mbalimbali, baadhi ya michezo hiyo ni handball, riadha, kuogelea, michezo ya gym, pool table, tenisi ya mezani na hockey.
Inamiliki kituo cha redio
Al-Masry FM ni kituo rasmi cha redio ambacho kinamilikiwa na klabu hii, inasikika mtandaoni, ilizinduliwa rasmi Desemba 28, mwaka jana, ndiyo klabu pekee ambayo inamiliki redio nchini Misri.
SOURCE: CHAMPIONI
Simba itawafunga hawa
ReplyDelete