Kocha Msaidizi wa Simba, Mrundi, Masoud Djuma, amefunguka kuwa ni lazima waifunge Mbao FC ili wasikaribiwe na watani zao wa jadi Yanga kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Simba ambayo inaongoza ligi kuu ikiwa na pointi 42 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 37, Jumatatu ijayo itapambana na Mbao FC kwenye mchezo wa ligi hiyo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Taifa, Dar.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Simba ililazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Mbao kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Masoud ambaye ni raia wa Burundi, amesema: “Mechi dhidi ya Mbao ni ngumu na lazima tushinde, hatuna kingine zaidi ya hicho, licha ya ugumu huo hatufikirii kutoa sare wala kufungwa kwani hivi sasa hatutaki kupoteza nafasi tunazozipata uwanjani. Tunataka kuzitumia zote kufunga mabao.
“Inafahamika wazi kwamba ili msimu ujao tushiriki michuano ya kimataifa ni lazima tuwe mabingwa wa ligi kuu kwani tumebakiwa na nafasi hiyo tu baada ya kuondolewa kwenye Kombe la FA.
“Kutokana na umuhimu wa mchezo huo, ndiyo maana kule Djibouti hatukucheza kwa nguvu kwa sababu tulikuwa tumeshafunga mabao mengi hapa nyumbani, hivyo haikuwa na maana sana kujichosha wakati mbele yetu tunatambua kwamba tuna mechi nyingi zenye faida kuliko ile.”
0 COMMENTS:
Post a Comment