February 23, 2018







NA SALEH ALLY
YANGA na Simba zimefuzu kucheza hatua nyingine ya michuano ya kimataifa chini ya Shirikisho la Soka la Afrika (Caf).


Yanga imesonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya mechi mbili dhidi ya St Louis ya Shelisheli ikiwa imefanikiwa kushinda 1-0 nyumbani Dar es Salaam na sare ya 1-1 ugenini.


Simba ikasonga mbele kwa kuitwanga Gendamarie ya Djibouti kwa jumla ya mabao 5-0 ikiwa imeshinda 4-0 jijini Dar es Salaam na 1-0 ugenini.


Timu mbili kubwa za Tanzania ndiyo wawakilishi wa nchi yetu na sasa zimefuzu kucheza hatua nyingine. Inawezekana si kila nchi timu zake zinazoshiriki michuano ya kimataifa zimefanikiwa kupiga hatua, hivyo hili ni jambo la kujivunia.


Simba na Yanga, zote zinaiwakilisha Tanzania au zinapeperusha bendera katika michuano hiyo ya kimataifa na zote mbili sasa zinaingia kwenye hatua ngumu zaidi, kwa kuwa zinakutana na timu ambazo zina uwezo zaidi na hauwezi kufananisha ya Sheliseli au Djibouti.

Simba itakutana na Al Masry kutoka Misri, Yanga inakutana na Township Rollers ya Botswana ambayo pia si timu laini kwa kuwa imevuka baada ya kuitoa El Merreikh ya Sudan ambayo inajulikana kwa ubora wake.

Kwa sasa hatua zilizofikia Simba na Yanga, huenda ni wakati mzuri sana wa kuungwa mkono na Watanzania kuliko wengine kutoka nje ya Tanzania. 

Kuliibuka mjadala wa mashabiki wa soka kwenda kwa wingi kuiunga mkono Yanga wakati ikicheza mechi yake ya kwanza na St Louis na siku inayofuata waende kwa wingi kuiunga mkono Simba ikiwavaa Gendamarie.

Lakini kabla hata ya mechi hizo, mjadala ukazidi kupaa na kuwa mkubwa. Kwani asilimia kubwa ya mashabiki wa kila upande walionekana wakipinga kwa nguvu kubwa sana wakikataa katakata kuunga mkono upande mmoja.


Mfano Simba walikataa katakata baada ya msemaji wao, Haji Manara kusema waende uwanjani kuiunga mkono Yanga. Baada ya mashabiki wengi Simba kuonyesha wazi hawataki, wale wa upande mwingine nao wameendelea kupinga nao hawataunga upande mwingine.

Ushabiki ni furaha, tena hii inakuwa ni furaha binafsi na kuna sababu ya kuamini kwamba wakati mwingine unaweza kusitisha furaha yako kwa ajili ya kuliunga mkono taifa lako.

Kama shabiki hawezi kabisa kuiunga mkono Yanga kwa kuwa yeye ni Simba, basi anaweza asiiangushe au kuisakama Yanga. Akaamua kuliunga mkono taifa lake kwa kukaa kimya kabisa akiachana na “biashara” ya Yanga wakati huo.


Kwa yule wa Simba, naye anaweza akaamua kukaa kimya, kutokwenda uwanjani badala ya kusema maneno ya kukatisha tamaa au kwenda uwanjani kuwazomea Yanga wakicheza mechi ya kimataifa wakiwa wawakilishi wa Tanzania.


Nawakumbusha tena kwamba kuna mashabiki wengi sana wa soka wamekuwa wakizishabikia timu hizo hasa Yanga na Simba kwa mapenzi ya maonyesho. Yaani wanashabikia wakitaka kuwaonyesha watu wengine wao wanazipenda sana Yanga au Simba, jambo ambalo si sahihi na ulimbukeni wa mambo.


Furaha yako haitakiwi kukaguliwa na wakati mwingine ni vizuri kuamua unachotaka bila ya hofu kwamba fulani anaweza akakuona wewe ni msaliti. Unapoona unaweza kuwa mzalendo, basi kuwa huru. Kwani kuna viranja wa kukagua mapenzi kwa Yanga na Simba?


Hao wanaotaka kukagua, hasa wanaotumia neno “mwenzetu” wengi huwa ni wababaishaji na wanapenda kuzitumia Yanga na Simba kama sehemu ya mtaji kuendesha maisha yao na wala si mapenzi ya dhati.


Ndiyo maana umewahi kusikia mashabiki wanazihama klabu hizo eti kwa kuwa siku hizi watu maarufu wa klabu hawawajali sana, wanakwenda kule kuliko na maslahi wakati wamewahi kuonekana wakizililia hadharani.


Tujifunze, uzalendo ndiyo utaifa wenyewe. Linapokuwa suala la utaifa, basi bila ya kujali ni yupi, tuungane kuonyesha uzalendo kwa taifa letu.



1 COMMENTS:

  1. Tatizo hata wewe katika kulielezea jambo hili umeingiza ushabiki. Uwe mkweli kwa Muumba wako. Baada ya kiongozi huyo wa Simba kuwataka washabiki wa Simba kutowazomea Yanga kwenye game yao, Kiongozi mmoja wa Yanga ndiye alitokea kupinga vikali na kusema wao hawatashangilia Simba hata siku moja. Baada ya hapo ndipo washabiki wengine wakaingilia kati mjadala huo kila mmoja akivuta kwake. Ndipo wengine waliandika kulani kauli ya yule kiongozi wa Yanga kukataa jambo la jema la kizalendo.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic