BILA SHAKA SASA LAUDIT MAVUGO ATAKUWA AMEPATA AHUENI
Na George Mganga
Mshambuliaji wa klabu ya Simba, Mburundi, Laudit Mavugo, bila shaka atakuwa ameanza kupata matumaini ya kujiamini na kujipanga vizuri kuelekea michezo ijayo katika Ligi.
Mavugo alionesha kupambana katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry uliokwenda suluhu ya bila kufungana.
Mburundi hiyo alionesha kiwango kizuri kilichopelekea kosakosa kadhaa kwenye lango la Waarabu, na kupelekea kuongeza hamasa ndani ya kikosi cha Simba baada ya kuingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Yusuph Mlipili.
Kiwango hicho kiliwaziba mdomo hata wale waliokuwa wanamponda wakianza kumsifia kwa sifa kedekede.
Hivi karibuni mchezaji huyo amekuwa akitupiwa lawama nyingi na mashabiki wa timu hiyo, ikifikia mpaka hatua baadhi wakimtaka akatafute maisha ya soka pahala pengine nje ya Simba.
Mavugo amekuwa akiingia kutokea benchi tofauti na msimu wa kwanza alivyojiunga na wekundu hao wa Msimbazi alikuwa akianza kikosi cha kwanza.
Mshambuliaji huyo amekuwa na ukame wa mabao kwa siku za hivi karibuni, jambo ambalo limesababisha mashabiki wa Simba washindwe kumvutia subira, kama ilivyo desturi ya mashabiki wengi wa soka la Tanzania.
Bila shaka sasa Mavugo atakuwa amepata ahueni ya kuweza kupumua kidogo kutokana na namna alivyopambana kwenye mchezo wa Jumamosi iliyopita dhidi ya Al Masry.
Mavugo anapswa kujipanga vizuri na kutokatishwa tamaa na mashabiki wachache wasio na subira, ingawa ni kweli ana mapungufu yake ambayo anapaswa kukaa na kuyarekebisha.
Ni vizuri pia benchi la ufundi chini ya Kocha Pierre Lechantre likakaa na huyu mchezaji kuweza kumshauri, pengine yawezekana tatizo la kisaikolojia linamuathiri.
Imekuwa ni kawaida kwa baadhi ya wachezaji kushindwa kumudu viwango vyao wanavyoondoka navyo kutoka timu moja kwenda nyingine haswa wanapokutana na mazingira tofauti kwenye timu.
Mavugo aliwasili Tanzania kutokea Vital'O ya Burundi akiwa mfungaji bora wa ligi, lakini makali yake yameenda tofauti kidogo akiwa na kikosi cha Simba.
Hatupaswi kumkatisha tamaa bali anapaswa kupewa moyo apate nguvu ya kupambana na kurejesha kiwango chake.
Shida moja inakuwa pia kwa desturi ya mashabiki wa Tanzania ambao hawana uelewa wa kuwa makosa katika mpira ni jambo la kawaida.
Ifikie hatua sasa waelewe hilo, kwa kawaida binadamu hawezi akaamka kila siku akiwa na furaha, kuna siku lazima anaweza akawa na fikra nyingine tofauti.
Ni mapema sana kusema Mavugo amesharejea katika ubora wake, lakini tumtazame zaidi katika michezo ijayo kama atatuonesha kile alichokuja nacho wakati anaanza kuichezea Simba.
Wachezaji kwa ujumla wanapaswa pia kujitambua ni kipi wanatakiwa kufanya wawapo uwanjani na si kusikiliza kelele na mshabiki ambazo mara nyingi zinakuwa hazina maana zaidi ya kujaza lawama.
0 COMMENTS:
Post a Comment