Unaweza kusema mapemaa wapinzani wa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Township Rollers FC ya Botswana, wameanza kuuza tiketi za mechi yao ya marudiano itakayochezwa Machi 17, mwaka huu.
Mchezo huo umepangwa kuchezwa Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa uliopo Gaborone, Botswana kuanzia saa 10:45 kwa saa za Tanzania. Awali Waswana walishinda mabao 2-1 dhidi ya Yanga.
Katika mtandao wa klabu hiyo, wametangaza viingilio vya mechi hiyo kuwa vimegawanywa kwa makundi manne ambapo kuna Jukwaa la Grand, Jukwaa la Panda, Jukwaa la Kaskazini na Jukwaa la Kusini.
Viingilio hivyo vimewekwa kwa fedha ya Botswana ijulikanayo kama Pula ambapo katika Jukwaa la Grand ambalo ndilo jukwaa kuu, kiingilio ni Pula 60 (Sh 13,800), Panda ni Pula 40 (Sh 9,240), Kaskazini ni Pula 30 (Sh 6,930) na Kusini ni Pula 10 (Sh 2,310).
Mchezo huo unatarajiwa kuchezeshwa na mwamuzi wa kati Redouane Jiyed, akisaidiwa na Youssef Mabrouk na Hicham Ait Abbou wote kutoka Morocco.
0 COMMENTS:
Post a Comment