Kiungo mshambuliaji Mtanzania anayecheza soka la kulipwa Klabu ya Difaa El Jadida ya nchini Morocco, Simon Msuva ametamka kuwa anataka kuifikia rekodi ya mshambuliaji wa Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta.
Kauli hiyo aliitoa baada ya wikiendi iliyopita kuifanikishia timu yake kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuiondoa Vita SC ya DRC.
Difaa ilifanikiwa kuindoa Vita kwa ushindi wa mabao 3-2 baada ya nyumbani kushinda bao 1-0 lililofungwa na Msuva kabla ya kwenda ugenini kupata sare ya mabao 2-2.
Msuva alisema rekodi anayoitaka ni kubeba Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika, mwaka huu kama ilivyokuwa kwa Samatta na Thomas Ulimwengu walivyolichukua wakiwa wanaichezea TP Mazembe ya nchini Congo DRC.
“Ndoto zangu ninaona zinaanza kutimia taratibu ni baada ya kufanikiwa kuiwezesha timu yangu ya Difaa kufuzu hatua ya makundi, niseme kuwa ni jambo jema kwangu.
“Nimeingia kwenye historia moja nzuri kwangu, hivyo sitakiwi kubweteka zaidi ni kuendelea kuipambania timu yangu iweze kuchukua ubingwa huu.
“Asante Mungu kwa nafasi nyingine sasa ni hatua nzuri hii niliyofikia, kikubwa ninahitaji dua zenu kwani ni wakatim mzuri wa mimi kukua na kusogea kisoka,” alisema Msuva.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment