April 2, 2018







Na Saleh Ally
TOKEA ameondoka Yanga misimu minne iliyopita, katika Ligi Kuu Bara, mshambuliaji Jerry Tegete amefanikiwa kufunga mabao tisa tu.


 Aliondoka Yanga na kujiunga na Mwadui FC, lengo likiwa ni kutafuta nafasi ya kucheza zaidi na kurudisha kiwango chake.


Mwadui FC, ndiyo ilikuwa chaguo lake na ilionekana ana nafasi ya kufanya vema kwa kuwa alikuwa akicheza. Msimu uliisha akiwa amefunga mabao matano, si haba kwa kuwa ilikuwa ni timu mpya na alitokea timu kubwa kwenda ndogo.


Matarajio katika hali ya kawaida, kwamba msimu uliokuwa unafuatia, Tegete angeinuka na kufanya makubwa zaidi. Maana alishazoea mazingira ya Mwadui FC na mji wa Mwadui na sasa kazi ingeanza.


Msimu uliofuatia akiwa na Mwadui FC, akafunga mabao matatu ikiwa pungufu ya mawili ya yale ya msimu mmoja uliopita.



Nafikiri Mwadui FC waliona hakuwa na msaada waliohitaji au yeye aliona si sehemu aliyoihitaji kupata nafasi ya kucheza na kurejesha kiwango chake. Akajiunga na Majimaji FC.
Hawa wanajulikana kama Wanalizombe, huku nako hadi sasa msimu unakwenda ukingoni, Tegete ana bao moja tu. Kufikisha matano inaweza kuwa miujiza, labda matatu kama ya msimu uliopita.


Kama ingekuwa ni kutumia takwimu, maana yake Tegete amekuwa akiporomoka msimu hadi msimu kutoka mshambuliaji hatari hadi wa kawaida.



Kwa hali inavyokwenda sasa, anatokea kuwa mshambuliaji wa kawaida hadi wa kawaida sana na huenda ndiyo ukawa wakati wa kusema “Byebye Jerson John Tegete”, kwa kuwa nafasi ya kuinuka na kuwa hatari wakati umri unakimbia kwa kasi ya kimondo inakuwa ni ngumu zaidi.


Tegete alishindwa kupata nafasi akiwa mwishoni Yanga, kocha wake Hans van der Pluijm alilazimika kuongea washambulizi, akiwaunganisha Donald Ngoma na Amissi Tambwe kwa kuwa aliona kulikuwa na utani.


Pluijm aliwahi kusisitiza kwamba hapendi watu wasio makini kama Tegete. Lakini hili pia liliwahi kuzungumzwa na kocha mkuu wa Yanga wakati huo, Ernie Brandts.


Kwa kuwa Tegete alikuwa kipenzi cha Wanayanga, hakujali sana. Wengine tuliamini ni utoto, huenda atakua zaidi na mambo kwenda vizuri zaidi. Lakini haikuwa hivyo na tukaamini kuondoka kwake Yanga ni nafasi nyingine ya kujitengeneza, hii nayo imeshindikana.



Kama unakumbuka miaka mitano iliyopita, Tegete alikuwa mshambuliaji tegemeo wa Yanga. Klabu hiyo haikukubali kumkosa hata mchezo mmoja. Kama unakumbuka alikuwa akifanya majaribio nchini Sweden, akapita.


Wakati akisubiri kuanza kazi, uongozi wa Yanga ukafanya juu chini kumrejesha aitumikie Yanga katika mechi dhidi ya Simba hata kama Simba walishachukua ubingwa. Kweli Tegete akarejea na kuitumikia Yanga. Alifunga mabao mawili na Yanga ikalala kwa mabao 4-3.


Baada ya hapo, hakurudi tena Sweden na maisha yakaendelea. Tegemeo ni kwamba, kila miaka inavyopanda angezidi kuwa tegemeo.


Hata baada ya Kocha Marcio Maximo kurejea Yanga, ikaonekana ulikuwa wakati mwafaka Tegete kurudi katika kiwango chake. Hadi Maximo anaondoka, mambo yalikuwa ni mabaya zaidi ya awali na Maximo akarejea Brazil.


Makocha Waholanzi wote, walisema Tegete si makini. Sasa amekwenda Mwadui FC, hawakusema jambo lakini alifeli, yuko Majimaji, sina sababu ya kukuambia.


Huenda Tegete ameshindwa kurudi kwa kuwa baba yake ameshindwa kuwa mkweli na kumueleza “anapokimbilia”. Huenda rafiki wa karibu tumezidi kuwa tunaomba matumaini ya upande usio sahihi kwa kuwa tunahofia kumuudhi.


Nani asiyejua uwezo wa Tegete anapopata nafasi ya kuutumbukiza mpira wavuni? Nani ambaye hakuwa na matumaini ya Tegete kucheza Ulaya? Mechi moja tu aliyopewa Sweden ya majaribio, alitupia mabao mawili.


Kipa kufungwa na Tegete, halikuwa jambo la kutafuta kwa tochi. Sasa anakwenda huyo, anakwenda kupumzika na kipaji chake na inaonekana hakitakuwa kimempa faida ya kutosha kwa ajili ya maisha ya baadaye na mwisho, “atabaki stori”.


Bado kuna nafasi ndogo ya kurejea ambayo Tegete anaweza kuitumia kama atapenda. Lakini haiwezi kuwa rahisi na akumbuke hata akirejea vipi, muda wa kutamba utakuwa mchache kwa umri nao ndiyo unakwenda hivyo.


Maneno haya yanaweza kuwa yanamuumiza Tegete, huenda nisingependa kumuambia kwa kuwa nia yangu sio aumie, lakini ukweli ndiyo maisha bora, kachezea nafasi ya maisha yake kwa kuwa ni mvivu, si mwenye hofu ya kufeli na huenda hana hofu maisha magumu baadaye.


Vizuri Tegete atumike kama bango bora la mafunzo kwa mnaoona hasa wale mnaochipukia, maana alipopitia yeye, wengine msikubali.


Pia mjifunze, kipaji pekee hakiwezi kuwa kila kitu. Nia ni jambo muhimu sana, lakini kujituma pamoja na nidhamu ni chachu sahihi ya kufikia mafanikio.


TAKWIMU ZA MABAO:
2015/16
Tegete          Mwadui        5           

2016/17
Tegete          Mwadui        3           

2017/18
Tegete                  Majimaji       1   



2 COMMENTS:

  1. Duh inasikitisha sana...na haya unayozungumzia kwa Tegete bado yanaendelea kwa wachezaji wengine hasa wa vilabu hivi viwili Simba na Yanga.Angalia issue ya Mohammed Mo baada ya kupewa mkataba mpya wala haonekani kuwa serious na bado wapenzi wa Simba, rafiki na ndugu hawampi nasaha za kuzingatia miiko ya kazi yake ya mpira.Kuwa na kipaji cha kucheza soka haimanishi ndio hutakiwi kufanya mazoezi na kumsikiliza kocha na mbinu zake anazotaka kukufundisha.Wachezaji wetu wa kitanzania mjitambue kuwa soka inahitaji nidhamu na kuwa serious.

    ReplyDelete
  2. Hivi mchawi wa mastaa wa mpira wa Kitanzania ni nani?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic