Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF Ndugu Wallace Karia ameipongeza klabu ya Young Africans kwa kufanikiwa kuingia kwenye hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Africa.
Young Africans imefanikiwa kuingia kwenye hatua hiyo kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1 baada ya kushinda mchezo wao wa kwanza kwa mabao 2-0 kabla ya kufungwa bao 1-0 na timu ya Welaitta Dicha ya Ethiopia.
Rais wa TFF Ndugu Karia kwa niaba ya TFF ameipongeza klabu ya Young Africans kwa hatua hiyo kubwa iliyofikia ambayo inaakisi mpira wa Tanzania kiujumla.
“Mafanikio ya klabu ya Young Africans ni mafanikio ya Tanzania kiujumla na TFF ambao ni wasimamizi wa Mpira nchini tunajivunia mafanikio hayo ya Young Africans ambao tumekuwa tunashirikiana nao bega kwa bega kuhakikisha wanapeperusha vyema bendera ya Tanzania”amesema Karia.
Amesema anaamini watafanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye hatua hiyo ya makundi.
0 COMMENTS:
Post a Comment