Kati ya burudani inasubiriwa kwa hamu na hofu kuu ni ile ya Jumapili wakati Simba watakapoivaa Yanga ambao ni watani wao wa jadi.
Yanga na Simba, zinakutana Jumapili katika mechi ya Ligi Kuu Bara na zote ziliweka kambi mkoani Morogoro.
Tayari timu hizo zimemaliza maandalizi, yamebaki kiduchu tu ili kumaliza kazi.
Yanga na Simba kila upande unatakiwa kushinda na kutakuwa na burudani nyingi lakini ile ya mshambuliaji Emmanuel Okwi dhidi ya Kelvin Yondani inaonekana itakuwa ni moja ya zile zitakazovutia zaidi.
Yondani ni beki kisiki wa Yanga na Okwi ni mshambulizi wa pembeni hatari wa Simba, wote wawili wana kasi.
Kutokana na Yondani kuwa na kasi, mara nyingi hulazimika kumaliza kazi ya kumdhibiti Okwi ambaye akiachiwa, ni matatizo.
Katika mechi ya mzunguko wa kwanza, mara kadhaa Yondani alilazimika kufanya kazi ya ziada kumzuia Okwi.
Wachezaji wote wawili ni wazoefu wakubwa wa mechi hizo za watani na waliwahi kucheza pamoja wakiwa Simba na baadaye pamoja tena wakiwa Yanga.
Lakini katika mechi hii, kwa mara nyingine wanakutana wakiwa wapinzani, kila mmoja akiwa amepania kuusaidia upande wake ufanye vizuri.
0 COMMENTS:
Post a Comment