April 15, 2018






Na Saleh Ally
HUU ni mwaka wa 11 sasa tangu Mfaransa, Franck Henry Ribery alipojiunga na kikosi cha Bayern Munich na huenda ameendelea kuwashangaza wengi kutokana na mafanikio ambayo ameendelea kuyapata. 

Ribery sasa ana umri wa miaka 35 na amekuwa akiendelea kufanya vizuri akiwa tegemeo la Bayern Munich ya Ujerumani kwa miaka yote 11.

Kwa sasa, tayari Bayern wameshabeba ubingwa wa Bundesliga ambayo kwa hapa nchini huonyeshwa kupitia ving’amuzi vya StarsTimes.

Lakini Ribery ni kati ya wachezaji walioiongoza Bayern kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiwa pamoja na AS Roma, Liverpool na mabingwa watetezi, Real Madrid.

Ribery alianza kutamba mwaka wa kwanza tu tokea ametua Bayern akitokea Marseille ya kwao Ufaransa na kukawa na mambo mengi kutokana na yanayotokea.

Kwani msimu wa kwanza tu alifanikiwa kufunga mabao 11 akiwa na asisti 8, hivyo kumfanya baadaye kutangazwa mwanasoka bora wa Ujerumani.

Ukiona sasa anaendelea kutamba Bayern unaweza kudhani maisha yake ni rahisi lakini amekuzwa na fedha za kazi za vibarua alizokuwa akifanya baba yake mzazi na wakati fulani aliingia kufanya kazi hizo hadi alipoona anastahili kuendeleza ndoto yake katika soka.

Kupitia timu maarufu kama Metz, Galatasaray na sasa Bayern, kumbuka Ribery amekuwa mwanasoka bora wa Ulaya mwaka 2013.

Huyo ni Ribery, lakini ana rafiki yake, Arjen Robben. Huyu ana miaka 34, pungufu ya mmoja wa Ribery. Yeye alijiunga Bayern miaka miwili baadaye, yaani 2009 akitokea Real Madrid.

Hadi sasa tayari ana miaka tisa naye anaendelea kung’ara na kuwa shujaa. Kipindi ambacho hatasikika, basi ni majeruhi lakini baada ya hapo lazima atakuwa tegemeo kama iliyo kwa Ribery.

Robben anatokea Uholanzi na maisha yake wakati akiwa mtoto hayakuwa mazuri sana na baba yake aliishi akifanya kazi za kawaida tu na maisha yalikuwa ni ya kuunga kiana.

Baada ya kuanza kufanikiwa katika mpira, Robben aliamua baba yake mzazi awe wakala wake na hadi sasa amekuwa akifanya kazi hiyo na kuendelea kujiingizia kipato chake na anaendesha maisha yake.

Wawili hawa wanafanana sana kutokea maisha ya awali lakini mwendo waliofikia sasa na siri yao kubwa pamoja na kwamba wana vipaji ni kujituma bila ya kuchoka na ile kuwa na ndoto ya kutaka kupata mafanikio.

Pamoja na kwamba wanaonekana ni kama “wamezeeka” lakini wao ndiyo vyuma vya Bayern. Siku wakiwa fiti wote na katika kiwango sahihi basi ujue kazi inayofanyika katika “mabawa” ya Bayern kutoka kushoto na kulia, lazima itamuumiza mpinzani.

Ukibahatika kufika katika Jiji la Munich nchini Ujerumani, wawili hao hujulikana kama pacha na kila mmoja ana sifa yake. Robben ni mpole, ila mjeuri. Ribery ni mkimya ila mjeuri ile mbaya.

Kinachovutia zaidi ni heshima kubwa wanayopata kutoka kwa Wajerumani ambao wanaamini katika utendaji bora wa kazi kwa kujituma bila ya kuchoka na kutobweteka baada ya kupata mafanikio.

Robben amebeba ubingwa wa Bundesliga kwa misimu saba, ameshinda Kombe la Ujerumani mara nne, akachukua Super Cup ya Ujerumani mara moja, Ligi ya Mabingwa mara moja na Uefa Super Cup mara moja.

Pia aliifikisha Uholanzi katika nafasi ya pili ya Kombe la Dunia mwaka 2010, Hispania wakiwa mabingwa.

Kwa upande wa Ribbery, amebeba ubingwa wa Bundesliga kwa misimu nane, ameshinda Kombe la Ujerumani mara tano, akachukua Super Cup ya Ujerumani mara moja, Ligi ya Mabingwa mara moja na Uefa Super Cup mara moja kama ilivyo kwa Kombe la Dunia la klabu.

Riberry naye aliiwezesha Ufaransa kushika nafasi ya pili Kombe la Dunia baada ya kufungwa fainali na Italia, mechi ambayo Zinedine Zidane alilambwa kadi nyekundu kwa kumtwanga kichwa Marco Materazzi.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic