Kampuni ya Azam Media kupitia Azam TV, Jumapili ya wiki hii itawakutanisha wadau na wapenzi wa soka hapa nchini na kushuhudia mechi ya wapinzani wa Ligi Kuu Hispania "La Liga" kati ya wenyeji Barcelona dhidi ya Real Madrid.
Azam TV ambayo imeiandaa siku hiyo maalum kwa kuiita El Clasico In Tanzania kutokana na mchezo huo kujulikana kwa jina la El Clasico, mashabiki wa soka wataushuhudia mchezo huo bure katika Ukumbi wa King Solomon jijini Dar es Salaam ambapo kutakuwa na skrini kubwa itakayoonyesha mechi hiyo na kutangazwa kwa Kiswahili.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando alisema siku hiyo mbali na kuonyesha mechi hiyo, pia kutakuwa na michezo mbalimbali ambayo watakaohudhuria watashiriki.
"Kutakuwa na burudani nyingi kama muziki, kucheza PlayStation, nyama choma na burudani zingine.
"Wasanii Mwana FA ambaye ni shabiki wa Real Madrid na JB shabiki wa Barcelona nao watakuwepo siku hiyo," alisema Mhando.
Wakati huohuo, Azam Media imetangaza kuwapeleka nchini Hispania Mwana FA na JB kushuhudia mchezo wa La Liga kati ya Barcelona dhidi ya Levante utakaochezwa wikiendi ya wiki ijayo.
Akizungumzia safari hiyo, JB alisema: "Kiukweli nimesafiri sana lakini kwa hili walilonifanyia Azam ni kitu cha kipekee, nimefurahi sana na naamini nikiwa huko furaha yangu itakuwa maradufu ikizingatiwa kwamba nitaishuhudia timu yangu ikicheza."
0 COMMENTS:
Post a Comment