NA SALEH ALLY
WANASOKA nao ni wafanyakazi kama mfanyakazi yoyote yule anayeamka nyumbani kwake na kuwa ofisini asubuhi na baada ya hapo, anarejea nyumbani.
Ofisini kwa wanasoka kunakuwa na tofauti kadhaa, kama vile kufanya mazoezi na inaweza kuwa asubuhi na jioni au mara moja kwa siku na kadhalika na baada ya hapo kuna suala la mechi na mafanikio pia.
Kila timu inaposhinda, hayo ndiyo yanakuwa mafanikio yenyewe kwa kuwa yanaongeza umaarufu wa timu, klabu na kuifanya kuwa na thamani zaidi.
Wanaofanya kazi kubwa katika klabu ni viongozi, benchi la ufundi na wachezaji ili kufanya mambo yaende sahihi.
Mafanikio ya klabu yanajengwa na wachezaji na mafanikio ya wachezaji yanajengwa na klabu. Klabu iliyofanikiwa itakuwa na wachezaji waliofanikiwa.
Angalia mafanikio ya Real Madrid, ndani yake unaona kuna wachezaji wengi wenye mikataba nje ya klabu na inawaingizia mamilioni ya fedha kama ilivyo kwa FC Barcelona, Manchester United, Bayern Munich na nyinginezo.
Wachezaji wao kama Cristiano Ronaldo, Gareth Bale, Lionel Messi, Luis Suarez, Paul Pogba na wengineo wanapata mikataba mikubwa kutoka katika makampuni mengine ya nje na si klabu.
Makampuni yanayowapa mikataba yanataka jambo moja tu, kujitangaza. Yanakuwa tayari na fedha na kutafuta ambao wanaweza kujitangaza.
Yanapoangalia klabu yenye mafanikio au timu inayofanya vizuri, yanapata wachezaji wa aina hiyo wanaoweza kuwatangaza.
Hili kwa hapa nyumbani lilitakiwa kuwa limeanza muda mrefu sana wachezaji waache kutegemea mishahara pekee na kubaki na majina yao makubwa wakiwa wamelala nayo nyumbani tu.
Wanatakiwa kupata mishahara, wafanye kazi kwa juhudi na maarifa kuzisaidia klabu zao kupata mafanikio kupitia timu wanazozichezea na baada ya hapo lifuatie suala la mvuto linaloweza kuwapa fedha.
Hapa nyumbani Tanzania, kumekuwa na hisia ambazo wachezaji wanapaswa kuzibadilisha, kwamba wachezaji wa Tanzania hawaaminiki au wasumbufu linapofikia suala la kupewa mikataba.
Wasumbufu kwa maana hawajitambui, hawana nidhamu sahihi katika suala la kuheshimu mikataba na wakati mwingine wanaweza kuona sahihi wao kulipwa fedha halafu katika utekelezaji wa mikataba wakawa si wazuri.
Hili suala lina ukweli ndani yake tena kwa kiasi kikubwa kwa kuwa wachezaji wengi wa Kitanzania wanakuwa hawana uongozi binafsi unaowaongoza kufanya mambo kitaalamu au kwa kufuata weledi.
Bahati mbaya wengi wao wanaamini kazi ya mwanasoka ni kucheza mpira pekee, jambo ambalo ni kosa kubwa na wanapaswa kuachana nalo mara moja.
Mwanasoka kupitia jina lake, anaweza kuwa mfanyabiashara mkubwa sana. Ndiyo maana leo tunaona Cristiano Ronaldo anamiliki hoteli katika nchi mbalimbali kwa kuwa analitumia vizuri jina lake kwa ushauri wake na wataalamu wake.
Ronaldo na wenzake ambao wanafanya biashara wakati wakiendelea kucheza wanajua kwamba soka ni mchezo wa muda mfupi, baada ya hapo wataendelea na maisha wakiwa nje ya uwanja.
Maisha nje ya uwanja, hayakupi nafasi kama ile uliyoipata wakati unacheza, maana yake wakati unacheza lazima kujiandaa na maisha ya baadaye kama wanavyofanya akina Lionel Messi, Ronaldo na wenzao.
Kwa hapa Tanzania, mchezaji hawezi kupata fedha kama wanazopata akina Pogba, lakini anaweza kupata kwa kiwango chake kwa kuwa balozi au kutangaza na makampuni mbalimbali.
Makampuni kabla ya kutangaza, hufanya uchunguzi wa kutosha kuhusiana na wanayetaka kumtumia awatangazie, maana yake ni kweli hasa lazima waridhike na nidhamu yake baada ya kukubali ubora wake.
Jonas Mkude wa Simba na Ibrahim Ajibu wa Yanga wamepewa shavu la kuwa mabalozi wa King’amuzi cha StarTimes wakati wa World Cup, lazima watakuwa wanajua utamu wake. Sasa hii haitoshi, uwepo ubunifu na juhudi zaidi, ili mjiongezee kipato zaidi kwa kuwa makampuni yanatafuta watangazaji sahihi.
0 COMMENTS:
Post a Comment