May 9, 2018




Na Saleh Ally
NAJUA sihitaji kukumbusha kwamba Yanga imesafiri kwenda Algeria kuwavaa USM Alger ikiwa hoi kwa maana ya wachezaji karibu wote walioonekana wanahitajika na wenye nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza wamebaki.


Wachezaji hao wamebaki wakitoa sababu mbalimbali tena rundo, lakini ukweli ni sababu moja tu, suala la malipo yao ya mishahara na mikataba mipya, full stop.


Yanga imeshindwa kulipa mishahara ya miezi inaelezwa ni mitatu, wachezaji wamechoshwa kukopwa na wameamua kuiacha Yanga katika kipindi kigumu kabisa. Mimi sikuzunguka, niliwaita ni wasaliti, hasa wale wanaodai mishahara kwa kuwa hata waliokwenda, wanadai mishahara pia.

Nawaita hivyo kwa kuwa wameshindwa kuonyesha uzalendo angalau kumaliza kazi moja na kuendelea kudai au ikiwezekana kujitokeza hadharani na kueleza uvumilivu umewashinda na wanahitaji kusaidiwa katika linalowakabiri badala ya kuiacha Yanga “ikafe yenyewe Algeria.”


Wakati nikiwa nawazungumzia wachezaji, ninaamini wako wengi watapishana na mimi kimtazamo, kwangu hili si baya kwa kuwa kila mmoja yuko huru kufikiri na kuamini anachokiamini.

Wachezaji, yes ni wasaliti lakini viongozi wa Yanga wanaoshindwa kulipa mishahara vipi? Kwa nini wapo tu na wana rundo la mitaji ambayo wanaendelea kuichezea huku ikiwa mikononi mwao?


Sasa mambo ni magumu kifedha, tatizo limewafika shingoni na wameshindwa kulitatua wakati katika mikono yao kuna mtaji mkubwa ambao wamekuwa wakiendelea kuuchezea miaka nenda rudi.

Nimeandika sana kuhusiana na hili, ninarudia kwa kuwa natambua sisi wanadamu tumeumbwa wasahaulifu. Kama Yanga itakuwa inategemea fedha kidogo za milangoni, fedha za kutoka kwa wadhamini na bado imeshindwa kulipa mishahara, vipi viongozi hawajiongezi ili tuone kuna kinachoingia na kuongeza kipato?


Mtaji wa mfanyabiashara ni wanunuzi wa bidhaa zake, Yanga ina watu zaidi ya milioni 15 wanaoiunga mkono (hapa sizungumzii wale makomandoo wanaofaidika na klabu, wakiwa hawaisaidii lolote).


Jengo la makao makuu ya Yanga, liko katika makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani. Hili ni mtaji, liko katika eneo zuri ambalo watu wanalipa mamilioni ya fedha kuishi au kufanya biashara, Yanga haiingizi hata senti na bado inasumbuka kulipa wachezaji wake mishahara?

Kwanini wasiingie ubingwa na kampuni ambayo inaweza kuwekeza kwa namna yoyote jengo hilo likawa sehemu ya kipato cha klabu hiyo?

Inaweza kuwa makao makuu kama ilivyo, lakini juu kukawa na ofisi za kampuni mbalimbali, kipato kinachoingia Yanga ikawa inapata angalau asilimia 20, baada ya miaka kadhaa, basi muwekezaji anawaachia Yanga jengo lao kama ni ghorofa sita, saba, nane, tisa au kumi na wanaendelea na maisha yao.

Wakati hili likifanyika, wao wanaweza kuendelea kusumbuka kuujenga uwanja wao ambao unaonekana wanaendelea kujaza kifusi ingawa haijajulikana mwisho wake ni nini hasa!


Kwa sasa jengo ni kichaka cha watu kujificha na kufanya biashara zao chafu. Jana, wako walitaka kumshambulia mpigapicha wetu eti hawataki jengo lipigwe picha, eti kwa kuwa wanaandikwa vibaya, nafikiri wanaumia kuelezwa ukweli kwamba wao pia ni mizigo, maana hawachangii lolote linapotokea tatizo na ukweli wanafaidika na klabu hiyo wakiwa wanaendelea kuidumaza.

Sasa wanajaa watu wanaofanya biashara za hovyo ndani ya jengo hilo upande wa nyuma, watu ambao hawana faida na lenyewe halina faida kwa Wanayanga hasa wenye mapenzi ya dhati, acha hao wachache wanaolitumia.


Nimepata bahati ya kufika katika klabu mbalimbali za Ulaya kama Real Madrid, FC Barcelona, Manchester United, Arsenal, Atletico Madrid na nyingine na sikuwahi kuwa mchoyo badala yake kupitia gazeti hili niliwaeleza nilichokiona.

Kati ya niliyowahi kuwaeleza kwamba klabu kama ya FC Barcelona au Real Madrid na nyingine nilizozitaja, wanauza nguo za watoto, nguo za ndani za watoto, vishika ufunguo, vikombe na wanaingiza mamilioni ya fedha.


Jezi nafikiri ndiyo jambo tunalolijua, kweli wameingia ubia na makampuni kama Nike au Adidas ndiyo wanaotengeneza na kuuza na klabu zinaingiza fedha zake kupitia asilimia.
Wakati Yanga inalalama haina fedha za mishahara, jezi zao zinaendelea kuuzwa mitaani na watu wanakula fedha na hakuna hatua wanayochukuliwa. Wakati mwingine hadi ninajiuliza, viongozi au uongozi wa klabu nao unafaidika?


Haya matatizo yanaweza kuwa yanaletwa na mfumo, mwisho wachezaji wamekuwa tatizo huenda wamechoka lakini hawakutumia busara. Lakini viongozi mnaweza mkawa tatizo kubwa zaidi kwa kuwa mnaendeshwa na mawazo ya makomandoo wenu na hofu huenda siku moja watawasema vibaya.


Silaha ya makomandoo feki wa klabu hizi kongwe ni kejeli (kwa kuwa hawana hoja), kutishia kupiga au kuumiza (kwa kuwa wanajua wao ni tatizo), kusingizia Yanga inaumizwa (badala ya kusema maslahi yao yanaumizwa). Viongozi nao wamekuwa waoga kwa kuwa wangependa kuonekana wazuri na kuepuka kejeli na vitisho ili kuzuia hofu ya kuaibishwa.

Viongozi amkeni sasa, badilikeni sasa, fumbueni macho na mioyo muache kuwahofia watu wasio na dira, wanafiki wanaotaka kuonekana wanaipenda klabu kwa maslahi yao na mfanye yaliyo sahihi kwa maisha ya sasa na baadaye ya klabu yenu. Nitarudi tena.





1 COMMENTS:

  1. Hakuna cha usaliti kwenye swala LA kutokulipwa mishahara zaidi ya miezi tatu...Je wewe Saleh waweza Fanya kazi miezi tatu bila malipo

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic