Kampuni ya MultiChoice Africa Limited imethibitisha uteuzi wa Wakurugenzi wawili ambapo Mtanzania Maharage Chande, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania anakuwa Mkurugenzi mpya wa kanda ya Afrika Mashariki na Magharibi wa kampuni hiyo.
Uteuzi huo uliotangazwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa MultiChoice Africa Brand de Villiers, unabainisha kuwa Maharage anachukua nafasi ya Stephen Isaboke, aliyekuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki ambaye sasa anakuwa Mkuu wa masuala ya Mamlaka (Group Executive Head of Regulatory). Uteuzi huu unaanza rasmi Juni 1, 2018.
Afisa Mtendaji Mkuu wa MultiChoice Africa Brand de Villiers amesema kuwa uteuzi wa Maharage umezingatia upeo na uwezo wake mkubwa aliouonyesha katika kipindi alipoiongoza MultiChoice Tanzania tangu alipojiunga na kampuni hiyo mwezi Juni mwak 2016.
“Ninaamini kwa uwezo na uzoefu aliouonyesha Maharage katika kipindi kifupi cha kuiongoza kampuni ya MultiChoice Tanzania ni dhahiri kuwa atakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha safu yetu ya uongozi na kusaidia katika kuongeza mbinu na ujuzi aliokuwa nao katika kuimarisha kampuni yetu na kuhakikisha tunaendelea kutimiza matakwa ya wateja wetu kote Afrika.”
Kwa upande wake Maharage amesema amepokea uteuzi huo kwa mikono miwili na kwamba bila shaka hayo ni matokeo ya jitihada kubwa zilizofanywa na yeye pamoja na wafanyakazi wote wa MultiChoice Tanzania.
“Kwa hakika kaitika kipindi kifupi tumekuwa na mafanikio makubwa sana – kuanzia katika kuongeza idadi ya wateja wetu, kuimarisha huduma zetu na pia kuongeza kuchangia katika maendeleo ya jamii na uchumi wa nchi yetu kwa ujumla. Haya ni mafanikio tunayojivunia sisi kama kampuni na tumeyafikia kwa jitihada, nidhamu na uchapakazi.
Hivyo naamini mafanikio haya ya Tanzania tunaweza pia kuyatumia kama chachu ya kuleta mafanikio kwa Afika nzima”
Baadhi ya wafanyakazi wa MultiChoice Tanzania wameonyesha Furaha yao kubwa kwa uteuzi wa Mkurugenzi huyo na kusema kuwa katika kipindi chake ameleta mageuzi makubwa katika kampuni hiyo ambayo yameleta mafanikio makubwa kwa kamppuni, wafanyakazi na jamii kwa ujumla.
Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo Esther Mtei amesema wamefurahi kuona mkurugenzi wao amekabidhiwa uongozi wa kanda na kwamba hii ni heshima kubwa kwa Tanzania ndani ya kampuni ya MultiChoice Africa.
“Uteuzi wa Maharage kuwa mkurugenzi wa kanda ni uthibitisho tosha kuwa Watanzania tunaweza kushika nyadhifa kubwa kama hizi na pia tunaaminika. Tunaamini uteuzi huu utakuwa ni chachu kwa watanzania kuongeza bidii katika shughuli zao kwani fursa kubwa zipo kila mahali.”
Kabla ya kujiunga na MultiChoice Tanzania mwaka 2016, Maharage alifanya kazi katika ngazi za juu za uongozi katika makampuni mbalimbali ikiwemo ya simu za mkononi ya Vodacom, Benki ya NBC na pia Ofisi ya Rais Maharage ana shahada ya teknolojia ya mawasiliano (Bachelor degree in Electronics and Communication) ya chuo kikuu cha Dar es Salaam na pia shahada ya juu ya uongozi wa biashara (Masters in Business Leadership) ya chuo kikuu cha Afrika Kusini (UNISA).
Na jina tamu vile vile lazima alitendee haki jina lake kuipaisha tz.
ReplyDelete