KICHUYA AIPA OFA YANGA
Mchezaji kipenzi cha mashabiki wa Simba, Shiza Kichuya tayari amesaini mkataba wa miaka miwili Simba lakini amesema kama Yanga watakwenda na dau kubwa analolihitaji atavunja mkataba na kwenda kusaini Jangwani.
Kichuya ambaye anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji amesaini dili jipya na Simba hivi karibuni kwa dau la Sh milioni 80 na atakuwa analipwa mshahara wa Sh milioni 5 kila mwezi.
Staa huyo ambaye msimu uliopita alifunga mabao saba, alitoa asisti 21 kwa wenzake na kuchangia ubingwa wa timu hiyo ambayo ilikuwa ikiupigania kwa muda wa miaka mitano.
Kwa mujibu wa gazeti la Championi, Kichuya ambaye ni mkazi wa Morogoro, alisema kwa upande wake haoni shida yoyote kwenda kuichezea Yanga kwa kuwa hana uadui nao wala timu nyingine itakayompa kile atakachohitaji kuanzia mshahara na dau la usajili.
“Nipo tayari kwenda na kwa upande wangu siyo Yanga tu ni timu ya aina yoyote ambayo itakuwa tayari kutoa mpunga ambao mimi ninataka na utakuwa freshi, nakwenda kwa sababu mpira ndiyo kazi yangu na hii iwe nje au ndani maana Simba haiwezi kuwa mwisho wangu katika soka kikubwa ni maelewano.
“Hakuna mashabiki wa Yanga wanaonichukia kwa kuwa tu niliwafunga, hapana kwa sababu kinachotokea uwanjani kinaishia uwanjani palepale kwa sababu hata kama itatokea wamekasirika ndiyo imeshafungwa haiwezi kufutika ila jambo zuri baada ya pale maisha ya kawaida huendelea bila tatizo lolote hivyo hainipi shida,” alisema Kichuya ambaye wakala wake ni msomi mkubwa nchini.
0 COMMENTS:
Post a Comment