SINGIDA UNITED KUFUATA NYAYO ZA SIMBA LEO, MOROCCO KUANZA KIBARUA CHA KWANZA
Na George Mganga
Michuano ya SportPesa Super Cuper Cup inaendelea kurindima tena mchana wa leo kwa Singida United kukipiga dhidi ya AFC Leopards ya huko Kenya kwenye Uwanja wa Afraha mjini Nakuru.
Singida inaingia kucheza mchezo huo ikiwa imetoka kupoteza mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania dhidi ya Mtibwa Sugar kwa mabao 3-2.
Mechi hiyo inayosuburiwa kwa hamu na wadau wengi wa soka nchini kwa ajili ya kuipa nafasi Singida kusonga mbele ikiiwakilisha Tanzania, itaanza majira ya saa 9:00 alasiri.
Tayari timu moja pekee ambayo ni Simba imefanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali jana kwa ushindi wa matuta (3-2) baada ya dakika 90 kwenda suluhu dhidi ya Kariobangi Sharks ya Kenya.
Kwa mujibu Kocha wake, Hemed Morocco, amesema kuwa wamjipanga kupigania matokeo kuelekea mchezo wa leo ili waweze kuiwakilisha vema Tanzania.
Morocco atakuwa anaanza kazi rasmi dhidi ya AFC Leopards baada ya kuingia mkataba wa mwaka mmoja na matajiri hao wa Singida baada ya kuondokewa na Mholanzi wake, Hans van der Plujim aliyetimkia Azam FC.
Endapo Singida United itapata matokeo chanya dhidi ya Leopards itakuwa timu ya pili kuingia hatua ya nusu fainali na kuungana na Simba iliyotinga huko jana.
Singida na Simba ndizo timu pekee zilizosalia katika mashindano baada ya JKU na Yanga kuyaaga juzi Jumapili.
0 COMMENTS:
Post a Comment