August 20, 2018






NA SALEH ALLY
HIVI karibuni tulitaarifiwa kwamba Simba imeingia mkataba mpya na kampuni ya vinywaji ya Mo Energy na sasa sehemu ya upande mmoja wa juu wa jezi yake watakuwa wanavaa nembo ya kinywaji hicho.

Kinywaji hicho tayari kilianza kuwa maarufu lakini sasa kitakuwa na nafasi ya kuwa maarufu zaidi kwa kuwa kinaidhamini Simba ambayo ni moja ya klabu kubwa kabisa za Tanzania.

Udhamini ambao wameupata Simba kwa mwaka mmoja unaweza kusema si mkubwa sana kama utachukua na ukubwa wa klabu yenyewe au jina lake.

Angalia, kwa mwaka mmoja Sh milioni 250, kwa Simba si kitu, lakini unaweza kujiuliza, waipate au waikose kabisa. Kama Mo Energy walikuwa tayari kutoa na wengine hawakuwa tayari, wangefanyaje?

Lazima utasema bora waipate na nilielezwa kwamba viongozi wa Simba walikuwa na uharaka wa kuhakikisha wanapata fedha ya kumalizia kukomboa nyasi zao na kuanza mara moja ujenzi wa uwanja.

Wanataka kutimiza ndoto zilizosimama kuhusiana na kuwa na uwanja wao angalau wa mazoezi ili kukamilisha jina rasmi kuwa hii ni klabu yenye timu kubwa ya soka.

Wakati viongozi wakifanya juhudi hizo, kumeanza kuwa na minong’ono pamoja na malalamiko mengi kutoka katika makundi mbalimbali, kuna watu wanalalamika wakiamini ile nembo ya Mo Energy pale kifuani kwa Simba ni kiasi kidogo.

Wanaona Sh milioni 250 ni chache sana na ilitakiwa zaidi. Hivyo wameanza kulalamika wakisema kuwa si sahihi na viongozi wa Simba walikurupuka.

Nimeiona mijadala hii mara kadhaa, kuanzia mitandaoni na hata baadhi ya wasomaji wa gazeti hili ambao wamekuwa wakituma maoni yao. Binafsi naona wana haki ya kufanya hivyo na kutoa maoni yao kuhusiana na kile wanachoona ni sahihi.

Lakini natamani kuwashauri kwamba hata wao wanapaswa kujiuliza mambo mengi kabla ya kulaumu pekee. Kwamba kama Simba haikuwahi kupata udhamini wa Sh milioni 250 na kupima utamu wake, itaweza vipi kupata zaidi?

Simba haikutakiwa kuziacha Sh milioni 250, baada ya mwaka itakuwa na nafasi ya kuwakaribisha wadhamini wengine au kumshawishi mdhamini waliyenaye kuongeza kitita cha fedha.

Hata yeye atakuwa ameiona faida ya kutangaza na Simba na atakuwa tayari kuongeza kiasi zaidi cha fedha kwa ajili ya kuendelea kujitangaza na Simba.

Wengine pia wataitamani hiyo nafasi. Maana yake kwa sasa, nafasi wanayojitangaza Mo Energy inazidi kupanda thamani kadiri siku zinavyosonga na Simba inazidi kujiwekea mazingira ya kupandisha thamani yake. Na hii itakuwa ni faida kubwa kwa klabu hiyo hapo baadaye hata kama Mo Energy hawatataka kuendelea. Ninaamini, haitawezekana mdhamini mpya akijitokeza au huyu wa sasa akiongeza muda, Simba itapata Sh milioni 250 tu.

Lakini hapo hapo, kuna kila sababu ya kwa kuwa sasa hawa watu ambao wamekuwa wakipenda kukosoa kila kinachofanywa na viongozi wa hizi klabu kwa nia njema hasa kama sasa tunavyoona, wanapambana kujenga uwanja.

Uwanja huo wa Simba, utakuwa ni wa Wanasimba na si viongozi wa klabu pekee ambao tunaamini hawatadumu milele au kuendelea kubaki hapo milele. Mwisho uwanja utakuwa faida ya wanachama na mashabiki wa klabu hiyo.

Pia tuache tabia ya kulaumu tu, inawezekana viongozi hao wana nia nzuri na wameteleza, basi vizuri kusaidiana nao kuhakikisha kinachofanyika ni sahihi na si kwa kulalama pekee. Basi vizuri kuwasaidia kutoa njia mbadala.

Angalia waliochangia kumuondoa Yusuf Manji wakati Yanga ina raha zake na kifuani ina Quality Group. Wakawa wanahoji na kulalamika kila kukicha. Sasa Yanga ina shida na hakuna anayepambana kusaidia Yanga iingize fedha na hakuna anayetoa njia mbadala! Mnasubiri siku ikipata mdhamini mwingine, muanze kushambulia na kulalama. Badilikeni.

5 COMMENTS:

  1. Hizi klabu zina watu wanajifanya wanajua. Lakini ndio hulka ya mtanzania mwingi wa maneno yasiokuwa na utafiti.

    ReplyDelete
  2. Umechanganya mambo mawili tofauti, pesa zisiwe chanzo cha kudhalilisha mali

    ReplyDelete
  3. Umesema vizuri sana binafsi nimeona makala zako zote ulizoziandika hii ina ushauri wa maana. Isipokuwa mwishoni umemalizia .... Badilikeni. Hapo umekosea. Muungwana ni binadamu kama hao wengine hata wewe unayo mapungufu yako. ungetumia maneno" TUBADILIKE". Huo ndio ungekuwa wito wako kwa wote. Lakini kiujumla ujumbe wako ni mzuri.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic