August 28, 2018


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya Wizara yake kuwaondoa mara moja wananchi wote waliovamia katika maeneo ya majeshi nchini.

Lugola alisema hayo baada ya kulikagua Gereza jipya la Wilaya ya Ruangwa linalojengwa ambalo lina ekari 100 lakini ekari 20 limevamiwa kwa kujengwa kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti, ufuta na korosho katika eneo hilo la Jeshi la Magereza.

Akizungumza baada ya kulikagua Gereza hilo, mjini Ruangwa leo, Lugola alisema kuanzia sasa viongozi wa vyombo vyake wahakikishe hawaruhusu mwananchi yeyote kuingia katika maeneo ya jeshi na atakua mkali kulifuatilia suala hilo.

Lugola ambaye pia aliikataa kuipokea taarifa ya ujenzi wa gereza hilo ambayo ilikua inasomwa na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Lindi, Rajabu Nyange, alisema taarifa hiyo ina upungufu mkubwa na hawezi kuipokea licha ya kua imeeleza kuhusu ardhi ya jeshi hilo kuvamiwa.

“Mimi huwa nashangaa sana inakuaje wananchi wanavamia ardhi ya jeshi tena bila woga, halafu jeshi linakaa kimya linabaki kunung’unika, hii haijakaa sawa kabisa na kamwe sikubaliani nalo,” alisema Lugola.

Lugola aliongeza kua, “uvamizi wa ardhi mara nyingi unakua kwa jeshi la polisi na magereza, mbona Jeshi la Wananchi silisikii hili, kwanini nyie mnakaa kimya wananchi wakivamia ardhi yenu, sasa nawataka muhakikishe ardhi ya jeshi popote nchini iliyoporwa inarudishwa ndani ya jeshi, na wote waliovmia waondooeni haraka iwezekanavyo.”

Kwa upande wake Mkuu wa Magereza mkoani humo, alisema licha ya ujenzi wa gereza hilo kuendelea kujengwa lakini ekari 20 ilichukuliwa kimakosa na kujengwa kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti na ufuta pamoja na kubangua korosho vinavyomilikiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.

“Jitihada za ufuatiliaji urejeshaji wa eneo hilo zimefanyika ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri hii ameonyesha nia ya kurejeshwa eneo hlo,” alisema Bakari.

Aliongeza kuwa, ujenzi wa gereza hilo ambalo linatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu, unatarajiwa kumaliza msongamano wa wafungwa na mahabusu kwenye Gereza la Wilaya ya Nachingwea kutokana na mahabusu wengi kutoka Ruangwa.

Waziri Lugola alifanya ziara ya dharura katika mikoa hiyo, pia aliambatana na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali, Jacob Kingu kwa kufanya ziara ya kutembelea Jengo lililokwama ujenzi la uhamiaji Mkoa wa Mtwara na Lindi na pia kulitembelea Gereza la mahabusu na wafungwa linalojengwa mjini Ruangwa, mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kubaini mapungufu ya ujenzi wa majengo hayo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic