Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe anatafutwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili arudishwe nchini na kujibu tuhuma zinazomkabili.
Kupitia ndugu zake, Championi limempata na kusikia akilalamika kuhusiana na Takukuru inavyomdhalilisha, hatua aliyoiita kuwa inawezekana ina msukumo unaotaka kumnyima haki, akihoji kinachoendelea.
Wiki iliyopita, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Brigedia Jenerali John Mbungo aliweka wazi kuwa wanamtafuta aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Simba, Zacharia Hans Poppe na mwenzake Frank Lauwo.
Hans Poppe na Lauwo wanatafutwa ili waunganishwe kwenye kesi ya kutoa taarifa za uongo akishirikiana na viongozi wengine wa Klabu ya Simba, Rais Evans Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’.
Viongozi hao wanakabiliwa na kesi ambayo inasikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar, ambapo Ijumaa ilishindwa kuendelea kwa watuhumiwa hao wawili kutokana na mwendesha mashitaka wa Takukuru kutokuwepo mahakamani hapo.
“Poppe anatafutwa kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kuhusiana na malipo ya kodi, kifungu 106(1) A& C(i) cha Income Tax Act sura ya 332 R.F 2008, kwamba kati ya Machi 10, 2016 na Septemba 30, 2016, mshitakiwa akishirikiana na wenzake Aveva na Kaburu, walitoa maelekezo ya uongo kwenye Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba Simba wamenunua
nyasi za bandia (Artificial Turf ) kutoka Kampuni ya Ninah Guangzhou Trading Company Limited kwa thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.
Maelezo ambayo yalikuwa ni ya uongo kwani nyasi hizo zilinunuliwa kwa UDS 109,499,” alisema Mbungo ambaye alitangaza donge nono kwa atakayefanikisha kukamatwa kwake.
Lakini Gazeti la Championi, liliamua kufanya juhudi ya kuwatafuta ndugu zake ambao walitoa ushirikiano na kueleza namna Hans Takukuru.
Hans Poppe kasikitishwa sana. Ngoja, kuna sauti yake hapa baada ya kuzungumza naye, unaweza kumsikia na namna ilivyo,” hiyo, Hans Pope akizungumza, Championi linakuu. “Nashangaa sana kuwa taasisi kubwa kama Takukuru wanaweza kufanya jambo kama hili.
wenyewe kuwa niliondoka kwa kutumia paspoti halali na mpaka halali kwa hiyo sikutoroka kwa sababu wiki moja tu kabla nilikuwa kwao na kuwapa ushirikiano kama ilivyokuwa tokea mwaka uliopita mwezi wa saba nadhani na waliendelea kuniita mara kwa mara na niliwapa ushirikiano vizuri tu,” inasikika sauti ya Hans Poppe.
“Mpaka naondoka sikuwa nimeitwa kuripoti kwao wala kutakiwa kujibu mashtaka. Mombasa nilienda kutafuta kazi ya kusafirisha mafuta kutoka yanakochimbwa kule Kaskazini kuyapeleka Lamu na wakati niko kule nikaanguka na kuumiza goti la kushoto ambalo niliwekewa vyuma Novemba, mwaka jana.
Bahati mbaya chuma kimoja kikawa kimehama na kunisababishia maumivu,” anazidi kuelezea Hans Poppe.
“Ikabidi nimtafute daktari wangu aliyenifanyia upasuaji wa mwanzo na bahati nzuri alikuwa Dubai nikaenda kumuona huko na akanishauri niende Marekani na nilienda huko na kuanza matibabu ambayo baada ya ‘physiotherapy’ (tiba ya mwili) nilipata nafuu lakini maumivu yakarudi tena hivyo nikarudi tena.
Kipindi hicho nikapata habari kuwa natafutwa na ati nimetoroka na kujificha. Nikamtafuta wakili wangu Mr Shio ambaye aliwaandikia barua Takukuru akiwafahamisha nilivyotoka na niko wapi na nafanya nini.
Iweje leo waseme hawajui niko wapi? “Kwa sasa inabidi nijiulize mara mbilimbili kuwa kulikoni nisakwe kwa nguvu za namna hii kwa kosa ambalo hata mtu ukitiwa hatiani lina faini ya chini 50,000 na juu 500,000? Utafikiri nimeua kijiji!
Hiyo ‘press conference’ (mkutano na waandishi) waliyoitisha Takukuru ni gharama kuliko hiyo faini. Na nikiangalia hayo mashtaka nahisi wanataka kunibambika kesi bure tu. Hiyo invoice (Ankara) iko chini ya jina la Simba na Simba ndio waliokuwa na mzigo wao na wao ndio walioipeleka huko TRA, sasa mimi naingiaje hapo kama sio kutafutwa kudhalilishwa tu?” anahoji Hans Poppe.
“Kosa ni la forodha kuna rushwa gani hapo? Juu ya yote walioipeleka hiyo invoice ambao ni SSC (Simba) wameadhibiwa kwa mujibu wa sheria za forodha na wamelipa hiyo faini na kukabidhiwa nyasi zao. Kwamba mimi sikupigwa hiyo faini, ni wazi kuwa hata hao TRA wanatambua kuwa siyo mimi niliyeitoa hiyo invoice na ndio maana adhabu yao ikaelekezwa kwa walioitoa.
Tuseme DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) hajui haya? Tuseme Takukuru hawayajui haya mpaka wafikie kunidhalilisha hivi?” anahoji Hans Poppe akionyesha kushangazwa.
Anaendelea: “Mimi sijajificha na sina sababu ya kujificha kwa kesi ya aina hii. Ila nimeingia wasiwasi kwa mwenendo mzima na maelezo ya Takukuru ambayo wenyewe wanajua dhahiri kuwa hawakuwa wanatoa taarifa za ukweli.
Najiuliza kwa nini taasisi kama hiyo ifanye hivyo kinyume na weledi kama hakuna msukumo wowote? Kama kuna msukumo huo nitendewe haki ya namna gani? Inabidi nipate uthibitisho pasi na shaka yoyote kuwa hakuna kitu nyuma ya pazia.
Mimi niko matibabu na nia yangu kurejea kujibu hayo mashtaka haraka baada ya kumaliza matibabu. Nitatafuta ushauri wa wakili wangu. Kwa hofu iliyonipata kwa jinsi mambo yalivyo siwezi kusema niko wapi na nimehama leo baada ya kuwaelezea wenyeji wangu juu ya hili,” sauti ya Hans Poppe inafikia tamati.
Baada ya hapo, jana hiyo, gazeti hili lilimtafuta Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba ambaye alisema yafuatayo:
“Ahha kwamba yupo nje kwa matibabu, sisi hatuna taarifa kama hizo bwana, sisi siyo wajinga, umenielewa!
“Sasa kama wana hizo habari si wangetuletea ofisini? We washauri kwamba waje ofisini. Si njia nzuri ile kulalamika kwamba tunaamua kumdhalilisha.
“Sasa wewe waambie kesho (leo) Jumatatu waje ofisini kama wanajua, watueleze. Barua imeletwa kwetu?
Hapana. Unajua mtu unaweza kusema umefikisha kumbe taarifa hazijafika kwenye ‘proper channel’ (wahusika sahihi), umenielewa!
“Unajua kuna watu wengine wanaweza kusema hivyo kumbe haikufika mahala pake, nashukuru kwa taarifa hizo.”
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment