September 3, 2018


Yanga wamesikia kejeli za Simba wanaowatania kwamba jina la Wakimataifa limekufa rasmi kwavile mwakani hawana chao, lakini Kocha Mwinyi Zahera amewajibu kwa kukaa chini na Heritier Makambo na kumwonyesha pakuwabania na kuwaziba midomo.

Kwa mujibu wa gazeti la Spoti Xtra, Kocha Mwinyi Zahera ambaye anamtegemea zaidi straika Makambo, amekaa kikao na wachezaji wote na kuwatengeneza kisaikolojia kwa kuwataka wasahau matokeo ya Rayon ambapo walifungwa bao 1-0 kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na badala yake kuelekeza akili zao kwenye ligi ambako ndiko kazi ilipo kwa sasa.

Zahera amefurahishwa na mabadiliko ya aina ya soka ambalo wachezaji wake wameendelea kulionyesha na sasa wataingia uwanjani kwenye michezo ijayo ya ligi bila ya kuidharau na watakaza sana.

“Baada ya mechi iliyopita, nilitenga muda maalumu kwa ajili ya kuzungumza na wachezaji wangu na kikubwa kuwatengeneza kisaikolojia ili warejee katika hali ya kawaida, kwani nilihofia baada ya matokeo hayo wangekata tamaa na tungefanya vibaya katika michezo ijayo ya ligi.

“Hivyo, sikutaka kuona hilo linatokea hivyo niliwapa maneno ya kuwapa moyo na kuwarejesha mchezoni kwani katika mchezo huo hatukuwa na kitu cha kupoteza kutokana na michezo iliyopita kufanya vibaya, hivyo tunarejea kweli.

“Kurejea kwetu hakutaidharau timu yoyote tutakayokutana nayo zaidi tutaingia uwanjani kwa lengo la kuchukua pointi tatu kwenye kila mchezo tutakaoucheza bila ya kujali hii timu ndogo au kubwa,” alisema Zahera ambaye timu yake inakabiliwa na ushindani mkubwa wa Simba iliyosajili kikosi cha gharama kubwa.

Kucheza na Tambwe

Zahera amefunguka kuwa atahakikisha anawapanga pamoja Makambo na Amissi Tambwe katika mechi zinazofuata kuhakikisha wanafunga mabao ya kutosha.

“Wakati tunaanza ilikuwa ngumu kuwatumia pamoja katika safu nzima ya ushambuliaji lakini kutokana na kucheza kwa muda katika programu za mazoezi ambazo tumekuwa tukifanya kwenye mazoezi ya maandalizi zimeweza kuonyesha mabadiliko makubwa kutokana na uwezo walioonyesha.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic