September 26, 2018






NA SALEH ALLY, POLOKWANE
MJI wa Polokwane uko umbali wa kilomita 320 kutoka katika jiji kubwa la biashara la Johannesburg nchini Afrika Kusini.

Huu ni mji ulio katika Jimbo la Limpopo na wakati wa miaka ya 1900 ulikuwa maarufu zaidi kwa mchezo wa kriketi na gofu kutokana na kukaliwa na Wazungu wengi.



Baadaye mambo yalibadilika na baada ya kuongezeka sana kwa idadi ya Waafrika, soka lilianza kutawala, sasa kuna timu takriban 100 za soka lakini Winners Park FC, Black Leopards, Polokwane City na Baroka FC anayochezea Mtanzania, Abdi Banda ndizo timu maarufu zaidi.

Takwimu zinaonyesha Polokwane ina wakazi Waafrika asilimia 74.4, Shombe asilimia 3.7, wenye asili ya Asia 3.1% na Wazungu au weupe ni 18.2. Bado mji huu ni kati ya ile yenye utulivu zaidi nchini Afrika Kusini na suala la usalama si kama miji ya Johannesburg, Durban na Cape Town.

Usalama wa Polokwane angalau mtu anaweza kutembea mitaani usiku bila ya hofu na Zabibu Kiba, dada wa msanii maarufu nchini, Ali Kiba amekuwa hana hofu.

Zabibu anaishi Polokwane, maisha yake yatakuwa hapa kwa kuwa mumewe, Abdi Banda anafanya kazi hapa. Anaichezea Baroka FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini. Timu nyingine mbili za Black Leopards na Polokwane City zinashiriki ligi hiyo na kuufanya mji huu kuwa na timu nyingi zaidi zinazoshiriki ligi kuu ya nchini hapa.

Zabibu ni kama Watanzania wengine na sasa maisha yake yamehamia katika mji huu ambao ni mwendo wa zaidi ya saa tatu na nusu kwa gari kutoka jijini Johannesburg.

Gazeti la Championi, limefanya mahojiano maalum na Zabibu akiwa nyumbani kwake mjini hapa na kueleza mengi.

Zabibu amesema kuna wakati amekuwa akipata shida kutokana na kubaki peke yake lakini limekuwa jambo lisilompa hofu kutokana na aina ya maisha yake hata kabla ya kufunga ndoa na Banda ambaye kwa sasa ni nahodha msaidizi wa Baroka FC.

SALEHJEMBE: Inapofikia Banda amekwenda nje ya mji kwa ajili ya mechi, mfano wanacheza Johannesburg, kwako inakuwaje?
Zabibu: Upweke ni lazima, lakini wakati huu nimeshazoea maana maisha yangu niliyokuwa naishi Dar es Salaam, hayana tofauti.

SALEHJEMBE: Maisha yako ya Dar es Salaam, yalikuwaje?
Zabibu: Muda mwingi nilikuwa nikishinda nyumbani, sikuwa mtu wa kwenda sehemu nyingi. Hivyo sioni shida sana kukaa ndani.
SALEHJEMBE: Vipi maisha ya hapa, kipi kinakushinda?
Zabibu: Naweza kusema hakuna. Kuna baadhi ya vitu vilikuwa vigeni lakini nimezoea na hata Banda akisafiri naelewa na kwa kuwa yuko kazini, namuombea zaidi.



SALEHJEMBE: Umekuwa ukienda uwanjani kumshuhudia akicheza?
Zabibu: Mara chache sana, kwa kuwa mimi pia si mpenzi sana wa mpira ingawa nimekuwa nikijifunza nikiwa na kaka zangu.


SALEHJEMBE: Kaka zako yaani Ali Kiba na Abdu Kiba? Je, ulikuwa unajifunza nini?
Zabibu: Unajua nipo na kaka zangu, sasa wao wanapenda mpira na nimekuwa nikikaa nao kuangalia mpira pamoja na tunafurahia na kwa kuwa imekuwa ni kawaida kufanya hivyo mwisho nikawa najifunza mambo kadhaa ya mpira. Nao wakifungwa wananuna pia.

SALEHJEMBE: Hapa Afrika Kusini unashabikia timu gani?
Zabibu: Baroka FC, hiyo haina mjadala ingawa naweza kuvutiwa na timu nyingine pia.
SALEHJEMBE: Uliposhuhudia mechi Banda akicheza nini kilikuvutia?
Zabibu: Anacheza kwa nidhamu, hili ndiyo limenivutia.

SALEHJEMBE: Kingine?
Zabibu: Hakuna, nidhamu ni zaidi.



SALEHJEMBE: Vipi kuhusiana na mashabiki wa hapa?
Zabibu: Wananivutia, wanajituma sana kuunga mkono timu yao. Naona wako tofauti na wale wa nyumbani. Maana hawachoki mwanzo mwisho na wanashangilia sana.

SALEHJEMBE: Ulisema Ali na Abdi walichangia wewe kupenda mpira na hata wakati mwingine wananuna timu zao zikifungwa hasa unapowatania. Je, kwa Tanzania unashangilia timu gani na nje ni ipi?
Zabibu: Tanzania nashangilia Simba, pia Azam FC. Kwa Ulaya mimi ni Manchester United.

SALEHJEMBE: Banda pia anashangilia timu hiyo?
Zabibu: Hapana yeye ni Liverpool. Tena ikifungwa anaweza akagoma hata kunisemesha maana anakuwa na hasira sana.

SALEHJEMBE: Wewe vipi ikifungwa Manchester United?
Zabibu: Sifurahii lakini siumii sana kama yeye ikifungwa Liverpool.

SALEHJEMBE:: Ali Kiba naye ni Liverpool, vipi ikifungwa?
Zabibu: Naye ni kama Abdi (Banda). Ikifungwa anakuwa mkali sana, wakati mwingine hataki utani. Angalau Abdu, ikifungwa Arsenal mnaweza kumzomea na kutaniana.

SALEHJEMBE: Unaweza kutaja angalau wachezaji wawili wa Manchester United?
Zabibu: Kwanza Lukaku, Pogba, Sanchez, De Gea, Matic na Mourinho ni kocha.

SALEHJEMBE: Huna timu nyingine zaidi ya Manchester kwa Ulaya?
Zabibu: Real Madrid ingawa hivi karibuni nitahamia Juventus.

SALEHJEMBE: Kwa nini?
Zabibu: (kicheko), unajua Ronaldo kahamia huko. Alipo tupo (kicheko).
SALEHJEMBE: Labda unakumbuka mlivyokutana na Banda?

Zabibu: (kicheko), dada yake ni rafiki yangu. Hivyo aliniona naye na baada ya hapo akaomba kuzungumza na mimi, tukaanza kama urafiki.

SALEHJEMBE: Banda ni mtu wa aina gani?
Zabibu: Ni mtu ambaye ana misimamo sana, lakini anaweza kusikiliza ushauri na wakati mwingine yuko tayari kubadilika.

SALEHJEMBE: Hakukuwa na shida kwako kuona ni kazi kuolewa na mwanasoka?
Zabibu: Hili lilikuwepo, kulikuwa na ugumu. Hata yeye nilimuambia lakini akawa ananishawishi na kunieleza namna alivyo tofauti na taratibu nikabadili msimamo.

SALEHJEMBE: Majirani wa huku ni vipi, unapata nafasi ya kwenda kupiga stori hivi?
Zabibu: Ni watu wazuri lakini kila mmoja na maisha yake, mambo yake. Ndiyo maana muda mwingi nakuwa mwenyewe ndani hasa Banda anapokuwa safari. Kama nilivyokueleza inanifanya niwe mpweke lakini taratibu nimekwenda naanza kuzoea.

SALEHJEMBE: Mungu akijaalia mnataka kupata watoto wangapi?
Zabibu: Kweli hatujajua, lakini kama itawezekana baada ya kupata inshallah basi tutapanga.

Huyo ni Zabibu, mwanadada anayetokea katika familia ya wanamuziki lakini pia vipaji vya soka na sasa ameolewa katika familia ya soka.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic