Nahodha Msaidizi wa Taifa Stars, kiraka Erasto Nyoni, ameweka wazi kuwa kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli juu ya pesa alizotoa, imewapa ujasiri mkubwa wa kupambana katika mchezo ujao wa kuwania kufuzu Afcon dhidi ya Lesotho.
Nyoni ameyasema hayo kufuatia Rais Magufuli kuwakabidhi Sh mil 50 kwa ajili ya kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mbio za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) huku akionya kuwa wakifungwa basi watazitapika kwa njia nyingine.
Stars imebakiwa na mechi mbili ambazo Rais Magufuli amewataka wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wanashinda.
Stars ipo kwenye nafasi ya pili katika Kundi L ikiwa na pointi tano, nyuma ya vinara wa kundi hilo, Uganda, wenye pointi kumi wakati Cape Verde wakishika nafasi ya tatu na pointi zao nne huku Lesotho wakiburuza mkia na pointi zao mbili.
Taifa Stars imebakiza mechi dhidi ya Lesotho ugenini mwezi ujao, kabla ya kumalizia nyumbani dhidi ya vinara wa kundi, Uganda.
Nyoni alisema kwa upande wao, kauli hiyo ni nzito lakini wameichukua kama changamoto ambayo inawapa ujasiri wa kuweza kuhakikisha mechi inayofuata dhidi ya Lesotho wanapata matokeo ya ushindi.
“Ujumbe mzito, ujumbe una changamoto ndani yake lakini na sisi tumeupokea kwa kuwa chachu ya kazi yetu na wachezaji wote tumeuelewa, kikubwa kwetu ni kuweza kupambana kwa kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi inayofuata dhidi Lesotho ili tuzidi kuwa kwenye nafasi nzuri ya kufuzu Afcon.
“Unajua yeye ni baba, kwa hiyo siyo rahisi baba kwa mtoto wake kuacha kumuonya wakati mwingine akimfokea kwa ustaarabu ila wakati mwingine anakupa neno la kukupa ujasiri na kuweza kufanya vizuri.
“Alichotuambia hakutuambia kwa ubaya ila ameongea kwa kutoa msisitizo wa kuweza kupambana ili kufikia mafanikio,” alisema Nyoni.
0 COMMENTS:
Post a Comment