Kwa sasa hatua tuliyofikia angalau kidogo tunaweza tukapongeza jinsi ambavyo ushindani ulivyo kwenye Ligi Kuu Bara. Bado ligi ni mbichi na hakuna ambaye amelalamika kuhusu matendo ya kununua matokeo wala kuonewa.
Ni jambo ambalo linaleta neema na kuweza kuanza kukubalika kwa baadhi ya watu ambao wanafuatilia soka kwa kuwa hilo la ushindani kwa sasa lipo wazi ligi ni ngumu kabisa kila timu inakomaa kuhakikisha inafikia malengo yake.
Habari ambayo imekuwa kubwa ni kutokana na mchezo wa Simba na Yanga ambao ulichezwa wikeendi iliyopita katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Nimeufuatilia kwa ukaribu mchezo ule na nimegundua mengi ya ajabu na kushangaza kwenye soka letu.
Jambo kubwa ambalo bado lisipotazamwa kwa ukaribu linaweza kuleta hatari wakati mwingine ni utaratibu ambao unakuwa kwenye mageti ya kuingilia, yaani hauvutii hata kidogo hasa kwa mechi kama ya Simba na Yanga.
Ubabe wa askari wetu bado upo palepale hata uwe na kitambulisho au tiketi wala hawakuelewi, sijajua wanataka kuendesha mechi hizi kwa mfumo upi jambo ambalo linaweza kuwa sawa kwa wote ambao wanafika Uwanja wa Taifa kutazama mechi hiyo.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapaswa kulitazama hili kwa jicho la kipekee kwa sababu mashabiki huwa wanakosa raha kabisa wakati wa kuzishuhudia timu zao wazipendazo, sijajua kwa nini mchezo wa mpira ambao una amani unatawaliwa na shari.
Nimebahatika kuwaona namna askari walivyokuwa wakiwapiga baadhi ya mashabiki wakidai walishindwa kufuata utaratibu hasa kwenye geti kubwa la kuingilia, hili nalo halipo sawa, kuna namna nzuri ya kuweza kuwaelekeza mashabiki na wakaelewa.
Baada ya mchezo huo, tumeona timu yetu ya taifa, Taifa Stars imeingia kambini ikijiandaa na mchezo ujao wa kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) dhidi ya Cape Verde.
Rai yangu ni kwamba wachezaji mnapaswa kutimiza wajibu wenu ipasavyo kwa kuonyesha juhudi isiyo ya kawaida hasa katika kuipeperusha Bendera ya Taifa huko kimataifa.
Muda pekee wa kuweza kuhakikisha kwamba kila kitu katika soka kinawezekana hasa kwa kufanya kweli katika mashindano hayo ni sasa kwa kuwa tuna wachezaji wengi ambao wana uzoefu na mashindano ya kimataifa.
Jambo kubwa la muhimu ambalo mnapaswa kufanya ni kuhakikisha kwamba mnaaonyesha nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya uwanja hali ambayo itasaidia kupata matokeo mazuri katika michezo ambayo mtashiriki.
Kuna tabia ambayo wachezaji wengi huwa nayo hasa baada ya kuitwa timu ya taifa, wanadhani kwamba wao wanaweza kufanya kila kitu jambo ambalo linawafanya wanavimba kabla hata ya kucheza mpira.
Kuvimba ama kuwa na dharau ni kosa kubwa kwa mchezaji kwani kwa kufanya hivyo kunadidimiza ule uwezo ambao unao na hata ukipewa nafasi utashindwa kuitumia vema.
Yatupasa tubadilike na tubadilishe makosa ambayo tuliyafanya wakati tunacheza na timu ya Uganda, hivyo kupata ushindi iwe ndio dhamira yetu kuu ya kwanza katika mchezo wetu huo ujao.
Mara nyingi nimekuwa nikiwaambia wachezaji ambao napata bahati ya kuonanana nao ni kwamba kuitwa timu ya taifa ni nafasi ambayo wameipata adimu sana na ni kubwa kuliko vile ambavyo wanafikiria, hivyo wanapaswa wafanye makubwa zaidi.
Kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza thamani ya mchezaji maradufu hali itakayoanza kufungua milango ya mafanikio taratibu bila papara yoyote ile katika ushindani ambao tupo kwa sasa.
Niseme tu kwamba kwa hatua ambayo kwa sasa tumefikia sio mbaya kwani kuna kitu ambacho kinaonekana kwa wachezaji na wanaweza kufanya maajabu hasa katika mashindano ya kimataifa ambayo tunashiriki.
Inawezekana meseji ikawa sent au ujumbe umefika. Ila vyama vingi vya mpira au taasisi zinazoshughulikia Timu za Taifa Africa zimeingia migogoro na wachezaji wanaokwenda kutumikia timu zao za taifa. Suala la uzalendo sawa lakini lazima tuwe wawazi juu ya maslahi ya wachezaji hao wa timu ya Taifa wakati wanapokwenda kutumikia taifa lao kama Tanzania basi lazima tuwe wawazi juu ya suala hili kungali mapema ili kuepusha uwezekano wa kuja kuingia katika migogoro isio ya lazima kati ya wachezaji na mamlaka husika. Tunaimani FIFA au CAF lazima watakuwa na fungu fulani kuhusiana na mashindano husika basi chonde kwenye fungu hilo wachezaji ndio wawe wanufaika wa kwanza na lazima kuwe na uwazi. Mpira sasa unahitaji motisha kwa wachezaji kwani ushindani ni mkubwa hata wa huo wa motisha kwa wachezaji wa timu nyengine kwa hivyo ni vizuri kusoma alama za nyakati .
ReplyDelete