November 14, 2018


Baada ya wimbo wa msanii wa WCB, Raymond Shaban Mwakyusa maarufu  Rayvanny  aliyomshirikisha Diamond Platinumz uitwao Mwanza kufungiwa na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na kumtaka auondoe mitandaoni, Diamond ameibuka na kuvunja ukimya huku akilishauri Baraza hilo kuwa kuufungia wimbo huo ni kuikosesha mapato ya zaidi ya Tsh. Milioni 48 Serikali ya Tanzania kwani ungewaingizia kipato kupitia YouTube na shows kisha wangelipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diamond ameandika;

KWA WAZEE WANGU WA BARAZA LA SANAA TANZANIA (BASATA)

Kwanza kabisa niwapongeze kwa kazi nzito na nzuri Mnayoifanya, lakini pia niwape pole kwa changamoto mbalimbali mnazokutana nazo, maana najua ugumu mnaopitia katika kusimamia sanaa yetu Nchini.

Ujumbe wenu kuhusu kufungiwa wimbo wa #Mwanza almaarufu kama #NYEGEZI wakuu nimeupata ila tu kwabahati mbaya mtoto wenu niko Canada katika harakati za kutafta rizki ili kuendelea kulijenga taifa na kuendelea kutangaza sanaa zetu, ila laiti ningelikuwa nchini ningekujamara moja kama mnavyonijuaga pindi mniitapo basi hufika haraka bila ukaidi.

Tukiwa kama Wasani ambao tumesajiliwa, tuna kila haki ya kuheshimu na kutii baraza letu la sanaa BASATA pindi linapotoa tamko, kwa sababu wao ndio wazazi na walezi wetu kwenye hii sanaa, na kwa kutambua kuwa Sanaa ni kazi ya Ubunifu, na kwenye kubuni wakati mwingine kuna kuwa na usawa na wakati mwingine kutokuwa sawa.

Ndiyo maana mliteuliwa nyinyi wazee wetu maalum kwa jili ya kuhakikisha wasanii wanapotoka nje ya Mstari mnawarudisha ili tuwe na sanaa ilio bora, tuzidi kufanikiwa, na kukua vyema na hata wasanii, mashabiki pamoja na taifa kwa ujumla lijivunie na linufaike na sanaa.

Ila Kwenye UFUNGIWAJI huu nami nilikuwa nina OMBI ama PENDEKEZO kwa balaza letu pendwa la sanaa Tanzania (BASATA).

Licha ya kuwa ni kweli #NYEGEZI ni eneo na Kituo cha Mabasi kilichopo MWANZA, lakini pia ni vyema kama balaza letu pendwa la sanaa kutambua pia kuwa sio kila nyimbo ni kwa ajili ya watoto wadogo. Hivyo kusema isipigwe kwenye TV na Radio tumekubali, lakini iwe kwenye Ule muda ambao serikali uliuweka wa kuwa watoto wako macho, ila pale wanapolala, basi uruhusiwe ili walengwa wautazame.

PILI:- Kusema tuifute Mitandaoni pia, naomba pia Baraza letu pendwa litutazame pia na hapo. Kwa sababu mtoto mdogo tunaemlenga kumlinda asiharibikiwe kimaadili hapa, sizani kama mzazi wake anaweza kumruhusu akaperuziperuzi bila mipaka mitandaoni maana kama kweli ana uwezo wa kufanya hivyo basi anauwezo wa kwenda kuangalia hata Video za utupu, na vitu vingine ambayo wote tunafahamu ndio hatari na Madhara zaidi kwa watoto, kuliko hichi kinyimbo chetu cha MWANZA  NYEGEZI.

Wazee wetu, vijana wenu ama wasanii wenu sasahivi tumefanikiwa kuingia kwenye masoko mbalimbali hivyo sio kila nyimbo ni kwajili ya soko la nyumbani Tanzania tu, mfano: UGANDA kuna Tamasha Linaitwa NYEGE FESTIVAL.

Na kwa nafasi niliyonayo UGANDA na kwajinsi nyimbo hii ilivyovuma kwa kishindo kila kona ndani ya siku tatu tu Viewers 1.5+ Millions Youtube, basi naamini kabisa Mwakani lazima NYEGE FETIVAL waniite kutumbuiza, na kama mnavyofahamu bei zangu huwaga si chini dola elf Sabini za Kimarekani ($70,000) kwa show sawa na milioni (160,300,000 za Kitanzania)….. ambazo kwa show moja tu ningeweza kuchangia pato la kodi si chini ya milioni (48,090,000 ya Kitanzania), hivyo naomba mlitazame na hapo Baraza letu Pendwa.

NNE:- Pia ikija Upande wa Kuitumbwiza stejini naomba pia mlitazame zaidi…Maana show zetu zote ni za Usiku wa manane ambapo watoto wamelala majumbani Tunaowaimbia ni Watu wazima…
na hata #WasafiFestival2018 pia ifikapo saa 12 jioni ni wenye Umri wa zaidi ya miaka 18 tu….hivyo tutaowaimbia ni watu wazima tu.

TANO:- Wazee wangu wa Balaza la sanaa BASATA nilikuwa naomba Muipe sikio tena Nyimbo pale kwenye kipande cha Amber Rutty.. kwasababu Ujumbe wangu pale ni kupingana na kile kitendo, na ndiomaana nikasema “kananivuta ghetto nikapige Bunduki, ila naogopa Centro Michezo ya Amber Rutty” Sasa hapo ubaya wake uko sehem gani…maana naamini kupitia mstari huo utakuwa ni kama Kumbusho kwa kijana ama mtuyoyote kuwa “usidiriki kufanya, Utapelekwa jela.” sasa hapo wapi ubaya wake wazee wetu.

SITA:- wazee wangu wa Basata ni siku tatu tu Tangu kutoka kwa wimbo huu, lakini kika Mwana Africa na hata asiekuwa Mwana Africa Ashapajua Nyegezi Mwanza, na naamini kulikuwa na wengi pengine hawapajui lakini kupitia wimbo Huu sasa wamepajua, na naamini wengi wanatamani hata wafike, Wapigepicha, wakapashangae kuwa kumbe #NYEGEZI kwenyewe ndio hapa, na hio ndio miongoni mwa faida ya kazi ya sanaa wazee wetu.

Mie yangu yalikuwa ni hayo tu, naamini Kwa Uelewa wenu na Upendo wenu mlionao kwa sanaa na wasanii wenu, mtatusaidia kwa hayo maombi yetu vijana wenu. Shukran.

Ni mimi kijana wenu
Nasibu Abdul Juma
(Diamond Platnumz)

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic