Mkurugenzi Mtendaji wa Sport Pesa, Abas Tarimba amesema kuwa wameamua kuialika Mbao FC kutokana na kuonyesha ushindani kwenye ligi Kuu Tanzania Bara ili kuungana na timu za Tanzania na Kenya zinazodhaminiwa na Sport Pesa kwenye michuano ya Sport Pesa Super Cup itakayofanyika nchini Tanzania.
Mbao inakuwa miongoni mwa timu 4 kutoka Tanzania ambazo zitashiriki michuano ya Sport Pesa Super Cup inayotarajiwa kufanyika mwakani Januari 22 ikiwa ni mara ya 3 tangu ianzishwe huku mshindi akikabdiwa dola za kimarekani 30000, pamoja na kucheza na timu ya Everton ya Uingereza.
"Tumeamua kuialika timu ya Mbao kwa kuwa inafanya vizuri kwenye michezo yake ya Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo tunaamini wataonyesha ushindani pia kwenye michuano ya Sport Pesa Super Cup," alisema.
Mwenyekiti wa klabu ya Mbao, Solly Njashi amesema kuwa kwao ni jambo la furaha na ameishukuru kampuni ya mchezo wa kubashiri ya Sport Pesa kwa mualiko huo kwa kuwa ni fursa yao ya kwanza kushiriki michuano ya kimataifa.
"Tunawashukuru Sport Pesa hasa kwa kutupa nafasi ya kuweza kushiriki mashindano haya ya kimataifa, ni nafasi kwetu kuweza kupata changamoto mpya," alisema.
Timu ambazo zitashiriki michuano hiyo zipo 8 ikiwa ni pamoja na Simba, Yanga, Singida United na Mbao FC za Tanzania na Kenya ni Gor Mahia , KariobangiSharks, Bandari FC na AFC Leopards.
0 COMMENTS:
Post a Comment