November 21, 2018






  
Na Saleh Ally
KILA mmoja amekuwa na nafasi ya kusema kuhusiana na kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kupoteza mchezo muhimu huenda kuliko yote katika kipindi cha miaka 28.

Taifa Stars ilishiriki Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) mara ya mwisho mwaka 1980. Mechi ya ugenini dhidi ya “katimu” ka Lesotho ndio ilikuwa inaamua nafasi nyingine ya Stars  kucheza Afcon kama ingeshinda na hakika ilikuwa na nafasi ya kushinda.

Taifa Stars iliyoweka kambi kwa siku 10 nchini Afrika Kusini ikashindwa kushinda dhidi ya Lesotho iliyofanya maandalizi ya siku tatu, tena ikiwa tayari inaonekana imepotea. Timu ambayo unaweza kusema kulikuwa na kila sababu ya kusema inawezekana kufungika.

Tuliona mchezo ulivyokuwa na iliwezekana kabisa kushinda katika mechi hiyo na binafsi nataka kutofautiana na wengi wanaoamini wachezaji hawakujituma au kufanya vizuri kwa kuwa uhalisia unaonyesha Kocha Emmanuel Amunike na benchi lake la ufundi hawakuwa na hesabu sahihi kuhusiana na mchezo huo, nitakuambia kwa nini.

KIKOSI: 
Kikosi kilikuwa katika hatua ya mwisho ya mapambano, si vibaya kusema ilikuwa nafasi nzuri ya mwisho. Kwa sasa Stars bado ina nafasi ya kufuzu kama itashinda dhidi ya Uganda na kuomba Cape Verde iiondoe Lesotho ambayo pia inaweza kuwa ngumu kwa kuwa imepata morali mpya tofauti na ilivyokuwa awali. Maana kama itashinda, mtindo wa head-to-head itaivusha yenyewe dhidi ya Taifa Stars hata kama itakuwa imeshinda.
 

REKODI YA WALINZI:
 Amunike ndiye alikosea kupanga kikosi kwa kuwa utaona ni rekodi mpya kwa kuwa na kikosi chenye washambuliaji wawili na walinzi tisa, jambo ambalo ni rekodi.

Ujumla wa kikosi, wachezaji wawili tu, Saimon Msuva na Iddi Chilunda ndio walikuwa washambulizi. Waliobaki wote ni walinzi ukianza na kipa Aishi Manula halafu mabeki wa kulia, ulianza na Ally Sonso, kushoto, Abdallah Kheri. Katikati Aggrey Morris na Kelvin Yondani halafu Erasto Nyoni, namba sita mwenye aina ya namba nne au tano.

Namba saba alikuwa Himid Mao, huyu ni mlinzi kwa kuwa ni kiungo mkabaji kama ilivyokuwa kwa Mudathiri Yahaya, ni wachezaji wa aina moja. Pembeni kushoto pia kulikuwa na mlinzi wa kushoto, Gadiel Michael.

Timu iliyoanza na walinzi tisa, hakika ilikuwa ni timu inayotaka sare na si ushindi. Lakini unaweza kujiuliza kuwa kweli Tanzania inahitaji kujilinda kwa vifaru na mizinga dhidi ya Lesotho? Ukiangalia sasa wana pointi tano na kati ya hizo, nne wamekusanya kutoka Tanzania! Sisi ndio wanyonge wa Lesotho.
 Mabeki wawili wa pembeni, Sonso na Sebo walikuwa ni watu ambao walikuwa ndio wanacheza kwa mara ya kwanza na hata kama utasema kuwa kocha aliona walifanya vizuri mazoezini, hakika tunapaswa kukubaliana kwamba wachezaji hao ni wazuri lakini walikuwa na hofu na walifanya makosa mengi ambayo Yondani, Manula na Morris walifanya kazi ya ziada kuyafuta.

Kusema wachezaji hawakujituma ni kuhukumu, ingawa ni sahihi kuwaeleza wanapaswa kujituma zaidi. Lakini mchezaji mlinzi unayemlazimisha kufunga, au kutaka Himid na Mudathiri kuichezesha timu katika aina ya unyumbulifu na kutengeneza nafasi, si sahihi.

Tunaweza kuwadharau wachezaji kama Thomas Ulimwengu, lakini hauwezi kusema sahihi kuwa umuweke nje Ulimwengu katika mechi ya kimataifa na nafasi yake acheze Himid ambaye ni mzuri katika ulinzi. Au akae nje, acheze Gadiel ambaye ni mlinzi.
Lazima Himid na Gadiel watacheza katika kiwango chao na walifanya vema, lakini wachezaji wazuri katika ufungaji sote tunajua. Ulimwengu hakufanya vizuri katika mechi moja dhidi ya Cape Verde mjini Praia. Lakini haina maana hawezi kufanya vizuri tena na katika mechi kama hizo anaweza kuwa msaada zaidi na uzoefu wake wa michuano migumu ya Afrika, ukawa msaada.

Msuva bado angeweza kuwa msaada mzuri zaidi angetokea pembeni upande wa Himid, Ulimwengu au John Bocco akawa katikati kwa ajili ya kuwapa wakati mgumu mabeki wa Lesotho, ingekuwa msaada pia.

Taifa Stars ilitakiwa na mtu ambaye ni mfungaji sahihi. Angalia mchezaji kama Chilunda, ana kipaji, alijituma na alikuwa ana nia ya kufanya vema. Mwisho naye uzoefu wa michuano ya kimataifa ulimuangusha kwa kuwa alikuwa na haraka au papara sana, alipoteza nafasi nyingine bila sababu akitaka kupiga langoni kila mpira. Alitaka mzoefu, alitaka maelekezo zaidi au kumuongezea ambao wangeweza kufanya vizuri zaidi na si mwishoni.

Kiungo cha upangaji mashambulizi, kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’, angekuwa msaada zaidi kama angepewa muda wa kutosha kama ambavyo ilikuwa kwa Bocco. Wote waliingizwa muda umeenda na hawakuwa na nafasi ya kutosha kunyumbulika na kufanya jambo.

 

Amunike hakupanga kikosi vema, kikosi sahihi na tusiwe waoga kumueleza ukweli. Hata maamuzi yake ya mwisho pia yalikuwa ya kubabia kwa kuwa alikuwa ni kama mtu aliyepigwa ganzi na kushindwa kuamua mapema.

Ukiangalia kingine ambacho haukugundua, Amunike alipanga mabeki watano wa kati kwa kuwa mabeki wote wa pembeni, Sonso na Kheri ni mabeki wa kati, Morris, Yondani na Nyoni. Hawa si watu wa kulaumiwa kuhusiana na kufungwa ingawa kweli walifanya uzembe katika bao Stars walilofungwa.

Baada ya MAnula kukutana na mpira uliokatika, aliugusa ukaenda juu. Wanasema “back on play”. Pale unakuwa mpira wa wote, ilikuwa ni kipa aruke tena lakini tayari alikuwa mbali, mabeki ndio walipaswa kuhakikisha wanaugusa mpira na si mchezaji wa Lesotho ambaye alifunga kwa ulaini sana.

 Sitaki kuwalaumu mabeki ambao walikuwa wakishambuliwa muda mwingi kutokana na kuwa na timu yenye wachezaji wengi wanaolinda badala ya kushambulia.

Soka la kisasa, unaweza kulinda kwa kushambulia zaidi. Unaposhambulia tayari una mpira, anayetaka kukushambulia analazimika kuuchukua kwanza mpira, ajipange ndio akushambulia.

 Acha tuamini, Taifa Stars ina nafasi ya mwisho, iifunge Uganda, halafu tubaki kwenye hizo dua za kuona Lesoth inafungwa na Cape Verde. Kama itashindikana, hatuna sababu ya kuhoji, eti Taifa Stars ligi iliwahi kufanikiwa? Kitakachofuata itakuwa ni Amunike kwenda nyumbani.

Katika mechi nne, ameshinda moja na sare moja, amepoteza mbili. Kumbuka tayari alikuta pointi zinazomuongezea idadi leo. Lakini jukumu lake ni sasa na nafasi ya kufuzu ilikuwepo, tukishindwa yeye kama kocha atakuwa ndiye aliyeipoteza na atatakiwa kuwajibika, hakuna mjadala.


Kwa wachezaji, wao wana uchungu zaidi ya Amunike kwa kuwa hili ni taifa lao, lazima wapambane, mfano wa mechi waliyopata sare ya 0-0 na Uganda kwao. Hapa nyumbani lazima washinde nah ii ibaki kuwa akiba, wakishindwa nao, basi, “Fyekelea mbali”.



6 COMMENTS:

  1. Upo sahihi kabisa,naunga mkono mawazo yako na naomba ujumbe huu uwafikie TFF na waziri wa michezo.Endapo tukashindwa kufuzu kocha atimuliwe Mara moja maana katuhujumu sana.

    ReplyDelete
  2. Ila tuseme ukweli ni kuwa hatutaweza kuwafunga Uganda Cranes

    ReplyDelete
  3. Safi sana umeeleza vizuri,pia mimi nachoona wachezaji nao kama hawana uchungu na timu wanagharamiwa sana ila hawajitambui

    ReplyDelete
  4. basi musitafute kocha. Sababu watanganyika nyote munaonekana ni makocha.short and clear watanganyika hamujui mpira bwana. muacheni Amunike apumue. Washakuja makocha wangapi kabla yake. Mumeenda huko AFCON?

    ReplyDelete
  5. Hayo ndo unasema leo hukumbuki makala yako ya nyuma abadaa uandike hivi ukaandika blah blah

    ReplyDelete
  6. leo umechambua kitu kinachoonekana na kutafsirika. Nakuunga mkono. Hatutakiwi pia kusubiri mechi ya Uganda, huyu Amunike ni heri aondoke mapema kabla hata ya hiyo mechi. Mechi inachezwa mwezi wa tatu mwaka 2019, muda wote anakaa anafanya nini na tayari ameshatupa kazi ngumu!. Aende tu.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic