December 7, 2018


Staa wa zamani wa Simba, Talib Hilal ameikubali kombinesheni ya mastraika watatu wa timu hiyo kuwa inatisha na kueleza ina ubavu wa kurudia maajabu ya mwaka 2003 kwa kutinga kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba imevuka hatua ya awali ya michuano hiyo baada ya kuitoa Mbabane Swallows ya Eswatini kwa jumla ya ma­bao 8-1 juzi Jumanne.

Simba itacheza na mshindi wa jana jioni kati ya Nkana Red Devils ya Zambia na UD Songo ya Msumbiji ambazo zilikuwa zinarudiana.

Simba ipo njia moja kusaka tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyofanya mwaka 2003 ilipoitoa Zamalek kwenye raundi ya tatu ya mtoano ambapo kipindi hicho ikinolewa na Talib aliyeshirikiana na mkenya James Siang’a.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Spoti Xtra linalotoka kila Alhamisi na Jumapili, Talib, ambaye alifanya makubwa Simba akiwa mchezaji na kocha kwa vipindi tofauti, aliifagilia timu hiyo kuwa ina mas­traika wa hatari Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na John Bocco.

Talib, ambaye ni kocha wa timu ya taifa ya soka ya ufukweni ya Oman, pia amemvulia kofia kiungo mshambuliaji Clatous Chama, ambaye anaamini ameongeza makali ya makucha ya Simba.

“Washambuliaji wa Simba wanatisha kwanza hata kwa maumbo yao halafu pia ni wafungaji wazuri, sioni sababu wasifike mbali kwenye mashindano ya Afrika.

“Unajua Simba iliweka historia katika mashindano ya kimataifa miaka ya nyuma kwa kuwa walikuwa na mas­traika wakali, kama unawakumbuka kina Abdalla Kibadeni, Zamoyoni Mogela, Malota Soma na wengineo,” alisema Talib, ambaye alicheza kama sentahafu wakati Simba ilipoifunga Al-Ahly ya Misri mabao 2-1 jijini Mwanza mwaka 1985.

“Huyu Mzambia anajua mpira aisee, yaani kwanza ana sifa kuu mbili moja ya kuwa na kipaji cha kuufanya mpira anavyotaka pamoja na kuwachezesha wenzake halafu na pili ni balaa katika kufunga,” aliongeza.

Mchambuzi mahiri wa soka nchini, Mwalimu Kashasha alisema; “Chama ni mchezaji ambaye anastahili kuja kwenye Ligi yetu kama mchezaji wa kulipwa,ana akili ya ziada ya mpira. Akiugu­sa mpira ana­kuwa tayari ameshafanya maamuzi zaidi ya matatu apige pasi nyuma, mbele au aukokote.”

“Ni mchezaji mwepesi kucheza na wenzake, anachezea miguu yote miwili na anacheza anavyotaka na ana jicho la kuona mbali…pasi zake ni hatari sana na anafanya maamuzi haraka sana, ni mgumu sana kukabika,” alisisitiza Kasha­sha. Katika mabao mawili ya juzi, Chama alilisifia la kwanza.

CHANZO: SPOTI XTRA

1 COMMENTS:

  1. Chama ni kifaa,mechi yake ya kwanza ya kimataifa ameonesha hana mchecheto na mabeki isipokuwa yeye ndie mwenye kuwatia mchecheto mabeki iwe nyumbani au ugenini. Ukiachana na uwezo wake katika kazi yake lakini kinachovutia zaidi kwa chama ambacho wachezaji wetu wengi wa kitanzania wanakosa ni kujitoa kwa ajili ya timu yaani ni mpambanaji hasa hata akifanya kosa anaonesha dalili ya kuomba msamaha kwa wenzake tofauti na wachezaji wetu wengi akifanya la kizembe anaweza kuishia kucheka au akakaushia kimya yaani hawaoneshi dalili ya kujutia kosa.Wachezaji wa Simba wakiendana na fighting spirit ya chama basi wanaweza wakawapatisha taabu sana wapinzani wao.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic