Na Saleh Ally
SIMBA imetuonyesha kuwa kweli ina kikosi kipana kwa ajili ya msimu wa 2018-19 ambao hakika bado haujafikia hata nusu.
Kwa haraka kama utauangalia msimu huu, unaweza kuona ni mambo rahisi. Lakini kwa timu kama Simba, lazima kuwe na mapambano ya kweli ambayo yatachukua muda mrefu.
Michuano ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho lakini Simba wanashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa na hata kama watatoka basi wanakwenda kwenye Kombe la Shirikisho la Caf ambako pia kazi ni ile ya kibingwa kwelikweli.
Maana yake, wanatakiwa kuwa na kikosi kipana ndiyo maana wakaweza kuanza na wachezaji 11 waliocheza dhidi ya KMC bila ya kuwa hata na mchezaji mmoja kati ya wale waliocheza katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nkana FC ya Zambia.
Baadaye waliingia baadhi kama Cleutos Chama na Meddie Kagere lakini bado ilionekana kikosi kile kilikuwa cha wachezaji wapya ambao nao walionyesha kiwango bora.
Kwa kifupi kwa asilimia kubwa, akiwemo mgeni kabisa, Zana Coulibaly raia wa Burkina Faso, walionyesha kiwango kizuri na kucheza katika ule mfumo wa Simba.
Wakati Simba wanafanya hivyo, naweza kuwazungumzia wachezaji watatu. Kwanza Said Hamis Ndemla, mchezaji huyu kinda Mtanzania ambaye hakika ni zawadi kwetu kama tutaacha ushabiki na kuendelea kuona anakua.
Pili ni Haruna Niyonzima, mchezaji mahiri katika kiungo kutoka nchi jirani ya Rwanda. Tunajua, Niyonzima akiwa APR na baadaye Yanga, hakuna ubishi ni mchezaji bora kabisa ingawa baadaye alikutana na misukosuko mingi baada ya kutua Simba. Tatu ni Mzamiru Yassin.
Ndemla ni mchezaji ninayemfahamu kitambo kidogo, huenda kabla ya mashabiki wengi wa Simba. Nilibahatika kumuona akiwa Ujerumani katika mashindano maalumu ya vijana akiwa na timu ya TSA kutoka Mwanza. Timu hiyo kutoka Tanzania ilibeba ubingwa na Ndemla alikuwa mmoja wa wachezaji walioacha gumzo kubwa.
Hata baada ya kujiunga na timu ya vijana ya Simba, dalili za ubora wa Ndemla katika soka uliendelea kujidhihirisha na kufanya kazi.
Sasa amekuwa akipambana kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha Simba ambacho hakika kina wachezaji wengine wengi bora na wamekuwa wakimuachia nafasi ya kukaa benchi kwa kuwa wanamzidi uzoefu.
Kama si uzoefu, basi Ndemla ana ubora wake unaomruhusu kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza na mimi binafsi naona ameiva.
Mtihani mkubwa ulikuwa juzi, kupewa nafasi ile ilikuwa ni mafuta ambayo yamechemka kama angekosea, basi angejikaanga. Kacheza vizuri na mwisho kafunga bao ambalo limeipa Simba nafasi ya kupata pointi zote tatu dhidi ya KMC.
Hivyo Ndemla amemuonyesha Simba anastahili nafasi licha ya kutokuwa na uzoefu wa wale wengine. Amemuonyesha kocha kwamba anapaswa kuaminika na hili ndilo linatakiwa kwa mchezaji anayeweza kupambana kwa ajili ya ubora.
Kwa upande wa Mzamiru Yassin, tumeona amepotea kitambo. Yeye alicheza kama namba sita, namba ambayo Simba walikuwa na mpango wa kuongeza mtu mwingine, lakini amedhihirisha yuko vizuri na anahitaji kucheza zaidi ili kufanya vema.
Mzamiru alikaba vilivyo, alisimama imara na ndiye alianzisha mashambulizi mengi akiyasukuma kwa Niyonzima. Hii pia ni sehemu ya weledi sahihi ya mchezaji kwa kuwa pamoja na kuendelea kukaa nje lakini hakuwahi kulalamika na badala yake akasubiri nafasi.
Hii pia inakwenda kwa Niyonzima, nani alisema amekwisha? Analo la kusema tena? Ameonyesha yuko vizuri na anahitaji muda wa kucheza zaidi na zaidi na hapo Kocha Patrick Aussems atakuwa amepata nafasi ya kucheza na kikosi anavyotaka.
Niyonzima alikuwa roho ya timu, utaona alipewa kitambaa cha unahodha na akaendesha timu sahihi, akatoa pasi ya mwisho ya bao.
Kama hiyo haitoshi, hata baada ya kuingia Chama ambaye wengi wamekuwa wanamshindanisha naye. Utaona wao wawili walitengeneza Simba ya aina yake ambayo iliamka na kuanza kucheza tena. Maana yake, Aussems kafaidika tena na kama atapata nafasi ya kuwatumia pamoja, uimara wa Simba utakuwa juu zaidi.
Wachezaji wote watatu, NIyonzima, Ndemla na Mzamiru, hakuna aliyewahi kulalama wala kupiga majungu. Mwisho wamepewa nafasi wameonyesha wanaweza. Huu ndio weledi kikazi na wameonyesha ni watu tofauti hivyo faida imebaki kwa Aussems kuwa ana kikosi kipana na hata kama mashindano ni mengi, bado kila kitu kwake, kinawezekana.
0 COMMENTS:
Post a Comment