December 18, 2018


Mshambuliaji wa zamani wa Nkana FC ambaye amejiunga na Al Hilal ya Sudan, Idriss Mbombo raia wa DR Congo, ameingia kwenye rada za mabosi wa Simba na muda wowote kuanzia sasa mchakato wa kumsajili utaanza.

Mbombo ambaye msimu uliopita akiwa na Nkana alimaliza ligi akiwa na mabao 20, amesajiliwa na Al Hilal kuwa mbadala wa Mtanzania, Thomas Ulimwengu aliyeachana na timu hiyo miezi michache iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti la Championi limezipata kutoka Zambia ambapo Simba ilienda kucheza na Nkana FC, ni kwamba mshambuliaji huyo amependekezwa na kiungo wa Simba, Claytous Chama raia wa Zambia.

Chama anamfahamu vizuri mshambuliaji huyo kutokana na msimu uliopita kucheza wote ligi ya Zambia. Chama alikuwa Power Dynamo kabla ya msimu huu hajatoa Simba.

Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, mshambuliaji huyo atajiunga na Simba pindi timu hiyo ikifuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika au mwishoni mwa msimu huu.

“Mbombo anaweza kusajiliwa na Simba kwa sababu Chama amesema ni mshambuliaji mzuri na anaweza kuwa msaada kwenye safu yetu ya ushambuliaji.

“Hivi sasa anacheza Al Hilal ya Sudan na msimu uliopita akiwa Nkana, alifunga mabao 20 na kushika nafasi ya pili kwa ufungaji.

“Tunasubiri tufuzu makundi ndiyo tumuongeze kikosini lakini hata hivyo tunaweza kumsajili mwisho wa msimu,” kilisema chanzo hapa Zambia.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wa Nkana waliozungumza na Championi, wamesema kuwa Mbombo ni bonge la mshambuliaji na kama angekuwepo kwenye mechi dhidi ya Simba, basi wangeshinda mabao mengi.

Ikumbukwe kuwa, Nkana na Simba juzi zilicheza mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika Hatua ya Kwanza na Nkana kuibuka na ushindi wa mabao 2-1. 

Timu hizo zitarudiana Jumapili ijayo na mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo. Viongozi wa Simba walipotafutwa jana kuzungumzia habari hii, simu zao za mkononi zilikuwa hazipatikani.

1 COMMENTS:

  1. Kama kweli Simba wapo serious waanze hata leo kumfuatilia huyo mchezaji kwani anaonekana ni mfanya kazi mzuri yaani anaijua kazi yake ya kutupia. Kama chama ndie aliependekeza basi wasiuchukulie ushauri wake kimzahahamzaha kwani kama mpishi wa forward ya Simba yawezekana kabisa kuwa ameshaona umuhimu wa kuingozea nyama forward ya Simba lakini kabla ya hata chama kupendekeza kuhusu fowadi wa ziada, wadau kadhaa walishashauri kwamba Simba bado inahitaji fowadi mmoja wa nguvu baada ya kuona mapungufu ya waliopo na hasa kama kweli Simba wana ndoto ya kweli ya kupeleka mtetemeko kwenye mashindano ya klabu bingwa Africa. Alhilal Sudani ambao Idris Mbombo anacheza wamechezea kichapo cha magoli matatu 3-1 na club African ya Tunisia hivyo wapo mguu mmoja nje wa kutokea kunako mashindano ya club bingwa.kweli usajili wa mchezaji wa kiwango cha kimataifa unagharama lakini ndio maana kuna fungu la maana la pesa kwa timu itakayoingia hatua ya makundi. Kazi ya Kahata kule Gormahia ya kenya juzi iliwalewesha club bingwa ya Nigeria Lobstar na kukubali goli tatu 3-1 pale kenya na kuwaweka wanaigeria hao katika hali
    ngumu ya kufikia hatua ya makundi. Wadau walimpigia sana debe kahata kusajiliwa Simba kutokana na uwezo wake kwenye safu ya kiungo. Ni matumaini yetu yakwamba viongozi kuwa wasikivu kuyafanyia kazi maoni ya wadau kwani ni watu wenye nia nzuri na maendeleo ya klabu.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic