JAMES KOTEI AFUNGUKA MAZITO KUELEKEA MECHI NA NKANA
Kiungo mgumu wa Simba, James Kotei, raia wa Ghana, amefunguka kuwa wamejisikia vibaya kupoteza mchezo wao wa kimataifa dhidi ya Nkana lakini wamepanga kujirekebisha watakapocheza nyumbani katika Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Simba ikiwa ugenini nchini Zambia ilipoteza mechi yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kukubali kichapo cha mabao 2-1. Kwa matokeo hayo, Simba wanahitaji kushinda bao 1-0 kwa ajili ya kujiweka katika nafasi ya kusonga mbele hatua ya makundi.
Kotei amesema kwamba matokeo hayo ya kichapo kwao yalikuwa mabaya kutokana na kujiandaa kushinda mechi hiyo ya ugenini lakini mwishowe wakajikuta wakifungwa hivyo kwa sasa akili zao wanazielekeza katika kushinda mechi ya nyumbani.
“Haya si matokeo mazuri ambayo tuliyatarajia, lakini tuna nafasi ya kujirekebisha katika mchezo wa marudiano nyumbani, tutakuwa imara zaidi,” alisema Kotei.
0 COMMENTS:
Post a Comment