AJIRA ya kocha wa Real Madrid, Santiago Solari itakuwa majaribuni wakati timu yake itakapoifuata Barcelona kwenye Uwanja wa Nou Camp kwenye mechi ya kwanza ya nusu fainali ya michuano ya Copa del Rey itakayopigwa Jumatano ijayo.
Mechi baina ya timu hizo mbili zenye upinzani wa jadi nchini Hispania hujulikana kwa jina la `El-Clasico’.
Miamba hii mara ya mara ya mwisho ilivaana kwenye `El-Clasico’ ya La Liga, ambapo Barcelona iliikung’uta Real Madrid 5-1 kwenye Uwanja wa Nou Camp, Oktoba 28, mwaka jana na kusababisha kutimuliwa kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Julen Lopetegui.
Baada ya kuondoka kwa Lopetegui ndio Santiago Solari akateuliwa kuinoa timu hiyo kwa muda na baadae alipewa ajira kamili.
Utakuwa mtihani mzito kwa Solari kwani kwa sasa Barcelona ipo moto ikinyanyasa kwenye La Liga na Real Madrid ipo kwenye harakati za kunyanyua kiwango chake baada ya kuyumba kwa muda mrefu.
Solari itabidi aandae mkakati mkali wa kumdhibiti staa wa Barcelona, Lionel Messi yupo vizuri katika kufunga na kutoa asisti.
Pia Barcelona itaongezewa nguvu na kupona kwa Ousmane Dembele, ambaye katika siku za karibuni ametokea kuwa tishio.
Solari kwa upande wake atakuwa anamtegemea zaidi Karim Benzema, ambaye ameanza kuliona goli katika siku za karibuni na pia nahodha wa timu hiyo, Sergio Ramos.
0 COMMENTS:
Post a Comment