February 19, 2019



BADO ganzi inazidi kuongezeka hasa kutokana na namna Ligi yetu ya Tanzania inavyoendeshwa bila kuwa na mpangilio ambao unaondoa ule ukakasi kwa wafuatiliaji hasa kutokana na upanguaji wa ratiba na mwendelezo wa viporo kwa baadhi ya timu.

Mpaka sasa ikiwa tayari mzunguko wa pili kwa baadhi ya timu umeanza huku bado kukiwa na timu ambazo zina viporo mkononi kwa zaidi ya michezo mitano jambo ambalo nadhani sio sawa hasa kwa wakati huu ambao tupo kutafuta mafanikio ya Soka.

Ukiangalia duniani kote kwa wenzetu namna ambavyo wanafanya licha ya timu zao kushiriki mashindano mbalimbali huwa haitokei timu kuwa na viporo zaidi ya mechi tano, jambo hili ni hatari kwa afya ya soka letu.

Mamlaka husika ikiwa ni pamoja na Bodi ya Ligi Tanzania inayofanya kazi chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) yapaswa ilitazame hili upya na kwa upekee kwani ni jambo la muhimu kuwa na ratiba bora.

Waamuzi wa michezo yote bila kujali ni Ligi Kuu Bara ama ile Ligi Daraja la Kwanza la Pili na la Tatu muhimu kufuata sheria 17 za mpira na kuzisimamia kwa usahihi.

Imeonekana maamuzi mengi yamekuwa ni ya upande mmoja hali ambayo inaua ile ladha ya soka na ushindani ambao ulikuwa unazidi kushika moto ndani ya ligi hivyo waamuzi wasikengeuke na kufanya mambo kwa shinikizo.

Wachezaji pia kazi yenu kubwa uwanjani ni kuona namna ambavyo mnapambana kwa kuzifuata sheria, mchezo wa mpira hauna maana ya kutumia nguvu nyingi uwanjani bali ni akili na mbinu ndio vinatawala.

Maana nimeona baadhi ya wachezaji wamekuwa wakigeuka mabondia ndani ya uwanja na kucheza rafu ambazo hazina maana hili sio sawa hasa kwa mchezaji ambaye anahitaji kupata mafanikio kupitia soka.

Nidhamu ndani ya uwanja na nje ya uwanja ipewe nafasi hali itakayofanya kila mmoja kucheza kwa upendo na hata akipoteza anaamini ilikuwa bahati mbaya kwani mpira ni mchezo wa makosa.

Mchezaji mwenye tabia ya kulipa kisasi ndani ya uwanja anatikiwa abadilike haraka kutokana na maana ya mpira wa miguu kutawaliwa na upendo na sio ngumi na lugha mbaya.

Viongozi wa timu niwakumbushe kuzingatia majukumu yenu mkiwa ni viongozi, sio kwa kuwa una nafasi basi unatumia vibaya madaraka inakuwa haipendezi.

Kila mmoja afanye kazi sawa na maelekezo yalivyo, ingawa hatujaskia kwa sasa kuhusu suala la upangaji wa vikosi ila ukweli unaonekana hasa kutokana na matokeo ambayo yanaendelea, Inaonekana kumekuwa na mchezo huo japo kimyakimya.

Itapendeza zaidi masuala ya ufundi akaachiwa mwalimu mwenyewe maana nimeskia hivi karibuni kuna timu zimefanya maamuzi kwa ajili ya wachezaji bila hata kocha kuwa na taarifa jambo ambalo linaonesha ni namna gani tunaanza kufeli kiasi.

Amani na iendelee kutawala katika kila sekta, inaaminika kwamba nchi yetu ni ya amani na upendo, asiwepo mtu wa kuvuruga amani iliyopo kwenye mchezo wetu wa mpira ambao unazidi kuleta matokeo chanya kila siku.

Malumbano kwa mashabiki hayafai kwani ni dalili mbaya kwa, mashabiki ni watu muhimu ila jukumu la kushangilia timu mwanzo mwisho ndio lao kuhusu matokeo hayo ni baada ya dakika tisini.

Chuki hazifai kwani tumeona baadhi ya mataifa mengi yakishindwa kuvumilia na kuamua kuumizana, mfano mzuri Misri ambapo tumeshuhudia timu zikifungiwa mashabiki kuhudhuria kwenye michezo yao ni matokeo ya chuki.

Upendo ukitawala kwa mashabiki na wachezaji utaendelea kuleta ule msisimko ambao tumekuwa tukiuona hata waamuzi pia wanapaswa wawe na upendo kwenye sheria zao kwa kufanya yale yanayofaa na sio kuamua kuikomoa timu fulani hili halitakuwa sawa.

Ukweli utabaki palepale kama haya malalamiko ya waamuzi yatachukuliwa poa italeta mtafaruku kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia na kusikia kwa baadhi ya ligi ambapo waamuzi wamekuwa wakipigwa na wachezaji ama kuzomewa.

Usawa inabidi uwepo kwa kila mmoja ambaye ni mwana michezo. Hilo linawezekana endapo kila mmoja atatimiza wajibu wake ipasavyo bila kutegea hasa kwa wakati sahihi na sio mpaka kusubiria kamati ya masaa 72.

Napenda nizikumbushe timu zote kwamba mzunguko wa pili ni wa lala salama na kila timu zinajua kwamba hakuna timu nyepesi inayokubali kupoteza pointi muda huu. Sitaki kusema kwamba ugumu wa mashindano ndo ufanye timu kutengeneza mazingira ya kutafuta urahisi hapana.

Ama kwa zile zenye viporo kuanza kutengeneza mazingira ya kununua mchezo hapana, kinachotakiwa ni kuendeleza juhudi na kucheza mwanzo mwisho ili kuweka ushindani wa kweli.

Ubora wa ligi utabebwa na ushindani ambao utasaidia kupatikana kwa bingwa halali na sio wa kuungaunga ambaye atapeperusha bendera kimataifa.Tunataarajia kuendelea kuona ushindani kwenye ligi Kwa timu ambazo zina viporo ni wakati wa kupangiwa na kumaliza kwa waki muda kwa sasa sio rafiki.




1 COMMENTS:

  1. Saleh Jembe kwa sasa unazungumza sana viporo vya msimu wa 18/19, haya ulitakiwa uyazungumze msimu was 16/17 ambapo pia Yanga ilikuwa inawakilisha taifa, Yanga ilikuwa na viporo lukuki lakini hukupiga kelele hizi tunazozisikia sasa hivi. Nategemea kwa sasa wanaotengeneza schedule ya michezo ya ligi watazingatia hitajio LA sasa.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic