February 19, 2019


WASHAMBULIAJI Wa Simba, Meddie Kagere na John Bocco, Jumamosi iliyopita wamefanikiwa kuandika rekodi katika Uwanja wa Taifa baada ya kuongoza timu hiyo kuibuka na ushindi dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Ndani ya siku tano, Bocco na Kagere wamefanikiwa kuiwezesha Simba kutoka kifua mbale katika mechi mbili ilizocheza, moja ikiwa ni ya kimataifa ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly lakini pia ile ya juzi ya ligi kuu dhidi ya Yanga.

Katika mchezo dhidi ya Al Ahly Februari 12, Simba ilishinda bao 1-0, bao hilo lilifungwa na Kagere kwa shuti kali dakika ya 64 baada ya kupokea pasi ya kichwa kutoka kwa Bocco. Bao hilo lilifungwa katika goli lililopo upande wa Kaskazini mwa uwanja huo.

Jumamosi iliyopita dhidi ya Yanga, Bocco na Kagere wakafanya kitu kama kile walichokifanya dhidi ya Al Ahly.

Katika mchezo huo, bao la Simba lilifungwa dakika ya 71 na Kagere kwa kichwa baada ya kupokea pasi kutoka kwa Bocco aliyopiga kwa mguu wake wa kulia.

Hata hivyo, bao hilo pia lilifungwa katika goli lilelile la upande wa Kaskazini la uwanja huo wa Taifa, likiwahusisha wachezaji walewale na kipindi kilekile cha pili.

1 COMMENTS:

  1. Utulivu wa Boko unaanza kuja taratibu. Kuwa ndani ya 18 sio kubutua tu, lazima uangalie kwanza kama kuna mwenzako ambaye ana nafasi nzuri zaidi yako ya kufunga. Vile ndivyo inavyotakiwa. Na manufaa yanaonekana sasa. Tamaa ya kufunga inatakiwa ikae pembeni, ushindi wa timu ni mkubwa zaidi kuliko ushindi binafsi wa kufunga sana. Matharani umepata nafasi 5 za kufunga halafu umekurupuka kubutua, katika hizo ukapata nafasi 2, lakini wapinzani wakifika langoni kwenu wanatulia na wanafunga magoli matatu. Msaada wako unakuwa ni upi hapo kwa timu!. maana wewe unakuwa umefanikiwa kufunga magoli mawili, sawa; lakini timu yako imefungwa 3. Maana yake pamoja na magoli yako mawili, bado hujaisaidia timu. Walau zile nafasi zingine 3 ulizopoteza kwa kubutua ungempa mwenzako pasi na akafunga, ungekuwa umeisaidia timu kupata ushindi na wewe umepata magoli yako mawili.

    Naamini Boko anaendelea kurejea katika ubora na umakini wake. Atangulize maslahi ya timu kwanza ndipo, nafasi ya kufunga huwa inakuja yenyewe tu. Nadhani hata jana ameona yeye mwenyewe ushindi ulivyo mnono dhidi ya Lyon, kafunga mawili, kaasist moja, mambo ndo yanavyotakiwa yawe.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic