February 18, 2019



Na Saleh Ally
WAKATI mashabiki wakifurahia au kuumizwa na matokeo ya mechi fulani, si kawaida kufikiria mengi ambayo yametokea katika mechi husika na hasa zile kubwa ikiwemo kama ile ya watani.


Mechi ya watani, Yanga Vs Simba imeisha na kumaliza ubishi mrefu wa takribani mwezi mzima. Wenyeji walikuwa Yanga na wamepoteza kwa bao 1-0 lililofungwa na Meddie Kagere, raia wa Rwanda mwenye asili ya Uganda.


Hakuna ubishi kwamba Yanga walikuwa na hofu kuu kuhusiana na mechi hiyo na hata mahudhurio yao uwanjani hayakuwa kama ambavyo imezoeleka na hii ni kwa kuwa tu hawakuwa wakijiamini kwamba wanaweza kufanya vizuri.


Mashabiki wa Simba walikuwa wanajiamini na kilichokuwa kinawapa hali ya kujiamini ni ubora wa kikosi chao na walitaka kuifunga Yanga ili kuituliza. Walitaka iwe hivyo kwa kuwa mashabiki wa Yanga wamekuwa wakiwazodoa sana na hasa baada ya kufungwa mabao 5-0 mara mbili katika Ligi ya Mabingwa.


Hii ni kawaida, Yanga lazima wawazodoe Simba kwa kuwa ndiyo watani wao na umekuwa ni utamaduni. Hivyo asilimia kubwa ya mashabiki wa Simba walikwenda uwanjani au walikuwa wakisubiri kuona Yanga inaadhibiwa kwa mabao 5-0 ili "kuwafunga mdomo."


Simba wana timu yenye wachezaji bora zaidi na hili halina ubishi lakini Kocha Mwinyi Zahera naona ndiye alikuwa msimamo wa nini cha kufanya kwa wachezaji wake ili waweze kupambana na Simba.



Kwa matarajio ya kawaida, ilikuwa inawezekana kabisa Yanga angalau kufungwa mabao 3-0. Lakini Zahera ameonyesha ni kocha anayeijua kazi yake baada ya kuwa amejipanga kuhusiana na mechi hiyo.


Pamoja na presha yote, Yanga wamepoteza mechi hiyo kwa idadi ya bao 1-0 tu. Lakini umeona wakati fulani wamewaweka Simba kwenye presha na mafanikio makubwa ya Yanga katika mechi hiyo zilikuwa ni dakika 45 za kwanza zilizoonyesha kuwa Zahera ni kocha mzuri hasa unapozungumzia ufundi.

Simba ilishambulia mara 12 katika kipindi cha kwanza, mashambulizi ambayo yalionyesha kuwa na madhara. Lakini Yanga waliweza kulinda, Zahera akahakikisha 4-4-1-1 aliyoanza nayo inafanya kazi kubwa, mbele akimbakiza Herietier Makambo pekee na ulinzi ukawa ni ule zaidi ya anaotakiwa kuupata mkuu wa nchi.


Zahera alianza mechi na mabeki watatu wa katikati ambao ni Shaibu Abdallah 'Ninja', Vicent Andrew 'Dante' na Kelvin Yondani lakini mbele yao, akaongeza kiungo mkabaji ambaye na Papy Tshishimbi ambaye hakuwa anatembea zaidi ya kufanya kazi ya kukaba.



Kwenye difensive Yanga walicheza kwa nidhamu ya hali ya juu, huku mabeki wao wakiwa hawapandi na muda mwingi wakawa wanachukua mipira na kuipeleka kwa viungo na mara chache kwa Makambo ambaye alionekana alipata mafunzo ya kutosha nini sahihi cha kufanya.


Makambo alitulia zaidi na mara nyingi unaona, mabeki wa Simba walilazimika kumfanyia faulo. Zahera alijua kama Makambo atakaa na mpira, wakati akiwasubiri wenzake, mabeki wa Simba lazima watakuwa na presha na kumfanyia madhambi.


Mabeki wa Simba wangekuwa na presha kwa kuwa wana mambo mawili. Kwanza ni kuzuia wasifungwe lakini kutaka kuchukua mpira wawape viungo na baadaye washambulizi ili wapate mabao maana waliamini kikosi chao lazima kiifunge Simba.


Presha hiyo, mara kadhaa wakafanya madhambi ambayo yaliwasaidia Yanga kupunguza muda wa mechi (kumbuka inapopigwa faulo, lazima dakika ipotee). Lakini ikawasaidia Yanga kupata uzalishaji wa mashambulizi na ndiyo maana licha ya kwamba walikaa nyuma muda mwingi, lakini wakapata mashambulizi nane langoni mwa Simba, mengi kati ya hayo yakizalishwa na kona ambazo zilikuwa mbili au mipira ya adhabu. 


Mipango ya Zahera inaonyesha alipanga kufunguka kipindi cha pili baada ya kufanikiwa dhidi ya Simba kipindi cha kwanza. Kawaida, timu inayoonekana itashindwa, inapovuka kipindi cha kwanza salama, basi ile iliyoamini itashinda inakuwa katika presha.


Hivyo Zahera aliingia kipindi cha pili akitaka kushambulia kwa kushitukiza kwa lengo la kutaka apate bao na baada ya hapo arudi na kulinda zaidi. Pamoja na kuwa na mipango mizuri, utaona kipindi cha pili kilianza kuwa kigumu kwake kutokana na timu.


Hapo nasema timu maana ndiyo unaanza kupata ubora wa kikosi. Kwa kuwa wachezaji unaokuwa nao wanaanza kuchoka na unatakiwa kuwa na benchi bora zaidi ambalo kama unaingiza wachezaji basi lazima wawe msaada.


Zahera alianza kulazimika kuingiza wachezaji akiwemo Mohammed Issa 'Banka' ambaye hakucheza muda mrefu na asingeweza kuwa msaada. Mwisho mbinu au mfumo alioutengeneza ukawa wazi, ukawa si imara kama kipindi cha kwanza ingawa mwishoni Yanga walitulia na kushambulia.


Nimejifunza kupitia Zahera kwa kuwa mechi alivyoipanga ilikuwa ni kama vile timu ya Tanzania inakutana na timu kutoka Misri. Alielewa wachezaji alionao na kuwatengenezea mfumo ambao utawalinda na hii ndiyo kazi ya kocha anayekijua kikosi chake. 


Ndiyo maana muda mwingi Zahera alijiamini na kusema wana nguvu ya kupambana na Simba jambo ambalo lilikuwa likitia hofu kwa kiasi fulani kwamba angeweza vipi kuizuia Simba ambayo inaweza kuwa rahisi kuzuiwa na timu ndogo lakini Yanga, kazi inakuwa ngumu zaidi.

Wachezaji wa Yanga pia wanapaswa kupongezwa kwa kuubeba mfumo, wamecheza katika kiwango ambacho baadaye kiliamsha matumaini kwamba hakuna kisichowezekana. Mwishoni, hasa kabla ya kufungwa na dakika takribani saba baada ya kufungwa walipoteana na hii hutokea katika mpira.



Zahera ameonyesha ni kocha anayeijua kazi yake, hasa kama utazungumzia suala la mfumo wa uchezaji na timu wanayokutana nayo. Tukubaliane, kama Yanga watasajili na kuwa na kikosi imara hasa, Mkongomani huyo, atasumbua sana msimu ujao, kama atakuwepo.

3 COMMENTS:

  1. kocha bora ni yule aliyesahinda tatizo Simba na Yanga mmoja wao akifungwa hataki kukubali Zahra aliingia na plan ya kupaki bus ndio maana kocha wa Simba alibadirisha mfumo kipindi cha pili

    ReplyDelete
  2. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  3. Alifanikiwa kupunguza idadi ya magoli ya kufungwa, hilo nami nampongeza. Ila mfumo wake wa juzi hauna tofauti sana na ule wa mechi ya mzunguko wa kwanza aliofanikiwa kupata sare tasa. Namshauri kuwa, anatakiwa ajiamini, Yanga ikifunguka, inaweza kufanya jambo kuliko ikipaki basi kama vile.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic