February 27, 2019





Na Saleh Ally
SIKU chache zimepita tangu litokee jambo moja ambalo halikuingia kwenye vichwa vya mashabiki wengi wa soka nchini lakini linaweza kuwa funzo kubwa baadaye.


Jambo hilo ni lile la watu walioitwa matapeli ambao walikuwa wakipita katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam wakiwaandikisha wanachama wapya wa Klabu ya Simba.


Watu hao waliokuwa wakiwaandikisha mashabiki hao kuwa wanachama, wameelezwa kutokuwa na idhini ya klabu hiyo, jambo ambalo linashangaza kidogo.


Kwamba, watu hao waliweza kukaa na kutafakari hadi mwisho kufikia kufanya jambo ambalo lilipata ushirikiano wa kutosha kwa kuwa walipata watu wengi sana waliokuwa tayari kujiandikisha.


Mashabiki wa Simba wamekuwa na hamu ya kujiandikisha kuwa wanachama. Kwa nini wanataka kuwa wanachama? Wanataka kuwa wanachama kwa kuwa wanafurahishwa na mwendo wa kikosi cha Simba katika michuano mbalimbali ukianza na Ligi Kuu Bara lakini pia Ligi ya Mabingwa Afrika.


Kumbuka Simba imefikia hatua ya makundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ambayo ni aghalabu kwa timu za Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki kufikia. Pamoja na kupoteza mechi mbili, katika mechi nne, Simba imefanikiwa kushinda mechi mbili, moja ikiwa ni dhidi ya Al Ahly, vigogo wa Afrika.


Katika mechi mbili, Simba wamefungwa dhidi ya timu ya DR Congo na Misri lakini wao pia wameshinda dhidi ya timu kutoka Algeria pia Misri. Hizi zote ni timu kutoka Ukanda wa Waarabu, yaani Afrika Kaskazini, sehemu ambayo soka limepiga hatua zaidi ya sehemu nyingine ya Bara la Afrika.


Simba lazima itakuwa timu inayohamasisha zaidi mashabiki, lazima itakuwa timu yenye ushawishi mkubwa kwa kipindi hiki ambacho pia wako katika hatua nzuri ya uwekezaji na ubadilishaji mfumo wa klabu hiyo.


Maana yake ni hivi, Simba kwa sasa ni lulu na kama unazungumzia biashara basi huu ndio wakati mwafaka kabisa wa kufanya mambo muhimu likiwemo suala la fedha kibiashara.


Kipindi hiki, kama utawashawishi wanachama wasio wazuri kulipa ada ya uanachama, basi watafanya hivyo mara moja. Lakini kama utakuwa unataka wanachama wapya, ni rahisi sana kupata kwa kuwa mwendo wa kikosi ni mzuri na matumaini ni makubwa.


Wanachama ndio nguvu ya klabu na hasa unapozungumzia suala la kuunga mkono kwa kuwa hao ndio wanakwenda kuwa waungaji mkono wa kikosi na klabu kwa ujumla.
Kama hiyo haitoshi, kuwa na wanachama wengi ni nguvu na msimamo unaojenga njia sahihi ya wapi klabu kwa ujumla inakwenda.

Wanachama ni nguvu ya klabu kwa kuwa kama utapata angalau milioni moja na nusu na milioni moja tu wakawa hai kabisa, kwa kila mwaka Simba itakuwa na uhakika wa kuingiza zaidi ya bilioni na ushee kupitia wanachama pekee ambao pia watakuwa msaada wa kuiunga mkono na kuishangilia.


Timu bila ya mashabiki wa kutosha au klabu bila mashabiki wa kutosha ni kupoteza muda. Sasa vipi hao walioitwa matapeli wameweza kuwa na akili ya kujua wakati mwafaka wa fursa wakati viongozi wa Simba wapo na hawaioni?
Kilichofanywa na hao matapeli ndicho kitu sahihi kilitakiwa kufanywa na uongozi wa Simba ambao umeshindwa kwenda na wakati!


Wakati watu wana furaha na kuamini zaidi, ndio wakati wa kushirikiana nao na kuwaeleza unachokitaka kwa faida yako na yao kwa kuwa inakuwa ni rahisi sana kukuelewa.


Ndio maana matapeli wakajua ni kipindi kizuri kwa wao kujiingizia kipato kwa kuwa uongozi wa Simba bado unaendelea kusubiri bila ya kukumbuka kwamba mambo ya mpira hayaeleweki. Leo vizuri na kesho haieleweki na mambo yanakuwa magumu.


Achana na hivyo, jiulize, kwa nini Msemaji wa Simba, Haji Manara ameamua kutangaza kwamba Simba kama klabu sasa hawatoi tena kadi za uanachama? Jibu liko wazi kwamba wameshitukia utoaji huo wa kadi bila ya utaratibu ambao wao waliuita "ujambazi".


Kwa mara nyingine, nimewaona Simba hawakuwa wepesi katika suala la ubunifu kwa kuwa baada ya kuchelewa mara ya kwanza, wamechelewa mara nyingine.


Nimefikiri tofauti na uongozi wa Simba ambao binafsi naona haukujikunjua kutafakari vizuri baada ya kutokea "tatizo" hilo ambalo bila ubishi lilisababishwa na uongozi kufikiri taratibu kwa kutoangalia fursa hadi walipokumbushwa na hao "majambazi" au matapeli.


Baada ya kujua kwamba kuna watu walikuwa wanafanya utapeli huo, walipaswa kuwadhibiti watu hao kwa kuwaelekeza wanachama wa Simba walio tayari kuingia kwenye uanachama, wapitie njia ipi sahihi.


Mfano, wangewaambia anayeshughulikia masuala hayo ya wanachama wapya anapatikana wapi na wapi na si kuzuia kabisa. Mashabiki wanapaswa kuwa wanachama, sasa vipi unawazuia? Labda useme kwa sasa Simba hawahitaji wanachama wapya au wanachama wapya wakiingia wanaweza kuwa tatizo kwao katika jambo fulani na kama ni hivyo, basi yatakuwa ni maajabu makubwa na kutakuwa na walakini.


Kusitisha kwao kumewadhibiti hao "majambazi" lakini kumekata kiu ya mashabiki kuwa wanachama, jambo ambalo Simba wanalihitaji sana na wanaamini hali hii ya "hamu ya kuwa mwanachama" itaendelea milele, jambo ambalo si sahihi hata kidogo.


Badala ya kusimamisha zoezi hilo, Simba watengeneze namna ya kuwawezesha mashabiki wake kuwa wanachama wa klabu halali kabisa, jambo ambalo halihitaji nguvu wala akili nyingi ya kujisifia.


Ninaamini Simba ina watu waelewa wengi wanaoweza kupita katikati ya mistari ya maandishi yangu na kuelewa ninachokielezea kwa faida ya klabu hiyo na wakayafanyia kazi pia kwa faida ya klabu hiyo.


4 COMMENTS:

  1. Safi sana umeliona hilo na umetoa ushauri mzuri naamini viongozi wetu watakaa na kulifanyia kazi!

    ReplyDelete
  2. Muandishi nakuunga mkono kwa tamko hilo na naomba lipokewe na litekelezwe kwa mikono miwili kwa kila anaehusika kwa Simba yetu kipenzi.Hongera kwa kumbusho ambalo ni la maana kubwa sana kwa kipenzi Simba yetu

    ReplyDelete
  3. Kwa upande wangu mimi bado naishangaa sana klabu yangu ya simba ambayo imeshindwa kabisa kuiona fursa ya kuandikisha wanachama wapya kwa kuwa klabu inafanya vizuri na mashabiki wametokea kuipendea kwa dhati ndani ya muda mfupi sana. Haji Manara nakushauri fanya haraka sana kuushauri uongozi kwamba popote pale simba wanapokwenda kucheza mpira lazima muhakikishe mnaandikisha wanachama wapya hata kwa kiingilia cha shilingi mia tano (500)tu.

    ReplyDelete
  4. Lakini pia mjue kwa upande mwingine yupo mwekezaji Mo. Kuingiza wanachama wapya inahitaji mipango na majadiliano na other stakeholders. May be ndo maana wamesimamisha ili kuja na utaratibu mzuri zaidi. Hata hivyo nakubaliana na maudhui ya mwandishi

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic