YONDANI AFUNGUKA KUHUSIANA NA KUUPOTEZEA MKONO WA AJIBU
BEKI mkongwe wa kati wa Yanga, Kelvin Y o n d a n i amefuta ukimya na kufungukia ishu yake ya kutopeana mkono na nahodha wake, Ibrahim Ajibu.
Hiyo, ikiwa ni siku moja tangu iibuke taarifa za wachezaji hao kutokuwepo katika mahusiano mazuri baada ya video kusambaa ya Yondani kukataa kumpa mkono Ajibu.
Kitendo hicho kilitafsiriwa na wengi kuwa Yondani ana kinyongo na Ajibu, baada ya kuvuliwa unahodha na mikoba yake kukabidhiwa kiungo huyo.
Tukio hilo la aina yake lilitokea wakati Ajibu akiwatambulisha wachezaji wake kwa mgeni rasmi wakati Yanga ilipocheza mchezo wake wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba juzi, Dar.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Yondani alisema hakuna bifu lolote kati yake na Ajibu huku akitaja uchochezi wa mashabiki ndiyo umesababisha minong’ono kuhusu tukio hilo.
Yondani amedai kuwa hakumpa mkono Ajibu kama masihara tu, kwa kuwa siyo utaratibu wa nahodha kushikana mikono na wachezaji wakati akiwatambulisha.
“Mimi Ajibu ni mdogo wangu na mara nyingi tumekuwa tukitaniana ndani na nje ya uwanja na hilo tukio la mimi kukataa mkono wa Ajibu nilijua ni masihara ananiletea, ndiyo maana nikakataa kumpa mkono.
“Kwa sababu Ajibu katika mechi zote za ligi ambazo tumezicheza hajawahi kutupa mikono wachezaji, yeye anaishia kututambulisha majina yetu na mgeni rasmi ndiyo anatupa mikono, hivyo nashangaa suala hilo linavyochukuliwa.
“Kama ningekuwa na bifu au chuki na Ajibu, basi nisingekuwa nampa ushauri na siyo huyo, wachezaji wengi wanafuata ushauri kwangu kutokana na ukongwe nilionao wakiwemo baadhi Samatta (Mbwana), Msuva (Simon) na Banda (Abdi), hivyo niwaondoe hofu mashabiki wa Yanga katika hilo, mimi sina ugomvi na Ajibu,” alisema Yondani.
Championi Jumatatu, lilimtafuta Ajibu kuzungumzia hilo simu yake iliita bila kupokelewa lakini taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ambayo haijathibitishwa kama ni ya Ajibu, inamnukuu hivi:
“Nahisi wenzangu walinishangaa kuwatambulisha kwa kuwashika mkono, mara nyingi huwa hatufanyagi hivyo, Yondani ni kaka yangu na siyo yeye pekee pia Dante (Andrew Vicent), Yondani alisita na kuniambia hii mpya. Sina shida na kaka yangu huyu, sisi ni wadogo zake na mengi tunajifunza kwake.”
CHANZO: CHAMPIONI
This comment has been removed by the author.
ReplyDeleteThis comment has been removed by the author.
ReplyDeleteTatizo la vyombo vyetu vya habari au baadhi ya waandishi na hata wapenzi wa soka la Tanzania wanakuza sana tukio....hebu tuiache hii tabia ya kulikuza jambo ili kutafuta vyanzo vya habari.....kama hamna habari acheni kuposti matukio ambayo hamna uhakika nayo....hili tukio linakuzwa tu....hakuna bifu lolote lililopo....hebu habari hii iishe tuendelee na mengine
ReplyDelete