Bondia nyota wa Tanzania, Hassan Mwakinyo amewasili mjini, Nairobi Kenya tayari kwa pambano lake la Kimataida dhidi ya bondia kutoka Argentina, Eduardo Gonzalez lililopangwa kufanyika Machi 23 kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta (Kenyatta International Conference Centre).
Mwakinyo kwa sasa ananoa makali yake chini kocha Tony Bellew kutoka Liverpool, Uingereza ambako alikuwa kambini chini ya ufadhili wa Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya SportPesa.
Mbali ya Mwakinyo, pia Bellew anamfundisha bondia Fatuma Zarika ambaye atapambana na Catherine Phiri wa Zambia katika pambamo la ubingwa wa dunia wa uzito wa Super Bantamweight wa Baraza la Ngumi za Kulipwa Duniani (WBC).
Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa Kampuni ya Sport Pesa Tanzania, Tarimba Abbas alisema kuwa bondia Mwakinyo atafanya mazoezi chini ya kocha huyo chini ya uwezeshaji wa kampuni yao.
Tarimba alisema kuwa mbali ya kampuni yao kuwezesha kambi ya Mwakinyo na Zarika, Pia Bellew amevutiwa sana na viwango vya mabondia hao na wanaamini kuwa watafanya vizuri katika pambano hilo.
Alisema kuwa mabondia hao wamepata mafunzo bora na ya kisasa kutokana na umuhimu wa pambano hilo.
“Wakiwa mjini Liverpool, Mwakinyo na Zarika walijiandaa vyema kwa kuwa wanajua ugumu wa mapambano yao. Kampuni ya SportPesa imeona umuhimu huo na lengo letu kubwa ni kuona mabondia hao wanapata matokeo mazuri na kuwafurahisha wadau wa ngumi za kulipwa katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Tarimba.
Alisema kuwa Gonzalez atawasili Kenya kesho (Machi 20) ambapo Ijumaa (Machi 22) mabondia wote hao watapima uzito kwenye hotel ya The Stanley.
Pia mabondia hao watatembelea ofisi za SportPesa na kufanya mahojiano kwenye vituo mbali mbali vya televisheni na redio mbali ya kula chakula cha jioni na wafanyakazi wa kampuni yao.
0 COMMENTS:
Post a Comment