MWAKILISHI CAF AWAVURUGA SIMBA
MWAKILISHI wa Shirikisho la Soka Afrika ‘Caf’ jana aliibuka kwenye mezoezi ya Simba yaliyokuwa yakifanyika kwenye Uwanja wa Boko Veterani jijini Dar. Simba leo itacheza na TP Mazembe kwenye mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Katika mazoezi hayo yaliyoanza saa 10 jioni, mwakilishi huyo wa Caf alifika mapema na baada ya Simba kufanya mazoezi kwa dakika 15 akawataka waandishi na mashabiki waliokuwa wakifuatilia mazoezi hayo kutoka nje ili Simba waendelee na majukumu yao.
Hata hivyo ilikuwa ngumu kutokana na mazingira ya uwanja kuwa wazi hivyo kusababisha mwakilishi huyo kuripoti kwa meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu ambaye naye alisema ni ngumu kuwatoa kutokana na hali halisi ya uwanjani hapo.
Baada ya kujibiwa hivyo mwakilishi huyo alianza kupiga picha mashabiki na waandishi picha za video na mnato baadaye alionekana akitoa maagizo kwa Rweyemamu.
Kwa mujibu wa kanuni za Caf, waandishi wanaruhusiwa kuangalia mazoezi ya timu kwa dakika 15 pekee na baada ya hapo wanatakiwa kuwapisha wachezaji kuendelea na majukumu yao.
0 COMMENTS:
Post a Comment