POGBA ATAKA BILION 1.5 MAN UNITED
MANCHESTER United ipo tayari kuanza kufanya mazungumzo ya mkataba mpya na kiungo wake, Paul Pogba, ambapo kuna mahitaji ya mkataba wa kulipwa pauni 500,000 (Sh bilioni 1.5) kwa wiki.
Taarifa hizo zimekuja wakati ambapo Klabu ya Real Madrid ikiwa inadaiwa kuwa inapambana kumsajili mchezaji huyo.
Kwa dau hilo jipya inamaanisha kuwa atakuwa mchezaji ambaye analipwa kuliko wote katika Premier League sambamba na Alexis Sanchez wa kwenye timu yake.
Hivi karibuni Kocha wa Madrid, Zinedine Zidane alinukuliwa akisema kuwa anavutiwa na Pogba, kauli ambayo ilitokana na mchezaji huyo kusema kuwa naye anatamani kufanya kazi na Zidane na kuichezea Madrid kwa kuwa ni ndoto ya mchezaji.
Kauli za wawili hao ni ishara kwa kocha wa sasa wa United, Ole Gunnar Solskjaer kuwa ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha mchezaji huyo haondoki klabuni hapo.
Mpaka sasa Pogba amesaliwa na miaka miwili katika mkataba wake, lakini majadiliano ya mkataba mpya yanamaanisha yataongeza muda uliosalia na kubo-resha maslahi yake.
Imefahamika kuwa United ipo tayari kumpa mkataba mpya wa miaka mitatu ambayo itamfanya aendelee kubaki hapo hadi mwaka 2024.
Wakala wa Pogba, Mino Raiola anaamini mazungumzo kati yake na klabu yatafikia pazuri.
Kwa sasa Pogba analipwa pauni 300,000 (Sh milioni 909) kwa wiki, ni mchezaji muhimu kikosini na ndiye ambaye inaaminika anasaidia katika mauzo ya jezi.
Solskjaer anajiandaa kufanya mabadiliko kadhaa kwenye kikosi chake ili kuwa na timu ya ushindani, ambayo itawania mataji msimu ujao baada ya kuyumba msimu huu kuanzia ilipokuwa chini ya Kocha Jose Mourinho.
0 COMMENTS:
Post a Comment