April 6, 2019





Na Saleh Ally
HAKUNA hata shabiki mmoja wa Simba ataingia uwanjani na kusema hana hofu hata kidogo na mechi ya leo wakati Simba watakuwa wakishuka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kuivaa TP Mazembe.

TP Mazembe kutoka DR Congo inajulikana, ina uwezo mkubwa wa kifedha na mengi imeyafanya kwa matendo kama kuchukua ubingwa wa Afrika mara tano, jambo ambalo Simba hawajawahi kufanya hivyo hata mara moja.

Watakaokwenda uwanjani leo, wana hofu lakini lazima watakuwa na matumaini na hii itatokana na walichowahi kukiona, kwanza ni ukubwa kama wa Mazembe, Simba wamecheza na timu kadhaa za aina hiyo. Lakini uwezo wa kufanya vema, kwa kuwa ilikutana na timu zinazotia hofu na ikafanikiwa kufanya vizuri.

Hofu na matumaini ndiyo njia ya kwanza Uwanja wa Taifa na itaendelea kutawala hata kabla ya mchezo lakini baada ya hapo itakuwa majibu sahihi maana si jambo la kusubiri tena, badala yake kila mmoja atashuhudia kitakachokuwa kinaendelea uwanjani na kujionea kwa macho yake.

Hakuna ubishi, Simba itashuka dimbani ikiwa na tahadhari kubwa lakini hata Mazembe nao watafanya hivyo na wameonyesha tayari kuwa wana hofu na Simba, hawajatua nchini “kizembe” badala yake wamekuwa makini kwa kila kinachowezekana wakihofia kuwa wenyeji wao wamejiandaa vya kutosha.

Mazembe ni timu kubwa, hiki ni vizuri kukielewa lakini sahihi zaidi kuendelea kuamini hakuna timu kubwa isiyofungika na hili si hadithi kwa kuwa tumeshuhudia. Katika kuamini zaidi si vizuri kuona Uwanja wa Taifa ni “machinjio”, hivyo kila atakayetua hatoki badala yake kuona kila mechi ni mwanzo mpya na mapambano yanayopaswa kupiganwa bila ya kuangalia nyuma au historia.

Mechi zilizopita za Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018-19 na hasa katika hatua ya makundi zinaonyesha Mazembe wana uzembe hasa wanapokuwa katika viwanja vya ugenini. Aina ya uchezaji wao zaidi ni mashambulizi ya kushitukiza na kujilinda sana.

Wazembe ugenini:
Katika mechi hizo za ugenini, kwa asilimia zaidi ya 70 wameonekana kufeli kwa kutokuwa na mwendo mzuri na Simba wanaweza kuitumia nafasi hiyo kwa kuangalia mashimo ya kupita kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mechi ya kesho.

Mechi tatu za ugenini walizocheza katika hatua ya makundi, hakuna waliyoshinda na mbili walipoteza dhidi ya Ismaily ya Misri ambayo baadaye iliondolewa pamoja na Constantine ya Algeria ambayo iliwacharaza kwa mabao 3-0. Club African ya Tunisia, yenyewe ikawa sare ya bila kufungana. Kumbuka katika mechi ya nyumbani, Mazembe iliwachapa Watunisia hao kwa mabao 8-0.

Simba wanachopaswa kujikita na uchezaji wa Mazembe ugenini, waangalie uzembe wao na wautumie kama tundu la kupatia matokeo mazuri kabla ya mechi ya pili kule Lubumbashi. Kitu kizuri kinaonyesha Mazembe kufungika hadi mabao matatu ni jambo linalowezekana na Simba kufunga mabao matatu, si jambo gumu.

Safu ya ulinzi ya Mazembe si ngumu katika kiwango cha kutisha sana na nimeangalia mechi zao wanacheza kwa kushambulia kwa kushitukiza lakini wamepata usumbufu sana na timu zenye washambulizi wenye kasi kama Constantine.

Kasi yao ilikuwa kubwa na kuwalazimisha Mazembe kutumia muda mwingi wakijilinda. Utaona hata mabao waliyofungwa, yalikuwa ya haraka na kama mpira ungeendelea dakika 10 zaidi, huenda wangefungwa hata mabao matano.

Hawadhibiti hofu:
Safu yao ya ulinzi pia haina utulivu, wanaposhambuliwa sana wanaonekana kupoteza mwelekeo ndiyo maana Mazembe inaingia kwenye rekodi ya kuwa moja ya timu zenye kadi nyekundu hatua ya awali na hatua ya makundi.

Hii inatokana na kuwa na safu ya ulinzi inayojichanganya kwa urahisi hasa kunapokuwa na hali ya hofu. Maana yake kama Simba watacheza na kushambulia mfululizo kuna nafasi ya kuwachanganya na kufanikiwa kufunga au kusababisha wapate kadi nyekundu.

Kama unakumbuka, wakati Simba wanafunga bao lao la pili katika dakika za mwisho dhidi ya AS Vita Club, walikuwa wameshambulia mfululizo zaidi ya mara nne bila ya mafanikio. Kushambulia mfululizo kunatengeneza hofu nayo huzaa makosa. 

Kawaida unapoona timu inatumia mfumo bora wa ulinzi ambao ni vigumu kuuvunja, vizuri kutengeneza njia ya makosa kwa mchezaji mmojammoja (individual mistakes) ambazo huweza kuzaa mabao kawaida, kwa penalti au mipira iliyokufa.

Sasa ni mechi za mtoano, Mazembe wanaweza kuwa na ‘approach’ tofauti na ilivyokuwa na makundi lakini haiwezi kuwa tofauti sana kwa kuwa kwa kipindi kilichopita wakiwa wanacheza ligi pia hawawezi kuwa na muda wa kuubadilisha mfumo kwa zaidi ya asilimia 20. Hivyo watakuwa Mazembe wanaofanana na wale waliocheza na Constantine, Ismaily na Club African.

Simba umakini:
Wakati Simba wanapiga hesabu ya kuifunga Mazembe leo, lazima wawe makini na hili lilitokea katika mechi dhidi ya AS Vita na Simba wakaweza kurejea.

Mawazo ya Simba yalikuwa kufunga lakini wakakuta wanajisahau na kuanza kufungwa wao, imekuwa ikiwatokea mara kadhaa, jambo hawapaswi kulipa nafasi tena kwa kuwa kuna wakati wanaweza kufungwa na wapinzani wakabaki basi na kuzuia kila kitu.

Mechi ya kesho, kama ni mipango sahihi kabla ya mechi ya marudiano, Simba ni lazima washinde, hili halina mjadala na wakubali haitakuwa kazi rahisi.

Mputu:
Hivyo, wakati wanajilinda kuna wachezaji wa Mazembe wanapaswa kuwa nao makini kwa kuwa wanaweza kucheza ndani na nje ya mfumo kwa maana ya kuwa na ujuzi unaojitegemea ambao unaweza kuamua matokeo nje ya mfumo.

Tresor Mputu amekuwa akionekana kama ni “mzee”, jambo ambalo ni kosa kubwa kwa kuwa yuko katika kiwango kizuri na ni mmoja wa wachezaji wanaowania ufungaji bora wa michuano hiyo.

Katika hatua ya makundi amekuwa mwiba na mabao yake ni mipira iliyokufa lakini ana maamuzi ya kushitukiza, haraka na anashangaza kila wakati. Mwepesi miguuni lakini anaweza asifunge lakini ni bora zaidi katika pasi za mwisho zenye ufundi wa juu, jambo ambalo Simba lazima walisome na kuonyeshana.

Wachungwe pia:
Ukiachana na Mputu, Mazembe wamekuwa na jambo linalowafanya kuwa tishio, kuwa na wachezaji wengi wanaoweza kufunga. 

Kwamba hatafunga Mputu lakini wana wachezaji zaidi ya wanne wanaoweza kufunga na kuivusha au kuifanya timu yao kuwa katika nafasi nzuri ya kufanya vizuri na kweli ni wachezaji wakuchungwa sana. Kwa Simba, hii ni mechi ya bila makosa.

Elia Meshack ni hatari kama ilivyo kwa Kevin Zatu na Jackson Muleka ambaye mtindo wake ni kupiga mashuti ya kushitukiza na hasa anapokuwa katika msitu wa watu.

Wakongo wengi wana uwezo wa kupiga mashuti lakini pia kuruka mipira ya vichwa wapo vizuri. Jambo ambalo Simba walilidhibiti walipocheza na Vita mechi yao kwenye Uwanja wa Taifa, tofauti na ilivyokuwa kule Kinshasa. Ni lazima wafanye hivyo tena leo ili kuepusha matatizo.

Dakika nzuri:
Mabao mengi waliyofungwa Mazembe yanaonekana ni kipindi cha pili na kuwa na makosa mengi katika kipindi hicho inaonyesha ni kupungua kwa umakini unaoweza kuwa unatokana na kupungua kwa fiziki sahihi.

Mabao mengi wamefungwa kuanzia dakika ya 51, jambo ambalo Simba wanapaswa kulifanyia kazi ingawa vema wakaanza kwa kufunga kipindi cha kwanza angalau bao moja, ikiwezekana hata mawili ili kukilainisha kipindi cha pili.


Asikudanganye mtu, mechi hii inaweza ikawa laini sana kama Simba watazingatia na kuubana ubora wa Mazembe. Kama wakiwa makini na ubora sahihi, hawana sababu ya kuwazuia kushinda lakini wakiruhusu makosa, Mazembe nao wana watu wa kuamua matokeo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic