Na Saleh Ally, aliyekuwa Manchester
BEKI kisiki wa kati wa Liverpool FC, Virgil Van Dijk, anaishi katika nyumba ya kupanga inayomilikiwa na Kocha Mkuu wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer.
Van Dijk ni mpangaji wa Solskjaer, anaishi katika nyumba ya kocha huyo yenye thamani ya pauni milioni 4 (Sh bilioni 12) ambayo aliinunua wakati akiwa mchezaji wa Manchester United.
Baada ya kuondoka Manchester, nyumba hiyo iliyoingizwa sokoni ilishindwa kupata wateja hadi hapo beki huyo alipojiunga na Liverpool akitokea Southampton alipoamua kupanga na kuifanyia ukarabati kwa kiasi alichoamini ni kiwango anachokitaka.
Nikiwa England, nilisafiri mara nne kwenda na kutoka Manchester hadi Liverpool. Mara tatu ikiwa kwa treni na mara moja kwa gari. Kwa gari ni takriban dakika 45 kati ya miji hiyo miwili, treni hali kadhalika.
Nyumba anayoishi Van Dijk si mbali kutoka Manchester lakini bado si umbali mkubwa hadi Liverpool. Ni kama mwenda wa dakika 20 na ushee, hivyo unaweza kusema anaishi Manchester licha ya kwamba anaitumikia Liverpool kwa kuwa miji hiyo iko karibu kabisa.
Ukiwa mbali na Jiji la Manchester, unaweza kuona kama mambo yanakwenda vizuri sana lakini ukweli kuna hofu kubwa na moja ya siku hizo ni leo Jumatano wakati Manchester United inakutana na wapinzani wao wakubwa katika Ligi Kuu England, Manchester City.
Manchester United haipo katika mbio za ubingwa tena, mwendo wao ulitengemaa na sasa umekuwa wa kusuasua. Na sasa hofu yao kubwa ni safu yao ya ulinzi kama kweli inaweza kuwazuia washambulizi matata wa Manchester City ambao kwa msimu huu pekee katika mechi 34 wameshapachika mabao 87 na kuwa timu yenye mabao mengi zaidi ya kufunga.
Hofu ya safu ya ulinzi ya Manchester United ndiyo gumzo kubwa, mashabiki wanaona kikosi chao kinahitaji kufumuliwa katika sehemu kadhaa na wanaamini safu ya ulinzi inataka “mtu” hasa awe kiongozi kama alivyokuwa Rio Ferdinand wakati wa kocha Alex Ferguson.
Wengi wanaona anayefaa katika nafasi hiyo ni mchezaji wa Liverpool anayeishi Manchester na mpangaji wa kocha wao, Solskjaer. Wanamtaka Dijk na wanaona inawezekana vipi kocha wao ashindwe kuzungumza na mpangaji wake?
Mashabiki wengi wa Manchester waliozungumza katika mahojiano na gazeti hili kabla ya mechi dhidi ya FC Barcelona ambayo walipoteza kwa bao 1-0, walikuwa wana hofu namna wanavyoweza kumzuia nahodha wa Barca, Lionel Messi kwa kuwa ulinzi wao hawauamini.
Wanaamini mpangaji wa kocha wao anaweza kuwa msaada mkubwa na mwokozi wa hali waliyonayo ya kuwa wanakwenda Old Trafford wakiwa na hofu kubwa.
Wanavyowaangalia mabeki zaidi ya 100 walio katika Ligi Kuu England, Van Dijk anaonekana ni mlinzi na kiongozi. Beki ambaye anajua anafanya nini na msimamizi sahihi wa ulinzi.
Wanajua haitakuwa kitu chepesi kumng’oa Liverpool ambayo ilitoboka na kutoa kitita cha pauni milioni 75. Wao wanaona hata kama Manchester United itaweka rekodi ya usajili na kutoa zaidi ya pauni milioni 100, basi ifanye hivyo ili waondokane na mateso ya moyo ambayo hawakuyazoea katika kipindi cha katikati na kile cha mwisho cha kocha Ferguson.
Katika msimamo wa EPL, Liverpool iliyo kileleni imefungwa mabao 20 tu wakati Manchester United imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 48.
Wakati Manchester City inayokimbizana na Liverpool kubeba ubingwa inaongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi yaani ina safu matata ya ushambulizi, Liverpool wao wana beki imara na kisiki zaidi kwa kuwa wamefungwa mabao 20 katika mechi 35 wakati katika mechi 34, tayari Manchester City wametunguliwa mara 22.
Mashabiki Manchester United wanataka ukuta wa chuma uwakomboe na baada ya hapo, waanze mipango ya uchezeshaji na upachikaji mabao.
Hivi karibuni Solskjaer aliwahi kutania baada ya kupewa mkataba kuwa kocha mkuu wa United, kwamba angemuondoa beki huyo katika nyumba yake. Mashabiki hao wanaona, amuache aendelee kukaa na badala yake amshawishi kutua Old Trafford katika kazi ya kuisuka Manchester United mpya.
Yote yanawezekana lakini haiwezi kuwa kazi rahisi kutokana na kupanda kwa haraka kwa thamani ya beki huyo ambaye sasa ni kati ya mabeki wanaotazamwa karibu na kila timu kutokana na ubora wa kiwango chake ambacho kinazidi kupanda kila kukicha na thamani yake sasa, huenda ni kati ya mabeki wachache wanaoweza kununuliwa kwa bei ya juu kuliko washambulizi nyota duniani.
0 COMMENTS:
Post a Comment