April 13, 2019









Na Saleh Ally, Manchester
KUTEMBEA ni sehemu ya kujifunza mengi na mara nyingi unapoona jambo la kujifunza waunganishe na wengine ili mpate faida nyote.

Nakumbuka niliwahi kuandika kuhusiana na namna Uwanja wa Old Trafford unavyochangia kuifanya Manchester United kuwa na nguvu ya kifedha.

Manchester United imeendelea kutawala kwa utajiri na unaona ni mara chache imerejea na kuwa ya pili dhidi ya Real Madrid ya Hispania.

Hakuna ubishi tena kuhusiana na ukubwa wa Manchester United na si kwa England au Ulaya pekee, hapa unazungumzia dunia nzima na jambo hili pia si jipya tena.

Mashabiki wa Manchester United wanaokwenda kwenye Uwanja wa Old Trafford wengi wamekuwa ni wale wanaokwenda mara kwa mara. Lakini fedha zinaingia kwa wingi kupitia viingilio, pia mauzo ya jezi na vifaa vingine katika ‘Mage Store’, duka kubwa la klabu hiyo uwanjani hapo.

Fedha hizo ni zaidi ya bilioni 2 za Kitanzania ambazo huingizwa kwa siku moja tu ya mechi na wakati mwingine inaweza kuzidi hapo kulingana na biashara ilivyofanyika upande wa hoteli, duka na viiingilio.

Utaona Manchester United ina zaidi ya mechi 40 katika michuano yote kulingana na namna hali inavyokuwa kama timu inafanya vizuri au la.

Ukiachana na nini kinaingia, imekuwa ni jambo la kawaida kabisa kuhusiana na utamaduni wa timu hiyo na kama ukiingia ndani ya uwanja huo wakati wa mechi unaweza kujifunza mambo mengi sana.

Achana na biashara namna ambavyo zinaiendesha klabu hiyo na kuzidi kuifanya kuwa kubwa lakini wanachama na mashabiki wamekuwa wakiiendesha klabu hiyo wanavyotaka wao ifanye kwa kuwa wanajua wao ni tegemeo.



Mashabiki na wanachama wanajua wao ni tegemeo la klabu hiyo kama ambavyo klabu pia inaitegemea klabu yake kuendelea kufanya vizuri kupitia timu yao.

Wakati wa mechi kwenye Uwanja wa Old Trafford, mashabiki huwa wanaimba kuanzia mwanzo wa mchezo hadi mwisho, wanaweza wakapumzika muda mchache lakini upande mmoja ukaendelea kuimba bila ya kuacha.

Mashabiki hao wanapokuwa wanashangilia unaweza ukajifunza zaidi ya mambo matatu ambayo hayapo kabisa katika mpira wetu wa Tanzania.

Moja ushangiliaji wao unakuwa ni wa kiwango cha juu, kelele zao ni zile ambazo zinaweza kukutisha ingawa naweza kukiri kwamba tokea nimeanza kuingia viwanja hivi vikubwa vya soka, wale wapinzani wao wakubwa Liverpool, wanaongoza.

Pamoja na hivyo kelele za mashabiki hao wa Manchester United ndiyo msukumo wa kikosi chao kwenda mbele. Wanaowaonyesha wachezaji wanataka nini kutokana na pasi zao kama ni nzuri basi watapiga makofi na kuendelea kusisitiza kwa kelele mara kwa mara, mfano “hit it”, “take him” na kadhalika kuonyesha kwamba wangependa wachezaji wao kuwapita wapinzani au kuachia mashuti.

Wana nyimbo kadhaa zinazowafanya wachezaji wajue wakati umefika. Kwamba twendeni, twendeni muda bado. Wakati mwingine wanaweza kusimama takribani uwanja mzima wakiimba kwa nguvu wakati wanaona timu yao inashambuliwa sana na wasingependa ifungwe au wanataka ifunge.

Kitu cha ajabu ambacho nilikiona kuwa kinaweza kuwa kinafaa hata na mashabiki wa nyumbani, ni kulaumu. Uwanja wa Old Trafford mashabiki wake ni wakorofi hasa. Wanalaumu huku wanapiga makofi.

Wepesi kukasirika wakati huohuo, lakini wanaweza kubadilika wakati huohuo na kusifia kwa juhudi kubwa kupita kiasi utafikiri si wao.

Wakiona mchezaji anasema jambo, hapohapo wanamtukana tena kwa jumla utafikiri wameambiwa, lakini akigeuka na kufanya vizuri wanaungana naye na kuanza kumshangilia kwa nguvu wakati huohuo.

Kama ni mgeni unaweza usicheze Old Trafford au kucheza pale kwa mchezaji analazimika kujipanga na kujua yuko wapi na mashabiki wanaomzunguka ni wa aina gani kwa kuwa unaweza kushindwa kucheza.

Katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona, Luis Suarez, juzi alionekana kushindwa kuvumilia. Huenda amewasahau mashabiki hao kitambo kidogo.



Baada ya Barcelona kupata bao, mwamuzi wa pembeni alisema hapana. Suarez alishakwenda kushangilia katika kibendera, wakati unafanyika uhakiki wa bao au la, Suarez alisogea kwenye chaki na kuanza kuzozana na mashabiki wa Man United, akiwaonyesha kuwa wana midomo sana.

Jukwaa lote upande wa Alex Ferguson lilikuwa limesimama kumtukana na kumsuta Suarez ambaye alionekana kutoogopa hata kidogo. Kwani hata baadaye aliendelea kuwatolea ishara ya kuwa wanaongea sana.

Kwa mashabiki hao, kwao si jambo la hofu hata kidogo kwa kuwa wao wanachotaka kuona ni timu yao inashinda. Wanataka kuona mchezaji anacheza kwa kujituma na maarifa ya juu.

Ndiyo maana unapoangalia mechi za Manchester United, utaona wachezaji wa kikosi hicho hucheza kwa kujituma zaidi kwa kuwa waliowazunguka wanakuwa kama walinzi au wakaguzi wanaoangalia kiwango chao, yule anayeteleza, wanamshughulikia hapohapo.

Hii imekuwa na msaada kwa Manchester United hata inapokuwa na kiwango duni. Ndiyo maana sasa unaiona haina kikosi bora unachoweza kukilinganisha na jina Manchester United lakini kimekuwa kikiendelea kusonga mbele ndani ya jina na utamaduni huo wa Manchester, wenyewe wanasema “We are United”.

Historia ya Old Trafford: 
Huu ni uwanja wa United kuanzia mwaka 1910 ukiwa ni kati ya viwanja vya soka vya siku nyingi zaidi duniani.

Old Trafford unachukua mashabiki 74,999 ndiyo uwanja mkubwa zaidi kwa klabu nchini England na unazidiwa na Wembley tu ambao unachukua mashabiki 90,000, ukiwa unashika nafasi ya 11 kwa ukubwa Ulaya.



Mwaka 2009, Manchester United walitangaza kuwa watauongeza ukubwa kwa majukwaa kadhaa likiwemo lile la Sir Bobby Charlton na Sir Alex Ferguson Stand na kufikia mashabiki 95,000, ili uwe mkubwa kuliko Wembley.

Gharama hizo zilikuwa zinatajwa kuwa zitafikia kitita cha pauni milioni 100, lakini kutokana na ujenzi wa reli ambao ulikuwa unapita kwenye uwanja huo na ujenzi wa nyumba zaidi ya 50 Manchester United ilitangaza kuwa shughuli ya upanuzi itafanyika baadaye.

Hata hivyo kuna wengi walikuwa wakipinga upanuzi huo wengine wakisema kuwa kama jukwaa la Sir Bobby Charlton litaongezwa urefu kutakuwa na tatizo la mwanga wa kutosha kwenda uwanjani.

Uwanja huu umegawanywa kwenye majukwaa manne, Mashariki, Magharibi, Sir Bobby Charlton na Sir Alex Ferguson na mara nyingi yote yamekuwa yakijaa wakati wa mechi za United.

1 COMMENTS:

  1. Sasa kwa nini mashsbiki wa hapa kwetu wakimlalamukia kodogo mchezaji wao wanaonekana hawajui mpira nadhani ndio maana wachezaji wetu wanakuwa legelege kila siku.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic