May 22, 2019


KUFA kufaana! Ndivyo ilivyokuwa baada ya zoezi la bomoabomoa kufanyika juzi katika Kituo cha Daladala cha Mwenge jijini Dar ambapo zoezi hilo liliibua utapeli wa aina yake. 

Katika zoezi hilo lililoshuhudiwa na mwandishi wetu, wafanyabishara ndogondogo almaarufu Wamachinga walijikuta wakiangua vilio baada ya mabanda yao kubomolewa ili kupisha ujenzi wa barabara na kituo cha kisasa eneo hilo.

Wakati wafanyabishara hao wakililia mabanda na bidhaa zao, wateja wao walikuwa wakilalamika kutapeliwa vitu vyao kama simu walizokuwa wamepeleka kwenye mabanda hayo kwa ajili ya matengenezo. Baadhi ya wafanyabishara walisikika wakibishana na wateja kuhusu vitu vyao ambapo kisingizio kikubwa kilikuwa ni bomoabomoa.

“Mimi ninachotaka ni simu yangu, hayo mambo ya bomoabomoa hayanihusu, mnatumia bomoabomoa kama kigezo cha utapeli,” alisika mwanadada aliyekuwa akimlalamikia mmoja wa mafundi wa simu wa eneo hilo. Katika bomoabomoa hiyo, wananchi wengine walilalamikia kutapeliwa na mafundi wa viatu, mabegi na saa ambao nao walidai walipeleka kutengenezewa.

Baadhi ya wafanyabishara na mafundi walilieleza gazeti hili kuwa walijua zoezi hilo lingechelewa kufanyika hivyo kuacha mali zao na za wateja wao kwenye mabanda hayo. Walijiteta kwamba baada ya zoezi hilo kuanza vibaka nao walitumia mwanya huo kuiba vitu vyao na wateja wao.

Wafanyabiashara walioathirika na zoezi hilo ni pamoja na wauza mitumba, wenye vibanda vya mitandao ya kutoa na kuweka pesa mtandaoni na huduma nyinginezo. Wakati bomoabomoa hiyo ikiendelea, mteja mwingine alifika eneo hilo na kuchanganyikiwa ambapo alidai jana yake kuna fundi simu alikuwa na kibanda mahali hapo ambapo alimwachia simu yake amtengenezee, lakini alipofika alistaajabu kukuta banda limesambaratishwa na magreda na fundi huyo hajui jinsi ya kumpata.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo alikuwa mstari wa mbele kusimamia zoezi hilo ambalo lilikuwa likienda kwa amani huku polisi wenye silaha wakisimamia amani. Katika kuonesha kukomaa kwa diplomasia, Chongolo alijumuika na wafanyabiashara hao ambapo alikuwa akiwaelimisha umuhimu wa kilichokuwa kikifanyika ambapo nao walionesha kumuelewa.


Akizungumza na Uwazi, Chongolo alisema wafanyabiashara hao kwenye wilaya yake ni watu muhimu mno ndiyo maana ulipofikia wakati za kufanyika zoezi hilo aliamua kulisimamia mwenyewe ili kuepusha malalamiko.

“Hili zoezi linaendelea vizuri kama unavyoona ndugu mwandishi kwa maana kabla ya kufanyika tulishawapa taarifa mapema. Hata hivyo, pamoja kuwaondoa eneo hili tumewatafutia eneo lingine njia ya kuelekea Kiwanda cha Coca-Cola.

“Tumewaandalia eneo zuri na tumeshawawekea miundo mbinu mbalimbali ikiwemo choo cha kisasa na mambo mengine yatakayowafanya waendelee kufanya shughuli zao kwa amani. “Tatizo kubwa lililopo kwa wafanyabiashara ni hali ya mazoea wanapoondolewa eneo moja kupelekwa lingine wanakuwa na hofu ya kuwapoteza wateja wao,’’ alisema Chongolo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic