May 23, 2019




Na Saleh Ally
LEO ni siku nzuri ya burudani hasa kwa wapenda mpira hasa baada ya kutua nchini kwa kikosi maarufu nchini Hispania na barani Ulaya cha Sevilla.

Sevilla wako nchini kuivaa Simba na ziara yao imedhaminiwa na kampuni ya michezo ya kubeti ya SportPesa ambayo hii ni mara ya pili inaleta timu kubwa na maarufu baada ya Everton FC.


Watanzania wapenda soka watarajie burudani ya soka la kuvutia na Simba watalazimika kujipanga na vizuri wakijiachia ili kucheza soka la uhakika linaloweza kuwafanya Sevilla kujiuliza.


Hata hivyo, ubora wa Sevilla uko juu, hawa ni mabingwa mara tano Europa League lakini hii haitawazuia wao kutofungwa kama Simba watajipanga vizuri.


Hata hivyo, kocha mkuu wa Sevilla ni mmoja wa makocha watundu, anajiamini hakika anatumia mfumo mmoja anaoubadilika mara kwa mara.


Kocha Mkuu Joaquín Caparrós aliwahi kuifundisha Sevilla mwaka 2000 hadi 2005 kabla ya kujiunga na Deportivo la Coruna ya Kaskazini Magharibi mwa Hispania. Lakini baadaye alizifundisha timu kadhaa katika La Liga kama Athletic Bilbao, Mallorca, Granada na Osasuna kabla ya kuhamia nchini Qatar na kuanza kuinoa A Ahli kwa mwaka mmoja kabla ya kurejea tena Hispania na kuwa kocha wa muda wa Sevilla ambayo baadaye alikabidhiwa mikoba.


Amemaliza na kikosi hicho kikiwa katika nafasi ya sita na alijiunga nacho kama mwokozi baada ya kuwa hakika mwendo mzuri na inaonekana amepania kufanya vizuri zaidi msimu ujao.



Caparrós ameviambia vyombo vya habari vya Hispania kwamba wanakuja nchini kwa lengo kubwa la kujifunza. Yeye alipokuwa Qatar anasema aliona mambo mengi tofauti na ilivyo Ulaya. Anaamini akiwa nchini kuivaa Simba leo lazima atajifunza.


Mfumo wake wa uchezaji mara nyingi anavutiwa zaidi na anapendelea mfumo wa 3-5-2, mfumo ambao anautumia katika aina tofauti kuhakikisha anafanya vizuri katika mechi zake.


Katika La Liga msimu huu, Sevilla imeshinda jumla ya mechi 17 katika 38, imetoka sare nane na kupoteza 13 kutokana na kipindi kigumu ambacho kililazimika kufanya uamuzi mgumu kubadili mwelekeo wake.


Mfumo wa 3-5-2, umekuwa ni mwokozi wa Caparrós na mara nyingi, Sevilla ni moja ya timu zinaoipa kazi kubwa FC Barcelona zinapokutana kutokana na aina ya uchezaji na zaidi ni kwa kutumia mifumo hiyo wakati wa ushambuliaji lakini wakati wa ukabaji pia.


Kocha Caparrós anavutiwa zaidi na soka la kushambulia na kumiliki mpira mwingi na mashabiki kwenye Uwanja wa Taifa leo wategemee kupata soka la pasi nyingi na za uhakika kwa kuwa kikosi chake kitakuwa hakina presha.


Kawaida kama kunakuwa wanacheza mechi kubwa au ngumu audhidi ya timu ambazo wana hofu nazo, basi 3-5-2 inakuwa na tofauti kidogo kwa kuwa wanamiliki mpira lakini kwa kukaba zaidi badala ya kufunguka na kuwa wazi sana.


Kwa leo hakutakuwa na presha kubwa sana, lazima Kocha Caparrós atataka kuachia "mabawa" kila upande ili timu yake icheze zaidi na kutoa burudani kwa kuwa yeye ni kati ya makocha wanaopenda timu itandaze soka wakati ikifanya mipango.


Sevilla imekuwa ikiisumbua Barcelona kwa kuwa soka lake ni la pasi nyingi na kasi, hivyo kufanya aina ya timu hizo kufanana na kutengeneza ugumu. Ndio maana mara nyingi Barcelona imekuwa ikilazimika kubadili mfumo kila inapoivaa Sevilla.


Kawaida Sevilla inatengeneza mistari mitatu kulinganana mfumo, ule wa nyuma unakuwa na watu watatu, katikati watano na mbele wawili. Na ule msitari wa katikati unakuwa na Sergio Escudero, Sergi Gomez, Simon Kjaer na Jesus Navas ambaye ni nahodha wa kikosi hicho. Mchezaji ambaye aliwahi kufanya vema pia akiwa na mabingwa wa England, Manchester City.


Kjaer ni raia wa Norway, mzuri kwa krosi za chini na juu. Utaona, zaidi wanapiga pasi za haraka na yeye anakuwa na jicho la mbali kama ilivyo kwa Escudero ambaye ni nahodha namba tatu, kawaida huvaa jezi namba 18.

Msitari wa juu unabakiza watu wawili mbele lakini hii ndio Simba wapaswa kuichunga sana, maana mfumo wa Caparrós unaweza kubadilika kwa namna tofauti wakati wowote. 



Wale wanne wa msitari wa kati wakiongezeka kwa kasi, hasa kama ni shambulizi la haraka, wao wanakuwa sita mbele na kwa hesabu za kawaida za kimpira maana yake wanakuwa wengi zaidi ya wapinzani wakati wao wakiwa na advantage ya mpira.


Kwa kuwa Simba ndio mabingwa wa Tanzania, wanapaswa kuwa makini sana na Sevilla la sivyo wataliharibu "pilau" lao la ubingwa. Kama watacheza open football kwa muda wote wanaweza kutoa nafasi ya kufungwa mabao hata mawili au matatu ya kushitukiza.

Wale washambulizi wawili wa juu ambao ni Mholanzi, Quincy Promes ambaye huvaa jezi namba 21 na Wissam Ben Yedder, Mwarabu mwenye asili ya Ufaransa anayevaa namba 21, ni watu wa kuchungwa sana. Uzuri wa timu nyingi za Ulaya zenye ukubwa kariba huu wa Sevilla zinakuwa na wachezaji wanaojua nini cha kufanya kwa wenzao.



Viungo wa Sevilla wanajua bora wa Promes na Ben Yedder, kwamba wanataka mipira ya aina gani na wakati upi. Unaweza kuona timu fulani inacheza na mpira hata dakika nne tano, wakichukua Sevilla wanakwenda kufunga kwa kuwa aina ya uchezaji wao ni kwa umakini lakini ni direct football.


Lazima kutakuwa na burudani, maana unapoona Mohamed Hussein Zimbwe akipambana na Navas au Erasto Nyoni akihakikisha Ben Yedder hafurukuti kwa kuwa ni mchezaji mjanja, basi hiyo ndio itakuwa burudani yenyewe.


Watakaokwenda uwanjani wanaweza kuwa na nafasi ya kufaidi zaidi namna burudani itakavyokuwa na Simba wasitarajie Sevilla watacheza “kishkaji” maana Wazungu, zaidi wanajali rekodi zao.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic