May 1, 2019










Na Saleh Ally
UKIKUBALI kuishi ni kujifunza, utaishi kwa raha sana. Maisha yanavyokwenda ndivyo unavyojifunza mambo mengi na ndiyo hasa maana ya kuishi.

Tunaujua ushindaji wa Ligi Kuu England, namna ulivyo karibu kila mwaka, lakini kwa msimu wa 2018/19, si vibaya ukasema kuwa mambo yamekuwa matamu maradufu.

Ligi Kuu England hadi zimebaki mechi tatu, bado haujui nani atakuwa bingwa. Timu zinazochuana vikali kuwania ubingwa, zimebaki mbili, Manchester City na Liverpool na tofauti ni pointi moja.



 Tayari timu hizo mbili zimechukua nafasi mbili za ‘Top Four’ katika msimamo wa Ligi Kuu England na sasa nafasi zilizobaki ni mbili tu ambazo zinawaniwa na Tottenham, Chelsea, Arsenal na Manchester United.


Timu nne zinazowania nafasi mbili za Top Four ni vigogo hasa, timu ambazo zimekuwa na nafasi ya kuwa mabingwa wa England. Sasa hazina nafasi hiyo ndani ya nne bora ili ziweze kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.


Kama hiyo haitoshi, kuna ushindani mwingine tena wa kuwania kucheza Europa League, kila upande unataka kufanya vizuri kuingia katika saba bora. Kwa maana ya timu zitakazoshiriki michuano hiyo ya Ulaya ambayo inafuatia baada ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.



Angalia Everton wanatumia msuli kupambana ili kuwapiku Wolverhampton ambao nao mwishoni wamekuwa moto na usisahau, moja ya mechi zao wanakutana na Liverpool anayewania ubingwa.


Wiki chache zilizopita, nikiwa kwenye Uwanja wa Anfield wakati Liverpool ikijiandaa kuivaa Chelsea, sababu ya baridi, mashabiki hutoka majukwaani na kukaa sehemu ambayo kunakuwa na vibanda maalum vya vyakula, ni nyuma kidogo tu ya majukwaa kwa lengo la kukwepa baridi hadi mechi itakapokaribia kuanza.


Kilichonishangaza, mashabiki wa Liverpool walikuwa wakifuatilia kwa ukaribu kabisa mechi kati ya Crystal Palace dhidi ya Manchester City waliyokuwa wakitaka kuiona inapoteza na wao waishinde Chelsea na kujiweka vizuri kuwa mabingwa.


Morali ya mashabiki hao ilikuwa kubwa utafikiri wako uwanjani. Walitaka kila mchezaji wa Man City akosee na wakati mwingine wakaimba nyimbo kuibeza Man City.


Ilinishangaza sana kuona namna walivyo na hamu kuu ya ushindi kwa timu yao lakini ambavyo wangependa kwa juhudi kubwa kumuona mpinzani wao akipoteza mchezo wake na ubingwa utue Anfield kwa kuwa wanaelekea mwongo wa tatu sasa bila ya ubingwa wa Ligi Kuu England.


Ushindani huu unazidi kupanda kutokana na ushindani huru, wa haki na weledi kuchukua nafasi kubwa katika kila nyanja ya mpira.

Wachezaji na makocha wanaijua kazi yao, waamuzi wanajua wanachofanya hata kama wana sehemu ya kukosea. 


Wanaopanga ratiba ni watu wanaojitambua, wanaifahamu kazi yao na wamefanya mambo ambayo ni sahihi na kila kitu kinakwenda kwa mpangilio ulio sahihi.


Hii imeifanya ligi hiyo kuzidi kuwa na mvuto, kuwa gumzo na inayoaminika kuliko nyingine zote duniani. Kuna jambo la kujifunza na kupoteza makosa kadhaa ambayo hupunguza mvuto wa ligi zetu na hasa hii ya Tanzania Bara.


Wapangaji ratiba wa Ligi Kuu Bara, ninaamini ni wataalamu kutoka Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wamekuwa na walakini mkubwa wa umakini.

Wao wasipokuwa makini wanachangia kushuka kwa ushindani, hili wanapaswa kuliangalia. Maana Simba kuwa na viporo vipi, imechangia kushusha ile morali ya ushindani na ilikuwa inawezekana kuwe na nafuu.



Huenda pia wao walikuwa na nia nzuri lakini siasa ya soka nchini imewalazimisha kutokuwa na namna ya kuepuka hilo. Maana yake, TFF au TPLB upande wa viongozi, wajitathmini na kuhakikisha halirudii tena. Timu kuwa na viporo hadi zaidi ya vitano ni jambo linalodhoofisha ushindani.


Kuna mengi yanaweza kumalizwa na kuifanya ligi ya Tanzania ipande na kuwa na thamani kubwa. Lakini TFF lazima iumalize upungufu uliopo sasa na yanawezekana kutoonekana tena.

Mwendo inaokwenda nao EPL kwa sasa ndiyo hasa ligi kuu inavyotakiwa kuwa, ligi kuu inayoeleweka kitu ambacho tunakitaka kitokee na hapa nyumbani na kutengeneza ushindani sahihi unaojenga mvuto maridhawa utakaowashawishi mashabiki wengi zaidi kufuatilia.


Wadhamini wengi zaidi kujitokeza na mpira kuingiza fedha nyingi zaidi katika mchezo huo, hivyo kutengeneza ajira za uhakika na biashara zinazoeleweka huku serikali nayo ikikusanya kodi yake kwa faida zaidi.

1 COMMENTS:

  1. Saleh unakumbuka shuka alfajiri. Ungeanza kwa kujiuliza timu moja inachezaje mechi 11 nyumbani
    Usiangalie tulipoangukia angalia tulipojikwaa.
    All in all mawazo yako ni mazuri lakini yamechelewa.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic