MSHAMBULIAJI wa Simba, Mnyarwanda, Meddie Kagere, amesema kitendo cha uongozi wa timu hiyo kumsajili kiungo Francis Kahata, basi mashabiki wa timu hiyo watarajie moto mkubwa kutoka kwao kutokana na kujuana vizuri.
Kagere ametoa kauli hiyo zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kikosi hicho kwenda kuweka kambi nchini Afrika Kusini Juni 15, mwaka huu kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu na michuano mingine watakayoshiriki.
Simba imemsajili Kahata kutoka Gor Mahia ya Kenya kwa mkataba wa miaka miwili kwa dau la shilingi milioni 80 na mshahara wa Sh mil 8 kwa mwezi.
Kagere alisema kuwa, anaamini ujio wa Kahata utasaidia Simba kuendelea kufanya vizuri katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika kwani anajua kazi yake vizuri.
“Binafsi kwangu naona ni jambo zuri kwa mtu ambaye nilicheza naye Kenya amekuwa sehemu ya timu yetu katika msimu ujao wa ligi na michuano ya kimataifa, kwangu ni kitu cha kujivunia kwa sababu namjua vizuri Kahata.
“Kikubwa mashabiki wasubirie tutakachokifanya ndani ya uwanja kwa sababu lengo la kwanza ni kuhakikisha tunatetea ubingwa na uwepo wake naamini nitafanya kazi kubwa zaidi ya msimu uliopita kwa kufunga mabao zaidi,” alisema Kagere.
0 COMMENTS:
Post a Comment