July 29, 2019




NA SALEH ALLY
UTAKUWA umesikia zile taarifa kwamba Kocha Mwinyi Zahera hawezi kurejea tena nchini kwa kuwa anaidai Klabu ya Yanga fedha zake, hivyo ameamua kusisitiza hatakuja nchini. Lakini tayari Zahera ameshatua nchini.

Zahera yuko Morogoro ambako Yanga imeweka kambi yake kujiandaa na msimu mpya. Na imekuwa ikiendelea na maandalizi chini ya kocha wake msaidizi, Noel Mwandila.

Inawezekana kabisa kwenye maandalizi yao kuna upungufu kadhaa, lakini tumeona kwa kiasi chao wamejitahidi kuendelea na maandalizi hayo kuhakikisha wanamaliza vizuri kabla ya kuanza msimu mpya.

Niliposikia kwamba Zahera ameweka mgomo kuja, sijui kuna kocha mwingine anataka kujiunga na Yanga kwa kuwa tayari mambo yamekuwa magumu, sikutaka kukurupuka. Taratibu nilianza kutaka kujua undani na mwisho wake nikapata ukweli.

Kwamba Zahera alikuwa ameshazungumza na uongozi wa Yanga na kuomba muda kidogo. Kweli kuna mambo kadhaa ambayo walishakubaliana kuhusiana na maslahi yake na kadhalika.

Baada ya hapo nikajua Zahera alikuwa njiani kuja Tanzania lakini sikuwa nimepata uhakika mzuri. Kilichonishangaza ni baadhi ya watu ambao ni Wanayanga kutaka kulikuza sana suala la Zahera kuja nchini.

Nikajiuliza mara kadhaa, kwamba kwa nini Zahera liwe jambo linalolazimishwa kukuzwa. Taratibu nikaingia “chaka” na kugundua kuna Wanayanga hawakuwa wakitaka Zahera arudi ili uongozi uumbuke.

Hawa Yanga, ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa. Kwa sasa wanapaswa kujipanga kwa utulivu na akili zao waelekeze kuhakikisha wanafanya maandalizi bora.

Wale ambao hawataki Zahera aje, wanaotaka kusambaza maneno yanayoweza kusababisha mgogoro itawasaidia nini hasa. Nimekuwa nikisema mara nyingi, wachawi wa hizi klabu na timu zao ni wanachama na mashabiki.

Kuna watu wana maslahi yao binafsi na mambo si mazuri, hivyo wangependa kuona timu inakwama ili viongozi waonekane hawafanyi kazi na baada ya hapo uanze mgogoro ili wao wapate mlango wa uwani kuingia tena.

Kama utasikia Yanga inayumba kuanzia leo, kesho au mwezi ujao, basi wachawi ni Wanayanga wenyewe kwa kuwa kuna wale wanaoangalia maslahi yao binafsi na wanakerwa sana na utulivu.

Ndani ya Yanga kunaweza kuwa na utulivu lakini wako ambao hawafurahishwi huenda baadhi ya vitu ambavyo awali vilionekana ni rahisi kuvipata, sasa vimebanwa kutokana na udhibiti.

Hivyo wanachofanya wao ni kuanzisha chokochoko ili kufanya hali ionekane imeharibika sana, mambo hayana utulivu na mwisho yayumbe kabisa ili nao wapate nafasi ya kuingia.

Kama unakumbuka miezi kadhaa iliyopita kwa muda mrefu Yanga haikuwa na viongozi wa kuchaguliwa. Waliokuwepo ni wale wanaokaimu na hawakuwa na nguvu sana na mwisho wale wanaojiona wana nguvu kupita na kufanya hata yasiyo sawa ulikuwa ni mkubwa sana, sasa mambo yamebadilika.

Kubadilika huko, kunawakera wengi ambao leo si vigumu kwa kumpigia simu hata kocha au mchezaji na kumshawishi vinginevyo ili tu kuukwamisha uongozi.

Wanaofanya hivyo wapo na inawezekana wakajulikana kama wataendelea hivyo. Vizuri wakawa msaada au kukaa kando maana migogoro imekuwa haina msaada katika soka hapa nchini.


Waungwana wapenda maendeleo wanataka kuyaona maendeleo na Yanga itakapotulia, Simba wakiwa kwenye utulivu, hali kadhalika, Coastal Union na hata klabu zisizo na wanachama kama Mtibwa Sugar na nyingine. Basi nguvu na akili itaelekezwa uwanjani pamoja na kwenye masuala ya maendeleo. 

2 COMMENTS:

  1. Unafiki tabia mbovu sana.Ikiwa upande wa Simba mnafurahia hata kuwapa majina ya kuwapamba hao wanaoleta chokochoko.Mzee Kilomoni kuitwa "ninja"kwenye blogu yenu.Sababu ni hizo hizo za kukataa maendeleo ili "status quo" iendelee na wao waendelee kushibisha matumbo yao.Kuweni wakweli na zingatieni weledi.

    ReplyDelete
  2. Kilomoni na genge lake anavyofanya ni hayo hayo na mnashabikia kwa nguvu ya kufa mtu lkn ikifanyiwa Yanga aah wanakosea.Sijakusikia wala kusoma article kutoka kwako ya kuwakemea kina Kilomoni lkn nakumbuka kuna article uliwashauri Wana-simba kumpa ushirikiano mwekazaji MO.Kama kweli unaenda vilabu hivi viwe na maendeleo basi natarajia utajitokeza kumkemea na kumuelimisha Kilomoni na genge lake.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic