July 8, 2019





NA SALEH ALLY
TANGU uongozi wa Rais John Pombe
Magufuli umeingia madarakani ikiwa ni
awamu ya tano, suala la kupunguza siasa
ili kazi ifanyike, limekuwa likizungumziwa
sana.


Suala la siasa limekuwa tatizo kubwa
katika masuala mengi ya kiutendaji na
tunaona kuna mambo mengi sana sasa
yametekelezeka.


Yametekelezeka kwa kuwa zile siasa na
maneno mengi yamekuwa ni tatizo hasa
bila ya utekelezaji. Siasa nyingi hasa
katika sehemu ambazo si sahihi,
zinaharibu mambo.

Hili ndio naliona katika Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), viongozi wake huenda
wanashindwa kusema kwa hofu za
kisiasa, jambo ambalo wanapaswa
kutambua, mwisho wao ndio watabeba
mzigo.

Suala la timu ya soka ya taifa sasa
limekuwa linakwenda kisiasa sana,

naona wanasiasa au wapenzi wa siasa
wameingia na kutaka kufanya kuwe na
ugumu ndani yake.

Tulizungumza suala la wabunge
kuishambulia timu ikiwa mashindanoni
kule Misri, kuwaita wachezaji hawana
afya kabisa na kadhalika.

Wakati timu ikiwa mashindanoni, wao
walipata nafasi ya kuiponda TFF
yenyewe kuwa ina uongozi mbovu na
kadhalika.

Yote haya tuliyazungumzia likiwemo
suala la kuangalia wakati mwafaka wa
kuzungumzia mambo. Maana TFF
isingekimbia baada ya mashindano.
Wangeweza kuambiwa hata baada ya
kwisha kwa mashindano yenyewe au
hao wachezaji wasingeweza kuboresha
afya yao ndani ya siku mbili, hivyo hili
nalo lingeweza kuzungumzwa kwa nia
bora zaidi badala ya zile tulizoona.

Leo tunaona mengi, kama yale ambayo
tunasikia kuna fedha za Taifa Stars
zimeliwa na taasisi iliyochangisha,
tunaendelea kusubiri ili tupate au
kupewa uhakika wa hilo.

Achana na hivyo, tunaona namna
ambavyo viongozi wanavyotaka
kuonyesha Emmanuel Amunike ni kocha
mzuri sana bila ya kujua kwanza
matatizo yake.

Awali nilidhani, viongozi wangekutana
na wachezaji kwanza ambao ndio
wazalendo wenyewe. Amunike hawezi
kuwa mzalendo zaidi ya wachezaji.

Ndio maana alipowatukana wachezaji,
wao kwa wao wakahimizana kizalendo
na kuendelea kupambana ingawa

wengine tayari walidondosha machozi
baada ya kudhalilishwa na kukatishwa
tamaa.

Wachezaji ndio walikuwa mashujaa,
wamepigana kwa kiwango chao na leo
wamerejea, taasisi ambayo
imekabidhiwa mpira inapaswa ipewe
nafasi ya kutathmini.

Tukubali kwamba kwa uzuri na ubaya,
kama wadau tunapaswa kurejea katika
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutaka
kujua walichofanya, walicholenga na
kadhalika.

Katika hili hatuwezi kuwafuata
wanasiasa na kutaka kujua imekuwaje.
Hivyo vizuri wakaiacha TFF ifanye kazi
yake, pale itakapofeli basi tuihoji
yenyewe na itakapofanikiwa tuipongeze
kwa kazi nzuri.

Kama TFF inaona Amunike ni bora,
tuachie na mwisho tuhoji matokeo.
Kama inaona hafai, iachiwe iwe huru
kuamua kuhusiana naye kwa kuwa ndiyo
inayomfahamu na ndiyo iliyomleta hapa
kama kocha.

Hakika kama tunataka kuendeleza soka
letu, Taifa Stars isigeuke nyenzo ya siasa
au ya kufurahisha nafsi za wanasiasa.
Badala yake tufuate njia sahihi na
tunajua, soka ni hesabu na mjumuisho
wake ni ufundi.

Vizuri wanasiasa wakatoa nafasi kwa
wahusika wa taaluma hiyo kufanya kazi
yao badala ya kuingilia kila sehemu.
Kuna sehemu za kiutawala nao
wanazijua wanaweza kushiriki kama
sehemu ya msaada.

Si kwa kuwa wanaweza kuingia kila
sehemu, basi wakaingia kila mmoja
akitamani kushindana na mwingine huku
wakijua kufanya hivyo wanaharibu njia

sahihi soka linapopaswa kupita.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic